Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima |
JOYCE KASIKI,DODOMA
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Dkt.Dorothy Gwajima amesema,matukio mengi ya ukatili yanayojitokeza hivi sasa hapa nchini huenda ni kutokana na jamii kukosa elimu sahihi ya malezi na makuzi walipokuwa watoto.
Akifungua mafunzo ya Sayansi ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto (SECD) jijini Dodoma yaliyokutanisha washiriki 79 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini Dkt.Gwajima amesema kupitia mafunzo hayo sasa yaende kubadilisha jamii katika vizazi vijavyo.
“Hivi sasa upo ukatili mwingi kwenye jamii kutokana na sababu mbalimbali pia ni sehemu na yatokanayo na jinsi gani ambavyo tuliwalea watoto wetu katika hatua za awali ikibidi tangu walipokuwa tumboni mpaka wanazaliwa.”amesema Dkt.Gwajima na kuongeza kuwa
“Tunaambiwa kitaalam kuwa katika hatua ambzo ubongo wa mtoto unakua kwa asilimia 70 ni kwenye miaka ya awali.”
Amesema,kutokana na mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo makundi mbalimbali juu ya sayansi ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto nchi inakuja kuwa na kizazi ambacho hakina changamoto zinazoonekana hivi sasa zikiwemo za matukio ya ukatili.
Dkt.Gwajima amesema,hatua ambazo hazikuchukuliwa katika malezi na makuzi ya watoto katika vipindi vya huko vinasababisha nchi kuchukua muda mwingi na gharama katika kupambana na matukio ya ukatili ambayo kwa namna ama nyingine inarudisha nyuma amendeleo ya nchi.
“Changamoto hizi tunazoziona sasa hivi na tunachukua muda mwingi sana kupambana nazo, ambazo kwa namna moja ama nyingine zinarudisha maendeleo nyuma,ni dhahiri hatua za malezi na makuiz zinazoanza kuchukuliwa hivi sasa ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto,zitaifanya nchi kuwa na kizazi ambacho kikiambiwa hiki siyo kitaelewa kwa urahisi pasipo kutumia nguvu nyingi sana.”
Waziri huyo ameushukuru Mtandao wa Malezi na Makuzi ya Watoto (TECDEN),Shirika lisilo la Kiserikali la Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (CIC) Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Nchini (UTPC) kupitia utekelezaji wao wa mradi wa ‘Mtoto Kwanza’ na kufanikisha kuwezesha wadau wengi kukutana na kupata mafunzo ya malezi na makuzi ya watoto wadogo kwa ajili ya kwenda kutoa elimu hiyo kwa jamii.
Vile viule ameishukuru Taasisi ya Agha Khan Development Network kwa kushiriki tangu uzinduzi wa Programu na mpaka sasa wameendelea katika utekelezaji wake.
“Serikali inatambua kwamba mafunzo haya ni fursa kubwa ya kipekee ya kuelekea kwenye kundi kubwa la wataalam watakaokuwa na ujuzi wa kutosha kwenye PJT MMMAM ,
“Ni imani yangu kubwa baada ya mafunzo haya tutapata watendaji wengi zaidi katika ngazi mbalimbali wenye utaalam wa sayansi ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto watakaoenda kuelimisha jamii ili ijue kwamba akikosea malezi katika umri wa awali anaweza kumpata mtoto ambaye siyo matarajio yake.”amesisitiza
Aidha Dkt.Gwajima amesema kupitia mafunzo hayo ushirikiano wa serikali na wadau wengine katika utekeleaji wa programu ya MMMAM utaimarika.
Vile vile amewapongeza waandishi vinara kwa kutoa machapisho zaidi ya 400 tangu programu hiyo ilipozinduliwa mwezi Disemba mwaka jana yenye lengo la kuelimisha jamii kuhusu suala zima la malezi na makuzi ya watoto wadogo huku akisema kupitia mafunzo hayo waandishi wataenda kuchapisha machapisho mengi zaidi na yenye ubora zaidi utakaoamsha ari ya wananchi katika malezi ya watoto wao.
“Kwa hiyo tutakuwa tunafuatilia na pengine mnaposema ‘score card’ hii iwepo hadi kwa wanahabari ilituwapate wanahabari wazuri wanaofanya vizuri na tuweze kushindanishwa na nchi nyingine katika uzalishaji wa habari nzuri,lakini hata waziri anapoenda safari zake anaweza kuwachukua hawa akaenda nao kwa sababu wanaweza kuandika habari nzuri zaidi kutokana na kazi wanayoifanya hapa.”amesisitiza Waziri Gwajima
Ametoa rai kwa Wataalam wa maendeleo ya Jamii,Ustawiwa Jamii na NGOs kuhakikisha baada ya mafunzo hayo,wanafuatilia juu ya sayansi ya malezi na makuzi ya maendeleo ya awali ya mtoto ipasavyo kwenye maeneo yeo ya kazi.
Pia amewataka kuwa mabalozi wa kuhakikisha jamii inayowazunguka inapata uelewa wa malezi na makuzi ya watoto wadogo ikiwa ni pmoja na kuhakikisha watoto wanapata lishe ya kutosha,ujifunzaji wa awali,uchangamshi,malezi yenye mwitikio na ulinzi na usalama wa mtoto ili watoto waweze kukua vizuri na kufikia utimilifu wao.
“Twendeni tukaeleze jamii kwamba katika umri huu wa kuanzia 0 mpaka miaka 8 ni muhimu kuwekeza kwa mtoto kwani ndipo ubongo wake unapokuwa kwa asilimia 70-80,zungumza na mtoto kipindi hicho ambapo ubongo wake unakua kwa kasi ,tukiyaweka mambo haya vizuri wanandishi wa habari watatusaidia kuyafikisha kwa wananchi.”
Aidha amesema,matukio ya ukatili kwa watoto yamezidi huku akisema zaidi ya watoto 11,000 wamekatiliwa,huku akisema,yakiachwa matukio ya kubakwa na kulawitiwa pia watoto wamekuwa wakifinywa na kupigwa vibao kupita kiasi na kuitaka jamii kuacha mara moja vitendo hivyo dhidi ya watoto.
Awali Mkurugenzi wa Mtandao wa Malezi na Makuzi ya watoto (TECDEN) Mwajuma Rwebangila aliiomba Serikali iendelee kuwaongoza katika katika utekelezaji wa PJT MMMAM hadi katika ngazi za mikoa na Halmashauri.
Naye Mkurugenzi wa Children in Crossfire (CIC) Craig Ferla,amesema kutokana na uzinduzi wa Programu ya MMMAM ,Tanzania imekuwa ni miongoni mwa nchi chache ambazo zimefikia hatua hiyo kwenye masuala ya MMMAM.
Amesema, CiC kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya MMMAM na TECDEN wapo tayari kuhakikisha utekelezaji wa Programu hiyo unafanyika kwa ufanisi mkubwa na kufikia ndoto zilizokuwepo wakati wa uaandaaji wa Programu hiyo.
Kwa upande wake Joyce Marangu kutoka Agha Khan University amesema,Mafunzo hayo ya Sayansi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (SECD) yanajumuisha katika ukuaji wa ubongo,kukabiliana na umahiri ,ikolojia ya utotoni,kuwasialiana na kujifunza na afya ya ukuaji.
Naye Victor Maleko kutoka UTPC ambao ni washirika katika utekelezaji wa Mtoto Kwanza unaowakilishwa na kutekelezwa na waandishi wa habari 26 nchi nzima.
“Waaandishi hawa walichaguliwa mahususi ,wana moyo wa kujituma na wakati Programu ya MMMAM inazinduliwa sisi tulikuwa tumeshaanza kufanya kazi hii ya kuhabarisha umma kwa ajili ya kuwekeza kwenye masuala ya malezi na makuzi na mandeleo ya awali ya mtoto Tanzania nzima tangu mwaka 2019 ,
“Na mpaka siku Programu ya MMMAM inazinduliwa story zaidi 1000 zilikuwa zimeshaandikwa Tanzania nzima ,ni juhudi za waadnishi hawa vinara wa masuala ya malezi na makuzi ya watoto,na tangu kuzinduliwa kwa PJT MMMAM mpaka sasa tayari habari zaidi ya 400 zimeshaandikwa.
Kwa upande wake mwakilishi wa washiriki wa mafunzo hayo Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Lindi Gaudence Nyamwihura amesema kwa kupitia mafunzo hayo watakwenda kuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu kwa jamii inazowazunguka.
No comments:
Post a Comment