MBUNGE WA ITILIMA SILANGA NJALU (CCM) |
NA JOYCE KASIKI,DODOMA
MBUNGE wa Jimbo la Itilima Silanga Njalu (CCM) ameihoji Serikali kwamba ni lini itajenga madaraja matano katika Mito Galamoha , Isolo,
Nyagokolwa, Mbogo na Mhuze katika wilaya ya Itilima.
Aidha katika
swali la nyongeza mbuge huyo ametaka kujua kwa nini serikali isiweke fedha za
maendeleo ili wananchi waweze kujengewa daraja hilo.
Akiuliza
swali Bungeni jijini Mei 30 ,2023,Mbunge huyo pia alitaka Serikali ione umuhimu
wa kufungua barabara ya Makutano-Makulija-Supaloji
ambayo imebaki kilomita 51 tu .
Amesema
kufungua barabara hiyo kutarahisisha shughuli za kiutalii katika wilaya ya
Itilima.
Akijibu
maswali hayo Naibu Waziri,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Deogratius Ndejembi amesema,katika Mwaka wa Fedha 2022/23, Wakala wa Barabara za
Mjini na Vijijini (TARURA) iliajiri Mhandisi
Mshauri-Chuo cha Ufundi Arusha kufanya Uchunguzi wa kijiolojia katika mto Galamoha
ambapo kazi hiyo imekamilika kwa gharama ya Shilingi Milioni 35.
Aidha
amesema kwa sasa TARURA inaendelea na Usanifu wa Daraja hilo kwa lengo la kupata
gharama halisi za utekelezaji wa ujenzi wake.
Kuhusu Mto Isolo kwa Mwaka wa Fedha 2022/23, Serikali
imetenga fedha kiasi cha Shilingi Milioni 41 kwa ajili ya kujenga daraja la
Mawe Sehemu ya
kwanza ya
Mto Isolo ambapo ujenzi wa Daraja la pili katika Mto Isolo usanifu wake
utafanyika katika Mwaka wa Fedha 2023/24 kwa kutumia wataalam wa ndani wa
TARURA.
Kuhusu Mto
Mbogo Ndejembi amesema,Serikali imetenga jumla ya Shilingi Milioni 40 katika
Mwaka wa Fedha 2023/24 kwa ajili ya usanifu wa Ujenzi wa Daraja kwa tekinolojia
ya upinde wa Mawe lenye ukubwa wa mita 15 ili kupata gharama halisi.
Kwa upande
wa Mto Mhuze Naibu Waziri huyo amesema,umetengewa
Shilingi Milioni 30 kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kijiolojia ili kuwezesha kusanifu
kwa daraja hilo.
“Mheshimiwa
Spika, Ujenzi wa madaraja katika Mto Galamoha , Isolo, Mbogo na Mhuze utaendelea
baada ya kukamilika kwa usanifu ili kupata gharama halisi za ujenzi.”amesema
Ndejembi
No comments:
Post a Comment