Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedct Ndomba akizungumzia kuhusu utekelezaji wa shughuli za Taasisi hiyo jijini Dodoma. |
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amesema Mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha inaijenga Serikali ya Kidijiti.
Mhandisi Ndomba ameyasema hayo jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji pamoja na mafanikio ya Mamlaka hiyo.
“Katika kuhakikisha tunaijenga Serikali ya Kidijiti, Katika kipindi cha miaka 10 ijayo, Mamlaka itaandaa na kutekeleza mikakati madhubuti ili kuimarisha zaidi utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kwa kuwa na Sehemu moja ambayo huduma mtandao zote zitakuwa zinapatikana. “alisema Mhandisi Ndomba
Pia alisema,ni lazima kuwa na uwezo wa kutumia teknolojia mpya zinazoibuka, hasa zile za akili bandia, sarafu za kidijiti na teknolojia za kifedha, ili kuwezesha maboresho ya kiutendaji katika Taasisi za Umma na utoaji wa huduma kwa Umma.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi pia ni lazima kuwa na vijana wa kitanzania wenye uwezo mkubwa wa ubunifu katika utekelezaji wa jitihada za Serikali mtandao na uzalishaji wa vifaa na miundombinu ya TEHAMA,Mifumo na miundombinu ya Serikali mtandao iliyo bora na imara zaidi.
Alisema,ili kufikia yote hayo katika kipindi kijacho, Mamlaka imepanga kushughulikia maeneo ya kipaumbele ambayo ni pamoja na kuendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi zote za umma.
Ambapo itapitia na kukagua miradi na Mifumo ya TEHAMA ya kimkakati, kisekta na kitaasisi ili kuhakikisha kuwa imetengenezwa na inatumika kwa kufuata Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo iliyopo na kushauri maeneo ya kuboresha na kufuatilia utekelezaji wake.
Ametaja maeneo mengine ya kipaumbele kuwa ni kupitia na kutathmini hali ya usalama wa Mifumo na Miundombinu ya Serikali Mtandao na kuzishauri Taasisi za Umma katika maeneo ya kuboresha, pamoja na kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha kuwa Mifumo na Miundombinu ya TEHAMA inafanya kazi wakati wote kwa ufanisi na usalama.
Kwa mujibu wa Mhandisi Ndomba ili kufikia azma hiyo pia katika kipindi hicho e-GA itaendelea kuunganisha Mifumo ya Taasisi za Umma kwenye Mfumo wa Serikali wa kubadilishana Taarifa,kuendeleza shughuli za tafiti na ubunifu katika matumizi ya teknolojia mpya za TEHAMA ili kuibua huduma mpya kwa umma na kuwezesha matumizi sahihi ya teknolojia mpya zinazoibuka.
“Kujenga mifumo tumizi ya Kisekta kwa kushirikiana na Sekta husika, ili kupunguza wingi wa mifumo na kuboresha utendaji ndani ya sekta na kuiwezesha kubadilishana Taarifa na mifumo ya sekta nyingine pale inapohitajika na kupanua uwezo wa Mtandao wa Mawasiliano Serikalini na kuufikisha katika Wilaya zote nchini ili kurahisisha utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao na kuwafikishia huduma wananchi wote popote walipo.