




Na Joyce Kasiki.Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaongiza viongozi mbalimbali wa Kitaifa kutoa salamu za rambirambi na kumkumbuka aliyekuwa Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, katika ibada ya kuuaga mwili wake jijini Dodoma.
Aidha ,viongozi hao wamemtaja Ndugai kama kiongozi mwenye maono, mbunifu na mpenda maridhiano.
Akizungumza katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, mara baada ya ibada maalumu ya kuuaga mwili wa marehemu, Rais Samia
ameahidi kwamba Serikali itaendelea kuenzi na kudumisha mchango mkubwa wa kimaendeleo uliotolewa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Job Yustino Ndugai
Hayati Ndugai alikuwa miongoni mwa viongozi wachapakazi waliotoa mchango mkubwa katika kuimarisha elimu, hususan kwa vijana wa Jimbo la Kongwa ambako alilitumikia kwa kipindi kirefu kama Mbunge.
“Kupitia utumishi wake, tumeshuhudia jitihada kubwa katika kuhakikisha vijana wanapata elimu bora na fursa za maendeleo. Kifo chake ni pigo kubwa si tu kwa familia na wananchi wa Kongwa, bali kwa taifa zima. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuifariji familia yake na kuwaongoza katika kipindi hiki kigumu,” alisema Rais Samia.
Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, alisema chombo hicho kinatoa shukrani kwa wote walioungana nacho katika kipindi hiki cha majonzi, kufuatia kuondokewa na kiongozi na ndugu waliyempenda.
“Kifo hiki kimeshtua wengi, hasa tukizingatia tupo katika mchakato wa uchaguzi, lakini Mungu ndiye mpangaji wa kila jambo, hivyo tunashukuru kwa yote,” alisema.
Dkt. Tulia alimwelezea marehemu Ndugai kama kiongozi aliyekuwa akitekeleza maneno yake kwa vitendo, bila kubagua chama, na aliyeleta mageuzi makubwa ndani ya Bunge.
Alitaja ubunifu wa kuendesha vikao kwa njia ya mtandao wakati wa janga la korona kama mfano wa fikra zake za kimapinduzi.
Aliongeza kuwa katika kipindi chake cha uongozi, Ndugai alisimamia utekelezaji wa sheria ya kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma, akihakikisha Bunge linaendelea kulinda heshima yake.
“Alikuwa mpambanaji dhidi ya utovu wa nidhamu na mleta maridhiano, huku wabunge wapya wakimwona kama mwalimu kwa namna alivyowaongoza,” alisema.
Dkt. Tulia aliwaombea faraja familia ya marehemu, akisema maisha yake yatabaki kuwa dira na somo kwa wote.
Aidha, alionya kuhusu baadhi ya watu wachache wanaotoa kauli za kuumiza familia, akisisitiza kuwa wema alioutenda unazidi kwa wingi maneno machache ya kuumiza.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatoa pole kwa Bunge na Watanzania wote walioguswa na msiba huo, akisema kazi ya Mungu haina makosa.
“Tunashukuru kwa ushirikiano tulioupata kutoka kwake katika kipindi cha uhai wake, na tunamuombea apumzike mahali pema peponi,” alisema.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, naye alieleza masikitiko makubwa kwa kuondokewa na kiongozi aliyeitumikia nchi kwa bidii na uadilifu.
“Msiba huu umetokea ghafla na umetuumiza, lakini hakuna budi kuupokea,” alisema.
Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, alisema Ndugai alikuwa rafiki na mshauri wa karibu, akimkumbuka tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Fedha.
“Msiba huu ni mkubwa na ni msiba wa kila mmoja wetu. Tumempoteza mtu wa thamani sana,” alisema.
Mwili wa marehemu Ndugai uliagwa leo kabla ya kusafirishwa kwenda wilayani Kongwa kwa maziko, huku mamia ya wananchi, wabunge na viongozi wa Serikali wakihudhuria shughuli hiyo ya kumuaga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule, alieleza kuwa Hayati Ndugai ameacha alama tatu muhimu katika mkoa wa Dodoma, ambazo ni: kuimarisha nidhamu na uwajibikaji katika vikao vya kimaendeleo, kufanya mapinduzi ya elimu hasa wilayani Kondoa, na kuhimiza kilimo cha zao la korosho katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa.
Awali, Katibu wa Bunge, Bw. Baraka Leonard, akisoma wasifu wa marehemu, alieleza kuwa Hayati Ndugai alifariki dunia mnamo tarehe 6 Agosti 2025, majira ya saa 9 alasiri jijini Dodoma, kutokana na shinikizo la damu kushuka kwa kiwango kikubwa (septic shock) kilichotokana na maambukizi makali ya mfumo wa hewa (severe pneumonia).
Katika maisha yake ya utumishi kwa umma, Ndugai alishikilia nyadhifa mbalimbali zenye mchango mkubwa kwa taifa, zikiwemo:
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanzania Wildlife Protection Fund (2001–2004),
Mjumbe wa Bodi ya Hifadhi ya Ngorongoro (2007–2010),
Mjumbe wa Baraza la Seneti la Chuo Kikuu cha Dodoma (2007–2010),
Mjumbe wa Bodi ya Uwekezaji ya Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola – Kanda ya Afrika (2015–2022).
Mbali na nafasi za kitaasisi, Hayati Ndugai pia alikuwa muumini wa Kanisa la Anglikana Tanzania na alihudumu kama Mzee wa Kanisa, na hadi umauti unamkuta alikuwa Lay Canon wa Dayosisi ya Mpwapwa – nafasi ya heshima inayomhusisha na ushauri wa kiroho kwa Askofu.
Hayati Job Yustino Ndugai alizaliwa tarehe 21 Januari 1963 katika Kijiji cha Laikala, Kata ya Sagara, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 65, na ameacha mke, watoto na wajukuu.







No comments:
Post a Comment