Na Joyce Kasiki,DAR ES SALAAM
OFISI ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi imeeleza kuwa inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa walipakodi na wawekezaji kwa kushughulikia changamoto za kikodi kwa haraka, hatua inayochochea ulipaji wa kodi kwa hiari na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, Erastus Mtui, alisema maonesho hayo yanatoa nafasi kwa taasisi hiyo kuwafikia wananchi, kuwaelimisha kuhusu huduma zake na kupokea malalamiko pamoja na taarifa zinazohusu kodi.
Alisema ofisi hiyo, ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa takribani miaka miwili na nusu, ilianzishwa ili kuwapa walipakodi na wawekezaji sehemu huru ya kuwasilisha changamoto zao za kikodi na kupata suluhisho kwa wakati.
Mtui alisisitiza kuwa ukusanyaji wa kodi ni msingi wa maendeleo ya taifa, hivyo ni muhimu kwa walipakodi kutekeleza wajibu wao kwa hiari huku Serikali ikiendelea kuondoa vikwazo vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa wajibu huo.
Alieleza kuwa mchango wa ofisi hiyo unaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi imara kupitia mazingira bora ya biashara na uwekezaji.
Kwa mujibu wake, wananchi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao kwa kutembelea ofisi za taasisi hiyo, kupiga simu za bure, kutumia mfumo wa mtandao au programu ya Suluhu ya Kodi App, huku maandalizi ya huduma ya USSD yakiwa katika hatua za mwisho ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa watumiaji wa simu za kawaida.
Amesema tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo, jumla ya malalamiko 593 yamepokelewa na kufanyiwa kazi, ambapo malalamiko 340 yalitatuliwa ndani ya mwaka uliopita pekee.
Amewahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kufika kwenye banda la Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi ili kujifunza zaidi kuhusu huduma zinazotolewa na namna ya kuwasilisha changamoto za kikodi.
MWISHO






























