Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknlojia |
Serikali yafungia shule ya chalinze
modern islamic kuwa kituo cha mitihani
Na WyEST,Dar Es Salaam
Serikali imeifungia Shule ya Awali na
Msingi Chalinze Morden Islamic kuwa kituo cha Mitihani kutokana na udanganyifu
uliofanyika katika Mtihani wa darasa la Saba uliofanyika Oktoba 5 na 6, 2022.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya
kufanyika uchunguzi kufuatia taarifa zilizotolewa na Mwanafunzi Iptisam
Suleiman Slim wa kituo cha Mtihani wa shule ya Awali na Msingi Chalinze Morden
Islamic akieleza kwamba alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati
akifanya mtihani wa somo la mwisho.
Akizungumza Jijini Dar es salaam
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema uchunguzi
uliofanywa na Kamati ya mitihani ya Mkoa wa Pwani na ule wa
wataalamu wa miandiko " Forensic" uliofanywa na Jeshi la
polisi umebaini ufanano wa miandiko kwa watahiniwa 7 wa shule hiyo .
Waziri Mkenda amesema kwa kuwa
kulikuwa na uzembe uliofanyika pamoja na kuifungia shule hiyo watumishi wa
Serikali ambao walikuwa wasimamizi wa kituo hicho watachukuliwa hatua za
kinidhamu huku akimuagiza Mmiliki wa shule ya Awali na Msingi ya Chalinze
Morden Islamic kuwafukuza kazi walimu wote waliohusika katika udanganyifu
huo.
“Kwa kuwa Shule hii ni ya
binafsi tunaifungia kuwa kituo cha mitihani na haitaruhusiwa kufanyia tena
mitihani, lakini pia mwenye shule hakikisha unawafukuza kazi mara moja waalimu
waliohusika na kama hilo halitafanyika nakuagiza Kamishna wa
Elimu futa usajili wa shule hiyo na kuifunga mara moja,”amesema
Waziri Mkenda
Aidha kufuatia changamoto hiyo Baraza
la Mitihani la Tanzania (NECTA) limefanya marekebisho ya namba za Mtihani za
watahiniwa husika ili kila mtahiniwa aweze kupata matokeo yake halali.
“Nakupongeza Mwanafunzi Iptisam wa
kuwa na ujasiri wa kutoa taarifa, tayari NECTA imefanya marekebisho hata kwa
wengine ambao wamefanyiwa udanganyifu kama huo. Natoa wito kwa wananchi na
wanafunzi wote ukiona mtu anafanya mchezo kwenye mitihani toa taarifa na
serikali itachukua hatua mara moja,”amesema Prof. Mkenda
Kwa upande wake Mzazi wa Mwanafunzi Iptisam, Suleiman Said ameishukuru Serikali kwa kufanyia kazi changamoto hiyo aliyoipata mtoto wake wakati wa kufanya mitihani yake ya kuhitimu darasa la Saba. Pia amevishukuru Vyombo vya Habari kwa kutoa taarifa hiyo na kuweza kuwafikia walengwa na kuifanyia kazi.