Na
Mwandishi wetu -Morogoro
VIONGOZI
wa dini nchini wamehimizwa kuwaelimisha na kuwajenga vijana katika
maadili mema, kuwaepusha na maambukizi ya VVU na kudhihirisha jitihada za
pamoja kati ya Taasisi za dini na Serikali katika kulinda na kuhamasisha vijana
kutambua hali zao za maambukizi ya VVU na kupata elimu ya Afya ya Uzazi.
Kauli
hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na
Uratibu Dkt. Jim Yonazi katika ufunguzi wa Mdahalo kati ya Vijana
na Viongozi wa dini uliofanyika Novemba 29, 2023 mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya
shughuli mbalimbali zinazoendelea kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku
ya UKIMWI itakayofanyika Desemba Mosi mwaka huu.
Dkt.
Yonazi amesema kufanyika kwa mdahalo huo iwe chachu ya kuhamasisha
na kutetea mitazamo chanya katika kupinga unyanyapaa na ubaguzi kwa watu
wanaoishi na VVU na UKIMWI na kuwa na mkakati maalumu kuhakikisha kuwa Nyenzo
na Miongozo iliyopo inatumika ipasavyo.
“Takwimu
zinaonesha kuwa moja ya makundi yaliyo nyuma katika kufikia malengo
yaliyowekwa ya Sifuri tatu ni kundi la VIJANA. Hii ni kwa kuwa pamoja na
uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo
kwenye afua za VVU na UKIMWI, vijana wengi wenye umri wa miaka 15-24 hawajui
hali zao za maambukizi ukilinganisha na watu wenye umri mkubwa,”Amesema Dkt.
Yonazi.
Pia
ameongeza kwamba Katika kufikia lengo la sifuri ya maambukizo mapya kama nchi,
maambukizi mapya yameendelea kushuka mwaka hadi mwaka, akisema hadi sasa
takwimu zinaonesha kuwa takribani watu 54,000 waliambukizwa VVU mwaka
2021 nchini ambapo ni sawa na takribani watu 4,500 kwa mwezi au watu 150
kwa siku.
“Vijana wenye
umri wa miaka 15-24 ndio kundi ambalo linaonesha kuwa na kiwango kikubwa cha
maambukizo mapya, kwani katika watu wote wanaopata maambukizi mapya ya VVU kila
mwaka, takribani asilimia 35 ni vijana wenye umri wa miaka 15-24 (yaani katika
kila watu 10 wanaopata maambukizo mapya ya VVU watatu ni vijana wa umri huu na
takribani asilimia 74 ni wasichana,”Amefafanua.
Katika
hatua nyingine Katibu Mkuu huyo amebainisha baadhi ya changamoto zinazojitokeza
katika mapambano dhidi ya UKIMWI kwa vijana kuwa ni pamoja na baadhi ya
viongozi wa Dini kuwazuia watu wanaoishi na VVU kutumia dawa za kufubaza makali
ya virusi kutokana na imani kwamba maombi pekee au uponyaji wa kimiujiza pekee
ndivyo vinavyokubalika.
“Baadhi
ya watu wanaoishi na VVU huacha matibabu kutokana na mafundisho na matamko ya
baadhi ya viongozi wa Dini, Baadhi ya viongozi wa Dini kutotoa tahadhari ya
kutosha kuhusu mahitaji maalum ya vijana wanaoishi na VVU na changamoto
wanazokumbana nazo zinazohusiana na matibabu,” Ameeleza.
Vivile
Dkt. Yonazi ametoa rai kwa viongozi wa Dini akiwataka kutumia majukwaa
yao kutoa elimu ili kusaidia kuhamasiaha waumini na jamii ambao ni watoto,
vijana na watu wazima katika mwitikio wa UKIMWI hatua itakayosaidia
kuongeza uelewa katika jamii kuhusu ufuasi mzuri wa dawa na matibabu,
kuhamasisha upimaji na kwa baadhi ya wazazi ambao hawawaweki wazi watoto wao
ambao wapo kwenye matumizi ya dawa, na kusaidia katika mapambano dhidi ya
unyanyapaa na ubauguzi na ukatili wa kijinsia.
“Hii
itaiwezesha nchi yetu kufikia malengo ya TISINI NA TANO (95%) TATU ifikapo 2025
katika mapambano dhidi ya VVU na Asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU
wawe wamejua hali zao za maambukizo; asilimia 95 ya waliopimwa VVU na
kugundulika kuwa wana maambukizo watumie dawa za kufubaza VVU (ARV) na asilimia
95 ya watu wanaotumia dawa wawe wamefubaza VVU),”Amesema Dkt. Yonazi.
Ikumbukwe
maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani hufanyika kila mwaka ambapo mwaka huu
Kitaifa yatafanyika mkoani Morogoro Desemba Mosi mwaka 2023 chini ya kauli mbiu
isemayo “Jamii Iongoze Kutokomeza UKIMWI”