Na Mwandishi wetu,Dodoma
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amewasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026 mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo ametaja mafanikio makubwa na mikakati kabambe inayolenga kukuza uchumi wa viwanda na biashara nchini.
Aidha hotuba ya Waziri Jafo imeonesha mwelekeo chanya wa ukuaji wa sekta ya viwanda na biashara nchini ambapo kupitia bajeti aliyoiwasilisha amesema, serikali inaendelea kujenga msingi wa uchumi wa viwanda unaoendeshwa na ubunifu, ushindani, na uendelevu wa masoko ya ndani na nje.
Akisoma hotuba hiyo Bungeni jijini Dodoma, Dkt. Jafo ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi 135.8 bilioni kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya wizara ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 93.9 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku shilingi bilioni 41.9 zikitengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Amesema kuwa sehemu kubwa ya matumizi ya kawaida ni mishahara ya wafanyakazi, inayofikia shilingi bilioni 75.8, huku bilioni 18.1 zikitengwa kwa matumizi mengineyo.
Jafo ametaja vipaumbele vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 kuwa ni pamoja na kuendeleza Viwanda, Masoko, na Maendeleo ya Watu.
Kwa mujibu wa waziri huyo , katika mwaka ujao, wizara yake imepanga kuendeleza juhudi za kuimarisha sekta ya viwanda kwa kuwezesha uanzishwaji wa viwanda vipya, kuendeleza viwanda vya kimkakati, na kujenga miundombinu ya viwanda vidogo na vya kati (industrial clusters).
Aidha, amesema kuwa wizara itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji, kuimarisha upatikanaji wa masoko ya bidhaa za Tanzania ndani na nje ya nchi, pamoja na kusimamia ubora na usalama wa bidhaa ikiwemo chakula na vipodozi.
Kuhusu uwanja wa biashara, wizara imepanga kuendeleza jitihada za kufungua masoko mapya, kurasimisha biashara mipakani, na kufanya utafutaji wa masoko ili kusaidia wafanyabiashara kufikia fursa zinazojitokeza.
Mauzo ya Bidhaa yavunja rekodi
Dkt.Jafo amesema,katika miaka minne iliyopita, Tanzania imepiga hatua kubwa katika mauzo ya bidhaa nje ya nchi ambapo alisema,
Mauzo katika soko la SADC yaliongezeka kwa asilimia 127.7, kutoka dola milioni 1,303.4 mwaka 2021 hadi dola milioni 2,968 mwaka 2024.
Katika soko la Afrika Mashariki (EAC) amesema, mauzo yalipanda kutoka dola milioni 1,161.2 hadi 1,163.8 mwaka 2024 huku jumla ya mauzo katika bara la Afrika yamefikia dola milioni 3,946.76 mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 61.2 tangu mwaka 2021.
Ametaja bidhaa zilizochangia ongezeko hilo ni pamoja na madini, pamba, kahawa, parachichi, saruji, sabuni, na bidhaa za kilimo.
AfCFTA: Tanzania yapanua wigo wa Biashara Afrika
Kwa mujibu wa Waziri Jafo, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zinazofaidika na Soko la Biashara Huru la Afrika (AfCFTA), ambapo hadi Machi 2025 nchi imefanikiwa kusafirisha bidhaa kwenda mataifa 18 ya Afrika kwa kutumia vyeti vya uasili wa bidhaa. Bidhaa hizo ni pamoja na nyuzi za mkonge, vioo, kahawa na mchele.
Soko la Kimataifa: Marekani na Umoja wa Ulaya
Waziri Jafo pia alieleza mafanikio ya Tanzania katika soko la Marekani kupitia mpango wa AGOA, ambapo mauzo yameongezeka kutoka dola milioni 33.06 mwaka 2021 hadi dola milioni 85.4 mwaka 2023 – sawa na ongezeko la asilimia 158.3. Bidhaa maarufu zilizouzwa ni nguo, kahawa na mbogamboga.
Kwa upande wa Umoja wa Ulaya (EU), mauzo yameongezeka kwa asilimia 38.5, kutoka dola milioni 891.5 mwaka 2021 hadi dola milioni 1,234.3 mwaka 2024. Bidhaa zilizouzwa ni pamoja na mazao ya chakula, madini, maua, na ngozi.
Vikwazo vya Biashara: Serikali Yashughulikia Changamoto
Katika juhudi za kuvutia biashara zaidi, serikali imefanikiwa kutatua jumla ya vikwazo vya kibiashara 70 kati ya Tanzania na nchi jirani, vikiwemo Kenya na Zambia.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo,hatua hiyo imesaidia kurahisisha biashara mipakani na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi kikanda.
No comments:
Post a Comment