Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima akiagana na wanafunzi jijini Dodoma |
Na WMJJWM, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amewaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha Miongozo ya Uanzishaji na Uendeshaji wa Mabaraza ya Watoto na Madawati ya Ulinzi kwa Watoto yanawafikia watendaji wote hadi ngazi ya Mtaa na Kijiji.
Dkt. Gwajima ametoa agizo hilo alipotembelea na kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Makulu na Shule ya Sekondari Sechelela katika Kata ya Dodoma Makulu, Jijini Dodoma Oktoba 30, 2022 kwa lengo la kukagua utekelezaji wa uanzishaji na Uendeshaji wa Mabaraza ya Watoto na Madawati ya Ulinzi wa Watoto Shuleni.
Amesema miongozo na nyaraka ambazo kila mwananchi hususani watendaji wanatakiwa kuielewa ili kurahisisha utendaji, hivyo hazitakiwi kufungiwa ofisini.
"Hii ni nyaraka ya wazi, kila mtu anatakiwa aisome, kuanzia Mwenyekiti wa mtaa, kijiji hizi hazitakiwi kufungiwa kabatini" amesema Dkt.Gwajima
Ametumia wasaa huo pia kuzungumza na wanafunzi wa shule hizo na kuwataka kuyatumia vema mabaraza ya watoto ili kujilinda dhidi ya ukatili mahali popote.
Dkt.Gwajima ameongeza pia kwamba, Serikali inafanya jitihada nyingi kutokomeza ukatili dhidi ya watoto ikiwemo kuanzisha mabaraza ya watoto na madawati ya ulinzi yawasaidie kujadili changamoto wanazokutana nazo na kutoa taarifa za viashiria vya ukatili panapostahili.
Kwa upande wao wanafunzi wa shule hizo wamemshukuru Waziri Gwajima Kwa juhudi zake za kukabiliana na vitendo vya ukatili na kuwa mabaraza na madawati ya ulinzi yamewasaidia kupunguza changamoto nyingi hasa mimba za utotoni.
"Katika shule yetu Dawati
limetusaidia hasa watoto wa kike kwani kabla ya Dawati walikosa mahali pa
kusemea shida zao" amesema Irene Boniphace
Naye mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Sechelela Grace Shiri amesema madawati ya watoto shuleni yamewasaidia hata walimu na wanafunzi katika shule hiyo.
"Dawati la wanafunzi limewasaidia
kujitambua na kuweza kusema shida zao pale wanapopata ukatili ndani na nje ya
shule, kujua majukumu yao na walimu yametusaidia kujua kwa haraka matatizo yao,
wamekuwa wazi na wanaongozana wenyewe" amesema Shiri
No comments:
Post a Comment