NAIBU Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel akijibu swali Bungeni jijini Dodoma leo Mei 19,2023.
NA WAF- Bungeni Dodoma
NAIBU Waziri wa Afya Dkt.
Godwin Mollel amebainisha kuwa, asilimia 7 ya Watanzania wanaishi na ugonjwa wa
figo huku akiwataka wananchi kupima ugonjwa huo mara kwa mara ili kuepuka
madhara yake makubwa ikiwemo gharama kubwa ya matibabu yake.
Dkt. Mollel amesema hayo leo
Mei 19, 2023 wakati akijibu swali la Mhe. Asia Abdukarimu Halamga katika
Mkutano wa kumi na moja kikao cha 29, Bungeni Jijini Dodoma.
Ameendelea kusema kuwa, ugonjwa
huu, kwa kiasi kikubwa unahusishwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu,
ugonjwa wa kisukari na maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Amesema, Katika kujali afya za
Watanzania wakiwemo wenye ugonjwa wa figo, Serikali ya Rais Samia imetoa kiasi
cha shilingi Bilioni 290.9 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali
za mikoa, katika vifaa hivyo vipo vifaa vya matibabu ya kusafisha damu
(dialysis) kwa wagonjwa wa figo.
Aidha, Dkt. Mollel amesema,
Serikali ipo katika mpango wa kuona namna ya kupunguza gharama ya matibabu ya
figo kupitia huduma ya kusafisha damu ili wananchi wenye uhitaji waweze
kunufaika na huduma hizo, huku akiweka wazi kuendelea kuwatazama wasio na uwezo
kabisa kupitia njia ya misamaha.
Sambamba na hilo Dkt. Mollel
ameendelea kusisitiza kwa kuwataka Wabunge kuwa mabalozi wazuri wa kuiunga
mkono Bima ya Afya kwa wote kwani ndio suluhisho la kudumu la matibabu ya
magonjwa yote na huduma bora kwa kila Mtanzania kwa ngazi zote kuanzia zahanati
mpaka hospitali ya Taifa.
No comments:
Post a Comment