Na Joyce Kasiki,Dodoma
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema wizara hiyo imejiwekea vipaumbele 10 inavyotarajia kuvitekeleza katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 kwa lengo la kuboresha huduma za afya nchini.
Hayo yameelezwa leo Mei 13 ,2024 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipokuwa akiwasilisha hotuba ya mapato,makadirio ya matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Ametaja vipaumbele hivyo ni pamoja na Kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa,Kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa na vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Taifa, Kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini.
Vipaumbele vingine ni Kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga, Kuimarisha upatikanaji na uendelezaji wa wataalam katika Sekta ya Afya kwa fani za kati,ubingwa na ubingwa bobezi, Kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi nchini,
Kuendeleza na kusimamia afua za Tiba Asili na Tiba Mbadala.
"Lakini pia Kuimarisha upatikanaji wa huduma za magonjwa ya kuambukiza, magonjwa
yasiyoambukiza na magonjwa ya mlipuko,Kuimarisha huduma za afya ya akili, huduma za utengamao hususan kwa watoto, wazee na watu wenye ulemavu na Kusimamia Tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya,"alisema Waziri Ummy
Kadhalika alisema kuwa Kwa mwaka 2024/25, Wizara imekadiria kutumia kiasi cha Shilingi 1,311,837,466,000 kutekeleza vipaumbele hivyo kwa kutumia afua 89 katika Kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa ambapo kiasi cha Shilingi 117,611,588,304.00 kimetengwa zitakazotekeleza afua mbalimbali.
Ametaja afua hizo ni pamoja na Kuendelea kuimarisha utekelezaji wa afua za chanjo kwa kuwafikia watoto 3,117,564 wenye umri chini ya miaka miwili (2), wasichana 871,429 wenye umri wa miaka tisa (9) na wajawazito 3,298,437 (Shilingi 115,369,238,904.00) na kutekeleza afua za lishe ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhimiza unyonyeshaji na ulishaji sahihi wa watoto.
Alisema afua nyingine ni elimu ya lishe kwa jamii na kuimarisha Mpango wa kuongeza virutubishi kwenye vyakula ambapo ununuzi na usimikaji wa mashine 300 za kuongeza virutubishi (Dozifiers)utafanyika (Shilingi 1,607,700,000.00) na kimarisha utekelezaji wa afua za usafi na afya mazingira katika jamii, Mipakani, taasisi za umma na binafsi ikiwemo kutekeleza kampeni ya mtu ni afya awamu ya pili.
Huduma za afya ya uzazi ,mama na mtoto
Kuhusu eneo hilo Ummy alisema ,Wizara
imeendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu
(SDG 2030) ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia chini ya 70 kwa kila vizazi hai
100,000, vifo vya watoto walio chini ya miaka
mitano kufikia 25 kwa kila vizazi hai 1000 na vifo vya watoto wachanga kufikia 12 kwa kila vizazi hai 1000 ifikapo mwaka 2030.
Ummy alisema,katika mwaka 2023/24 Sekta ya Afya imefanya uimarishaji wa huduma mbalimbali zikiwemo huduma kabla ya ujauzito, huduma wakati wa uchungu na kujifungua, huduma baada
ya kujifungua, huduma kwa watoto, afya ya uzazi kwa vijana wa rika balehe, na huduma za masuala ya kijinsia.
Alisema,uwekezaji mkubwa ambao
Serikali ya Awamu ya 6 imeufanya katika eneo hili ni pamoja na utekelezaji wa afua mbalimbali vimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 80 kutoka 556 mwaka 2015/16 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, kupunguza vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kutoka 67 mwaka 2015 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1000, kupunguza vifo vya
watoto wachanga kutoka 25 hadi 24 kwa kila vizazi hai 1000 kwa mujibu wa utafiti wa TDHS ya mwaka 2022.
"Mwenendo huo wa kupungua kwa
vifo vitokanavyo na uzazi na vile vya watoto chini ya miaka mitano inaonesha kuwa nchi yetu ipo kwenye mwelekeo mzuri katika kufikia malengo ya kidunia ifikapo 2030. Hali ya vifo vitokanavyo na uzazi kwa nchi za Afrika Mashariki na zile zinazotuzunguka ni kama ifuatavyo; Uganda 189 (UDHS 2022), Burundi 494 (UN 2023), Kenya 530.
Kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
Alisema ,Wizara imeendelea kupanua huduma za kuzuia maambukizi ya
VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
kwa kujumuisha huduma za kuzuia maambukizi ya Kaswende na Virusi vya Homa ya Ini aina ‘B’ katika afua hizo.
Lengo la kujumuisha huduma hizo
pamoja ni kutumia rasilimali za kuzuia maambukizi ya VVU kutokomeza maambukizi ya Kaswende na
Virusi vya Homa ya Ini aina ‘B’ kwa watoto.
Takwimu zinaonesha kwamba, jumla ya vituo 7,830 sawa na asilimia 96 ya vituo 8,164
vinavyotoa huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto viliweza kutoa huduma za kuzuia Maambukizi ya VVU na Kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto.
Aidha alisema , jumla ya wajawazito 1,453,235 sawa na asilimia 97.4 ya wajawazito 1,492,931 waliohudhuria kliniki walipimwa VVU katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 ikilinganishwa na Wajawazito 1,627,685 sawa na
asilimia 98.9 ya wajawazito 1,645,417 waliopimwa katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23 Wajawazito 43,323 sawa na asilimia 2.98 ya wajawazito wote walibainika kuwa na maambukizi ya VVU kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 ikilinganishwa na wajawazito 47,475 sawa na
asilimia 2.85 waliobainika kuwa na maambukizi ya VVU kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23.
Kwa mujibu wa Ummy katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, wajawazito 38,951 sawa na asilimia 90 ya wajawazito waliobainika kuishi na maambukizi ya VVU waliunganishwa na huduma za matibabu ya dawa za kufubaza VVU (ARVs)
ikilinganishwa na wajawazito 43,208 sawa na asilimia 91 ya wajawazito 47,475 waliobainika waliunganishwa na huduma za matibabu ya VVU kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23.
Aidha alisema utoaji wa huduma kwa wajawazito unaenda sambamba na utoaji wa huduma kwa watoto ili kumkinga na maambukizi ya VVU kutoka kwa mama ambapo katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, jumla ya watoto 27,808 sawa na asilimia 80 ya watoto 34,998 waliozaliwa na akina mama wanaoishi na maambukizi ya VVU walipimwa vinasaba vya VVU katika umri wa miezi miwili ikilinganishwa na watoto 31,021 sawa na asilimia
79 ya watoto 42,788 waliopimwa vinasaba vya VVU.
Huduma za Lishe
Katika eneo hilo Ummy alisema Wizara imeendelea na utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa pili wa Kitaifa
wa Lishe 2021/22 – 2025/26 ambapo kupitia Mpango huo Wizara imetekeleza afua za lishe zilizothibitishwa kuwa na matokeo makubwa ili kukabiliana na matatizo ya utapiamlo wa lishe duni na lishe ya kuzidi .
Alisema,baadhi ya afua hizo ni pamoja na; utoaji wa matone ya vitamin A, dawa za kutibu minyoo ya tumbo,
matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto, utoaji wa vidonge vya madini chuma na foliki asidi kwa wajawazito, uongezwaji wa virutubishi vya madini na vitamini kwenye vyakula vinavyoliwa kwa wingi
na wananchi ikiwemo unga wa ngano, unga wa mahindi, chumvi, mafuta ya kula, utoaji wa elimu ya lishe na uhamasishaji wa masuala ya ulaji unaofaa kwa kutumia vyakula vinavyopatikana kwenye maeneo yetu pamoja na kufanya mazoezi.
Alisema katika kuhakikisha jamii
inazingatia masuala ya unyonyeshaji maziwa ya mama, Wizara imeendelea kusimamia utekelezaji wa miongozo inayohimiza unyonyeshaji sahihi wa watoto ikiwemo mtoto kuanza kunyonyeshwa
ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa na
unyonyeshaji wa watoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo.
Ummy alisema Elimu ya unyonyeshaji imeendelea kutolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya, katika ngazi ya jamii na kupitia maadhimisho mbalimbali ikiwemo wiki ya unyonyeshaji ambapo kufuatia jitihada hizo, unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa watoto ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa umeongezeka kutoka asilimia 59 kwa mwaka 2015 hadi asilimia 70 kwa mwaka 2022.
Hali kadhalika alisema hali ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita imeimarika kutoka asilimia 58 ya mwaka 2015 hadi asilimia 64 mwaka 2022.
"Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, Wizara imeendelea kuimarisha afya na lishe ya watoto chini ya miaka 5 kwa kuendelea kutekeleza Kampeni ya Kitaifa ya utoaji wa matone ya Vitamini A kwa watoto walio chini ya miaka mitano. Malengo ya kampeni yalikuwa ni kutoa matone ya Vitamin A kwa watoto 9,460,369 wenye umri wa kati ya miezi 6 mpaka miezi 59 nchi nzima. Jumla ya watoto 9,456,436 walipatiwa matone ya vitamin A ambayo ni sawa na asilimia 99 ya lengo."alisema Ummy
Alisema kuwa Kiwango cha utekelezaji kimeongezeka ikilinganishwa na watoto 9,052,340 waliofikiwa kipindi kama hicho
mwaka 2022/23 huku akisema huduma ya utoaji wa matone ya Vitamini A kwa watoto chini umri wa miaka mitano hufanyika katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa utaratibu wa kawaida ambapo mtoto akitimiza umri wa miezi sita hupewa matone ya vitamini A na huendelea kupatiwa matone hayo kila baada ya miezi sita hadi atakapotimiza umri wa miaka mitano.