MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajab Mabele akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya miaa 60 tangu kuanzishwa kwa JKT |
NA MWANDISHI WETU ,DODOMA
JESHI la Kujenga Taifa (JKT)
limeelezea mafanikio yake linapoelekea kutimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake
huku likitaja Moja ya mafanikio ni kuchangia katika Pato la Taifa kwa kutoa
gawio Serikalini kupitia Shirika lake la uzalishaji Mali la SUMA JKT.
Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajab
Mabele ameyasema hayo leo Machi 3,2023 wakati akizungumza na waandishi wa
Habari kuhusu maadhimisho ya miaka 60 ya JKT yanayotarajiwa kufanyika Julai 10
mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo Rais Samia Suluhu
Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi.
Meja Jenerali Mabele amesema SUMA JKT
,kwa nyakati tofauti limeanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji Mali na
huduma kupitia Sekta za ujenzi ,uhandisi na ushauri,sekta ya Kilimo,Mifugo na
Uvuvi ,sekta ya viwanda pamoja na sekta ya huduma na biashara lengo likiwa
kujiongezea kipato huku akisema hatua hiyo imesaidia kupunguza mzigo wa
kibajeti kwa Serikali wa uendeshaji wa shughuli za JKT ,miundombinu ya Makambi
ya zamani Serikali imekuwa ikiyaboresha pamoja na kuanziaha Makambi mapya
bila kuathiri majukumu ya msingi.
"Jeshi la Wananchi wa Tanzania
na Taifa kwa ujumla linajivunia
mafanikio ya JKT katika kutimiza Malengo yake kwa jamii na shughuli zake za
kiuchumi ambapo kutokana na umuhimu wake katika Taifa ,JKT limeweka utaratibu
wa kujitathimini wapi limetoka,lilipo na linapoelekea kwa kipindi Cha
miaka 10."
Vile vile ameelezea mafanikio
mengine ya JKT ni kupitia kilimo mkakati ambacho kilianzishwa kwa ajili ya
kuhakikisha JKT linajitosheleza kwa chakula huku akisema ili kufikia azma ya kujilisha wameanzisha kilimo
mkakati ambacho pamoja na changamoto za hali ya hewa hapa nchini ,lakini kwa
sasa hawategemei kununua mahindi wala mchele kwa ajili ya kulisha vijana na
kwamba mkakati wao ni kuhakikisha ifikapo 2024/2025 tunajilisha
na kwenye malengo hayo hatuna wasiwasi lengo hilo litafikiwa.
Kwa mujibu wa Meja Jenerali Mabele , kuelekea
maadhimisho hayo JKT litafanya shughuli za kijamii ikiwemo kuchangia damu
,kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ikiwemo hospitali
,upandaji wa miti ili kuendelea kuifanya
Dodoma ya kijani na kutoa msaada wa kibinadamu kwa wahitaji .
Aidha Meja Jenerali Mabele amesema
pamoja na utekelezaji wa shughuli zote hizo lakini pia JKT bado limeendelea na
majukumu yake ya msingi ya malezi ya vijana ,uzalishaji mali na Ulinzi limekuwa
likifanya maboresho mbalimbali ili kuendana na wakati pamoja na mabadiliko ya
satansi na Teknolojia
Kwa upande wake Mkuu wa Tawi la Utawala
wa JKT Brigedia Hassan Mabena amesema Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikiitumia
Taasisi hiyo kuhakikisha vijana wanapata uzalendo,ukakamavu,mafunzo ya
ujasiriamali,mafunzo ya ufundi stadi ambapo vyote kwa pamoja vinakwenda
kuwasaidia wao katika kujiajiri na kuendesha maisha yao.
Naye ,Mwenyekiti wa Kamati ya
Maandalizi ya Maadhimisho hayo Kanali George Kazaula amesema JKT limewaalika
wadau mbalimbali kuelekea maadhimisho hayo kwa lengo la kuhakikisha yanafanyika
kama yalivyopangwa.
No comments:
Post a Comment