
Joyce Kasiki,DODOMA
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, amezindua rasmi Mkataba wa Huduma Bora kwa Wateja, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuongeza uwajibikaji miongoni mwa watoa huduma katika vituo vyote vya afya nchini.
Akizungumza leo, Juni 25, 2025 jijini Dodoma katika hafla fupi ya uzinduzi wa mkataba huo, Waziri Mhagama ameagiza utekelezaji wake ufanyike kwa haraka na kwa ufanisi katika ngazi zote — kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa, taasisi na vituo vya afya binafsi.
"Ndani ya muda mfupi sana, nataka kuona kila kituo cha afya nchini kikiwa kimekamilisha mkataba huu. Hii ni pamoja na Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya, Rufaa za Mikoa na Kanda, pamoja na Taasisi zote za afya,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, amesisitiza kuwa mkataba huo si tu utakaoainisha haki na wajibu wa watoa huduma na wagonjwa, bali pia utatoa mwongozo wa gharama na viwango vinavyopaswa kuzingatiwa ili kuhakikisha huduma bora, za haki, na zenye uwiano sawa.
Waziri Mhagama amesema mkataba huo pia utawezesha utoaji wa taarifa muhimu kwa wagonjwa kabla ya matibabu, jambo linalojenga imani na kuondoa sintofahamu.
"Ni matarajio yangu kuwa kupitia mkataba huu, kila mmoja atatimiza wajibu wake. Hii itasaidia kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima na kuifikisha sekta ya afya pale ambapo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka ifike,” ameongeza.
Katika hotuba yake, Waziri huyo pia amepongeza juhudi za Rais Samia katika kuimarisha sekta ya afya kwa kuwekeza katika mafunzo ya wataalamu wa afya, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa kama MRI, PET-Scan na mashine za X-Ray — vifaa ambavyo amesema ni adimu hata kwa baadhi ya mataifa mengine.
Aidha, amesema mkataba huo unaendana na dira ya Wizara ya Afya ya kujenga jamii yenye ustawi bora inayochangia kikamilifu maendeleo ya taifa, sambamba na dhima ya utoaji wa huduma bora za afya kwa wote.
"Kazi kubwa tuliyobakiwa nayo sasa ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora bila kikwazo cha fedha. Tumeshatekeleza bima ya afya kwa wote, sasa tunalenga kuhakikisha fedha za kuendeleza huduma zinapatikana ili tuendelee kuwekeza zaidi,” amesema.
Pamoja na hayo, mkataba huo umeainisha huduma zitakazotolewa ikiwa ni pamoja na ushauri wa kitaalamu wa masuala ya afya, huduma za chanjo, utoaji wa vyeti vya usajili wa kitaaluma, leseni na vibali, pamoja na taarifa mbalimbali za sekta ya afya.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Seif Shekalage, amesema mkataba huo utaimarisha zaidi utendaji kazi na kuongeza uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment