



Na Mwandishi wetu,Dar
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameiagiza Wizara ya Nishati kuongeza kasi ya kupanua mtandao wa usambazaji wa gesi asilia ili kukidhi mahitaji ya Taifa.
Amesema kwa kufanya hivyo kutawawezesha wananchi kupata nafuu ya gharama katika uendeshaji wa vyombo vya moto na matumizi mengine ya nishati pamoja na Serikali kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza mafuta.
Amesema hayo leo Februari 09, 2026 alipozindua kituo Mama cha Gesi Asilia Iliyosindikwa (CNG) cha Puma Energies kilichopo Salasala jijini Dar es Salaam. Ujenzi wa kituo hicho umegarimu takriban shilingi bilioni 13.
“Wizara ya Nishati pia endeleeni kuongeza kasi ya utafutaji wa gesi asilia ili iwe nishati ya kawaida ya maisha ya kila siku ya Mtanzania, Watanzania wote jitokezeni kwa wingi kutumia fursa ya uwepo wa gesi asilia iliyoshindiliwa”.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa uzinduzi wa mradi huo unaakisi utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nishati na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. “Vilevile, inaendana na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha rasilimali za nishati, hususan gesi asilia zinatumika kama kichocheo cha maendeleo ya viwanda, usafiri na uzalishaji wa umeme”.
Amesema mradi huo unaashiria hatua muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi, salama, nafuu na ya uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. "Kwa kufanya haya Puma Energies mmeunga mkono kwa vitendo jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuijenga Tanzania inayotumia nishati safi.”
Kadhalika Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo kuhakikisha uwepo wa sera thabiti, mifumo rafiki ya udhibiti, uwazi katika utoaji wa maamuzi na ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali na sekta binafsi.
“Serikali inathamini sana mchango wa Sekta Binafsi katika kutekeleza Miradi ya Maendeleo na utoaji wa huduma kwa umma, Serikali imeendelea kushirikiana na sekta binafsi katika ujenzi wa vituo vya gesi asilia iliyoshindiliwa”.
Waziri Mkuu amesema kuwa katika kipindi cha siku 100 za Rais Dkt. Samia madarakani, Serikali imewezesha upatikanaji wa majiko banifu 13,575 yenye ruzuku ya asilimia 85 na Mitungi ya LPG 28,653 ya kilo sita (6) yenye ruzuku ya asilimia 50. “Vilevile, Serikali imewezesha Taasisi 89 zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia na hivyo kufikia jumla ya taasisi 1,136.”
Naye Naibu Waziri Wizara ya Nishati, Salome Makamba amesema kuwa moja ya maeneo yanayokua kwa kasi katika matumizi ya gesi asilia ni sekta ya usafirishaji kupitia matumizi ya Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG), ambapo kwa sasa zaidi ya vyombo vya moto 15,000 nchini vinatumia CNG.
Amesema kuwa hadi kufikia Januari 2026, vituo vya kujazia CNG vilikuwa 11 ambapo 9 viko katika Jiji la Dar es Salaam, kimoja kipo Mkoa wa Pwani na kingine kipo Mtwara.
“Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi tumeweka mpango wa kuongeza idadi ya vituo kufikia 20 ifikapo Juni, 2026 hususani katikamikoa ya Morogoro na Dodoma, ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za CNG katika miji mikubwa na kwenye barabara kuu za usafirishaji”







No comments:
Post a Comment