



Na Joyce Kasiki, MBEYA
CHUO cha Ufundi Stadi (VETA) mkoa wa Mbeya kimeonesha ubunifu mkubwa katika teknolojia ya kisasa kwa kuja na mfumo wa mafunzo ya magari ya Hybrid yanayotumia mota za umeme, huku yakipunguza au kuondoa kabisa utegemezi wa mafuta.
Teknolojia hiyo imewasilishwa katika maonesho ya Wiki ya Vijana kitaifa, yakionesha mwelekeo mpya wa VETA katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya teknolojia duniani.
Mwanafunzi Adam Akyoo kutoka VETA Mbeya ameleza kuwa, mashine hiyo ya Hybrid imeundwa kwa kutumia mota maalum inayoweza kuzalisha umeme na kusaidia gari kusafiri hata pasipo mafuta.
"Faida kubwa ya mota hii ni kwamba inaweza kuendesha gari bila kutumia mafuta kabisa,inapunguza gharama za uendeshaji na kumrahisishia mtumiaji safari, hasa pale mafuta yanapokatika na sheli ipo mbali," amesema Adam.
Adam amehimiza vijana wa Kitanzania kutumia fursa zilizopo kupitia vyuo vya VETA ambavyo vinaendelea kuimarishwa na serikali ili kuwapa vijana ujuzi wa kujiajiri au hata kuajiri wenzao.
“Tuna 'mode' ya kujifunza kwa vitendo, kila mwanafunzi anapata nafasi ya kujua teknolojia inavyofanya kazi. VETA haitoi tu nadharia, bali inakuandaa kuwa mtaalamu wa kweli wa teknolojia ya kisasa,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Afisa Habari na Uhusiano wa VETA, David Mpondyo, teknolojia hiyo mpya ya magari ni sehemu ya juhudi za VETA kufundisha vijana ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la sasa.
“Tuko kwenye maonesho ya Wiki ya Vijana tukionyesha kile ambacho vijana wanafundishwa kwenye vyuo vyetu. Si wote wanaofika vyuoni, lakini kupitia maadhimisho haya, wananchi wanaweza kuona na kuelewa kile kinachotolewa na VETA,” amesema Mpondyo.
Ameongeza kuwa VETA kwa sasa ina vyuo 80 ambapo kuna chuo katika kila mkoa, na kwamba ujenzi wa vyuo vingine 65 unaendelea katika kila wilaya nchini, juhudi zinazoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi stadi kwa wananchi wote.
Mpondyo amesema pia kuwa VETA imeamua kuandaa vijana kwa ajili ya teknolojia ya magari ya umeme kwa kuwa magari hayo sasa yameanza kuingia kwa kasi nchini.
“Awali magari yote yalikuwa ya dizeli au petroli, lakini leo magari mengi yanatumia umeme,wateja wakipeleka magari hayo gereji, mafundi wengi wanayaharibu kwa sababu hawana ujuzi huo,ndiyo maana VETA imeamua kufundisha mfumo huu mpya kupitia 'mode' za kisasa,” amefafanua.
Mpondyo amesema, VETA inaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya teknolojia na ujuzi nchini, ikiwapa vijana wa Kitanzania fursa ya kuendana na mabadiliko ya dunia na kuwa sehemu ya nguvu kazi yenye maarifa yanayoendana na wakati .
.







No comments:
Post a Comment