Ongezeko la ugonjwa wa selimundu huchangiwa na uelewa mdogo wa jamii kuhusiana na ugonjwa huo

Pichani ni seli nyekundu nzima (za duara) na seli nyekundu zenye shida (zilizojikunja) ambazo husababisha selimundu kutokana na kujikunja kwake (PICHA YA MTANDAO)

                 NA JOYCE KASIKI,DODOMA

UELEWA mdogo kwa jamii kuhusu ugonjwa wa Selimundu ni moja ya changamoto inayochangia ugonjwa huo kuendelea kuongezeka siku hadi siku hususan kwa watoto wadogo hali inayosababisha kuathiri ukuaji wao na hivyo kushindwa kufikia utimilifu wao.
Daktari  Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma  Halima Kassim amesema,watoto wanaohudhuria kliniki za Selimundu (Cycle cell) kwa mkoa wa Dodoma wameongezeka kutoka 338 mwaka jana hadi kufikia 559 mwaka huu huku akisema elimu bado inatakiwa kutolewa kwa jamii ili kuufahamu ugonjwa huo na kuchukua hatua za kukabiliana nao ikiwa ni pamoja na wapenzi wanaotarajia kuingia kwenye ndoa na kupata watoto kupima hali ya vinasaba vyao.
Akizungumzia kuhusu dalili za ugonjwa huo amesema zinaanza kuonyesha mtoto akiwa na umri wa kuanzia miezi sita tangu kuzaliwa huku akizitaja dalili hizo kuwa  ni pamoja na mtoto kulia mara kwa mara , weupe kwenye viganja vya mikono pamoja na kuvimba  mikono na miguu .
“Kwa hiyo tunashauri mzazi au mlezi  akiona dalili hizo amuwahishe mtoto hospitali haraka kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa kuangalia kama amerithi ugonjwa wa selimundu (Cyclecell) kutoka kwa wazazi wake.”amesema Dkt.Halima na kuongeza kuwa 
“Hatua hiyo itasaidia mtoto kuanza kupatiwa tiba mapema na hivyo kupunguza changamoto za ugonjwa huo ambazo ni  kupungukiwa damu ,maumivu ya mifupa lakini pia kupunguza kupata uambukizo wa bakteria,kuumwa kifua,kubanwa kifua ,kupooza ,kupunguza shida ya nyonga na kulazwa mara kwa mara.”
Pichani ni seli nyekundu nzima (za duara) na seli nyekundu zenye shida (zilizojikunja) ambazo husababisha selimundu kutokana na kujikunja kwake .(PICHA YA MTANDAO)


Dkt.Halima amesema,ugonjwa wa Selimundu kwa kiasi kikubwa unaathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto na makuzi yake kwa ujumla huku ikielezwa kuwa kukosekana kwa fursa za ukuaji kwa watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi minane kunaweza kusababisha changamoto katika maendeleo yao ambayo yanaweza kuathiri kizazi na kizazi lakini pia Taifa kukosa nguvukazi yenye tija.

“Ugonjwa huu una athari nyingi kwa mtoto kwa sababu muda mwingi mtoto anakuwa ni mwenye kuugua, kuongezewa damu,hapati afya lakini hakui kulingana na umri wake,unaweza kumwona mtoto wa miaka 11 lakini ukadhani ana miaka saba kwa sababu ya kuumwa mara kwa mara,

“Ugonjwa huu pia  humwathiri mtoto kisaikolojia kwa sababu ya kuumwa lakini pia unamwathiri mtoto kwa kushindwa kuhudhuria masomo yake mfululizo kwani kila wakati anakuwa wodini hivyo uchumi mwingi kutumika kwa ajili ya kumuuguza,lakini pia hawezi kuwa mtu ambaye ataweza kuzalisha au kuongeza kipato kwa maana ya uchumi wa Taifa .”amesema Dkt.Halima

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa jamii hasa kwa wachumba wanaotarajia kufunga ndoa na kupata watoto kuvunja ukimya kwa kupima ili kujua hali zao za vinasaba vya selimundu ili kuepuka kuzaa watoto wenye ugonjwa huo.

“Kwa kufanya hivi tutavunja mduara na tutapunguza hali ya maambukizi ya selimundu na kupelekea kupata kizazi kisichokuwa na selimundu na hivyo Taifa kuwa na nguvukazi yenye tija.”amesisitiza

Vile vile ametoa rai kwa jamii kuwapima watoto wao mapema ,kusikiliza vyombo vya habari kupata elimu ya ugonjwa huo ili  waweze kujua umuhimu wa wao kujua hali zao lakini pia kuweza kujua hali za watoto wao ili kuwakinga baadaye wasije wakapata wenza wenye vinasaba na wakatengeneza watoto wenye selimundu.

Aidha amesema,upo umuhimu wa elimu ya ugonjwa huo kutolewa kliniki za akina mama wajawazito na watoto ili wajenge uelewa kuhusu ugonjwa huo,licha ya kuwa tayari wameshaingia kwenye ndoa na kupata watoto, lakini itasaidia kujua hali ya mtoto mapema na kuweza kumsaidia kama amesharithi vinasaba vya ugonjwa huo na kupata matibabu mapema.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya selimundu ambayo huadhimishwa Juni 19 ya kila mwaka,Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa, zaidi ya watoto 300,000 duniani huzaliwa na Sikoseli kila mwaka.
Aidha amesema, nchini Tanzania takwimu zinaonyesha kuwa, takribani watoto 11,000 huzaliwa na ugonjwa wa sikoseli kila mwaka ambayo ni sawa na watoto 11 kati ya watoto 1000 wanaozaliwa. 

Kwa mujibu wa Ummy takwimu zinaonyesha kuwa, takribani watoto 7 kati ya watoto 100 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki hapa nchini kutokana na madhara yanayohusiana na ugonjwa wa sikoseli.
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza hivi karibuni katika maadhimisho ya Siku ya Selimundu Duniani

Amesema,katika kuboresha zaidi huduma kwa wagonjwa wa Sikoseli, serikali inaendelea kufanya tafiti za sikoseli nchini ambazo zitasaidia kupata takwimu na kufanya maamuzi ya Kisera yenye uthibitisho wa kisayansi unaoendana na mahitaji ya nchi  ili kuwa na kizazi kisichokuwa na ugonjwa wa sikoseli.

Kwa upande wake Mkurugenzi idara ya Tiba wa wizara ya Afya Prof Paschal Ruggajo amesema Serikali inaendelea kutoa elimu ya kupunguza uwezekano wa kupata watoto waliorithi vinasaba vya sikoseli kwa kuhamasisha ushauri na upimaji wa vinasaba vya sikoseli kwa vijana kabla ya kuingia kwenye mahusiano.

Aidha takwimu zinaonyesha kuwa, asilimia 15-20 ya watanzania 100 wana vinasaba vya ugonjwa huu, yaani wana uwezekano wa kupata watoto wenye ugonjwa wa Sikoseli iwapo watakuwa na wenza wenye vinasaba vya Sikoseli. 

Juni 19 ya kila mwaka ,Tanzania huungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku ya Selimundu yaani ‘Sicklecell ‘huku ikielezwa kuwa ugonjwa huo husababishwa na kurithi vinasaba vya ugonjwa huo kutoka kwa wazazi wote wawili.

Simon na Doreen Aloyce ni wachumba wanaotarajia kufunga ndoa wakizungumza na mwandishi wa habari hii wamesema,ni jambo zuri kwenda kupima kuangalia hali za vinasaba vyao vya selimundu ili waweze kuchukua hatua zaidi za kitaalam kwa lolote litakalotokea mbele yao.
Hata hivyo wameiomba Serikali  iendelee kutoa elimu kwa jamii kwani bado  haina elimu ya ugonjwa huo huku akisema wengi waliozaa watoto wenye selimundu huenda ni kutokana na kutokuwa na elimu hiyo.
Share:

Walimu darasa la awali wajengewa uwezo

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania

 

                       NA JOYCE KASIKI,DODOMA

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt.Aneth Komba amewataka walimu na wadhibiti Ubora wa shule kuhakikisha vitabu vyote vikiwemo vya darasa la elimu ya awali vinavyotumika shuleni ni vile vilivyopata ithibati tu na siyo vinginevyo.

Dkt.Komba ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa walimu wa darasa la awali yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Children in Crossfire (CiC) kupitia Mradi wake wa Watoto Wetu Tunu Yetu uanaotekelezwa katika mikoa ya Dodoma,Morogoro na Mwanza kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Kwa mujibu wa kiongozi huyo matumizi ya vitabu vilivyopata Ithibati yatasaidia watoto kujifunza yale yaliyoandaliwa kwa ajili yao hasa watoto wadogo ambao ndiyo wanaanza kujifunza vitu ikiwemo maadili ya kitanzania.

“Serikali  inasisitiza matumizi sahihi ya vitabu vya ziada na kiada ambavyo vina ithibati,kuna utaratibu wa vitabu kupewa ithibati na Kamishna wa Elimu,kwa hiyo wanafunzi watumie vitabu ambavyo vimeidhinishwa na serikali ,na ili tuhakikishe kwamba tunapenda utamaduni wa kujisomea ni muhimu mtoto atumie vitabu vyote vya kiada na ziada.”amesema Dkt.Komba

Katika hatua nyingine amewaelekeza Wadhibiti Ubora wa shule wakasimamie vyema utekelezaji wa mafunzo hayo ili kuhakikisha  kwamba baada ya mafunzo hayo walimu wanakwenda kutumia mafunzo hayo kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi wa darasa la awali.

“Mnapaswa mkakague na  kuhakikisha kweli mwalimu anaandaa darasa changamshi ,anaandaa zana za kutosha za kufundishia na watoto wanaweza kupata ule umahiri uliokusudiwa hasa mahiri za Kusoma,Kuandika na Kuhesabu.”amesema na kuongeza kuwa

Kwa upande wake mwakilishi wa Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Watoto Wetu Tunu Yetu unaolenga kuimarisha elimu ya darasa la awali Lustica Turuka amesema,ni matumaini ya mkoa wa Dodoma kwamba mafunzo hayo yanakwenda kuwapatia walimu  mbinu mpya za ufundishaji wa darasa la elimu ya awali.

“Lakini pia tunategemea ,walimu hawa watakuwa walimu wa mfano kwa ajili ya shule nyingine ambazo walimu wake hawajapata mafunzo haya kwa sababu tumetoa mwalimu mmoja kwenye kila kata ,hii inamaanisha kwamba yule mwalimu aliyepata mafunzo haya ,anakwenda kuwaambukiza wenzake ambao hawajapata mafunzo haya.”amesema na kuongeza kuwa

“Hatutaki tena ule utaratibu wa kufundishia watoto wa darasa la awali chini ya miti ,tunataka kuona wanafunzi wa daras la elimu ya awali wanasoma kwenye madarasa mazuri na ambayo ni changamshi na yanayoongea  ambayo humwezesha mtoto kujifunza kwa kuona na kucheza lakini pia kupenda shule na mwisho wa siku tunategemea mafanikio makubwa sana hasa kwenye suala la kusoma,kuandika na kuhesabu kwa sababu darasa la elimu ya awali ndiyo msingi wa madarasa mengine yote.”

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa CiC Heri Ayubu amesema kuwa mradi huo wa "Watoto Wetu Tunu Yetu" unatekelezwa katika mikoa mitatu ya Mwanza, Morogoro na Dodoma ukiwa na lengo la kuendelea kuchangia uboreshaji wa utoaji wa elimu ya Awali nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Serikali.

Amesema kuwa,mwisho wa mradi huo wanatarajia kuona ongezeko kubwa la wanafunzi wenye utayari wa kuingia darasa la Kwanza kwa kuweza kumudu KKK kwa maana ya Kusoma,Kuandika na Kuhesabu. 

Mwalimu Kinara wa darasa la awali kutoka wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ambaye alishapata mafunzo hayo kupitia Mradi huo wa Watoto Wetu Yetu ulioanza kutekelezwa wilayani humo mwaka 2019 Regina Masawe amesema,mafunzo hayo yamemwezesha kupata nyanja nyingi za ufundishaji wa watoto wa darasa la awali na ufundishaji wake ulikuwa ni tofauti na wakati hajapata mafunzo.

Naye mwalimu wa shule ya Msingi Igoji Kaskazini Wilayani Mpwapwa Frank Masamale amesema,amefurahishwa na CiC kutambua umuhimu wa elimu ya awali na kuandaa mafunzo hayo kwa walimu ambao sasa watakwenda kufundisha watoto kwa namna rahisi itakayowawezesha kuelewa bila kutumia nguvu .

Ameomba mafunzo hayo yawe endelevu ili walimu wote wanaofundisha elimu ya awali waweze kufikiwa ili kufikia lengo lililokusudiwa la kutoa elimu bora kwa watoto wadogo ambao wanaandaliwa kulitumikia Taifa hapo baadaye.Afisa Elimu Kata,Kata ya Lumuma Wilayani Mpwapwa Batlet Mfugale amesema ,watoto elimu ya awali wanahitaji kufundishwa  kwa ukaribu zaidi ili waweze kujifunza na kujua kusoma kuandika na kuhesabu ili wawe wazuri zaidi wanapofika madarasa ya juu.

“Watoto wengi unakuta hawajui kusoma kuandika na kuhesabu wanapofika madarasa ya juu kwa sababu hawakuzingatiwa katika ufundishwaji kulingana na umri wao ,lakini kupitia mradi wa Watoto wetu tunu yetu kama ukizingatiwa,kusimamiwa na watoto wakapata stahili zinazotakiwa wataweza kumudu stadi zote tatu watakapokuwa madarasa ya juu kwa sababu elimu awali ndiyo msingi wa watoto wetu.”

Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya miaka mitano 2021/22-2025/26 inayolenga kuhakikisha mtoto anakua kwa utimilifu wake na hivyo Taifa kuwa na nguvu kazi yenye tija hapo baadaye.



Share:

Shekimweri : Wadau wa michezo tangazeni vivutio vya Utalii Dodoma

 


                               NA JASMINE SHAMWEPU,DODOMA

WADAU wa michezo nchini wametakiwa kutumia michezo kutangaza vituo vya Utalii vilivyopo Jijini hapa ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutangaza Utalii wa ndani. 

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri amesema hayo jijini hapa wakati  akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kutambulisha rasmi maandalizi ya Mbio za Mtembezi zitakazofanyika Julai 1,2023 Jijini Dodoma 

Mbio hizo zimeandaliwa na Mtembezi Adventure kwa kushirikiana na Ofisi yake kwa lengo la kuhamasisha Utalii wa Ndani.

Mkuu huyo amesema hatua hiyo itasaidia kuvitangaza vivutio vingi vya kihistoria vilivyopo mkoani hapa huku vingi vikiwa vimebeba historia ya Mkoa wa Dodoma.

"Mfano asili ya neno Dodoma ambalo Tembo alididimia na kuzama moja kwa moja na kupelekea wenyeji na wakazi wa eneo hilo lililopo Kata ya Kikuyu  kukiita kitendo hicho Idodomya yaani imedidimia na kupelekea Mkoa huo kuitwa Dodoma hadi leo," amesema.

"Dodoma tuna michoro ya mpango,mapori ya swagaswaga na wanyama wapo,tunataka kupitia mbio hizi za Mtembezi watu wajue Dodoma ni sehemu ya Utalii Kwa kuwa tuna vivutio vya kutosha, watanzania wanatakiwa kuipenda asili yao na kuijua kwa kina hivyo ni wajibu wetu kupitia michezo tuwe  vinara wa kutunza asili ya utanzania,"amesema.

Naye Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Jeshi la uhifadhi Ofisi ya TANAPA Dodoma Dkt.Noelia Myonga

ameielezea Tasisi ya mtembezi Adventures, kuwa ni mfano kwa kuwa kinara kuhamasisha Utalii kwa Ubunifu wa hali ya juu.

Amesema,ni muda mrefu sasa kumekuwa na harakati mbalimbali za kuhamasisha utalii lakini Kwa Mkoa wa Dodoma juhudi zaidi Bado zinahitajika na kusema kuwa kupitia mbio hizo itasaidia watanzania kutilia mkazo mambo yote yanayohusu utalii na uhifadhi. .

Alisema Mkoa wa Dodoma una vivutio vingi vya kihistoria na kutolea mfano," hapa Kikuyu mbali na kuwepo kwa eneo la tembo,ukiingia ndani ya chuo kikuu cha St.Jonh  kuna mti mkubwa uliotumika kunyongea wahalifu kipindi Cha utumwa lakini ukiwauliza wanaosoma pale hawajui chochote kuhusu mti huo,"amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Taasisi hiyo ya mtembezi Adventures,  ambayo ndiyo waandaaji wakuu wa mbio za  Mtembezi Samson Samwel amesema kwa  kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma  mbio hizo zitachochea Utalii Dodoma.

Amefafanua kuwa mbio hizo zitafanyika tarehe 1 july ambapo kwa kuanza zitasindikizwa na Maonyesho ya siku tatu yatakayolenga kuonyesha utalii wa ndani Dodoma na Tanzania kwa ujumla na kwamba mbali na Dodoma zimefanyika katika mikoa mitatu tofauti yaani Dar Es Salaam,Kigoma na Tabora.

"Tulianza rasmi mwaka 2021 na tulipata umaarufu na kukua zaidi baada kwa kushindwa na aliekua mkuu wa wilaya ya Temeke wakati huo DC jokate mwigelo,tunajivunia kuwa na mafanikio zaidi,"anafafanua.

Mbali na hayo ameeleza kuwa  Mtembezi Marathon ni mbio ambazo huandaliwa kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani nchini na kufanyika katika kanda na mikoa mbalimbali na kutangaza  fursa za utalii zilizopo katika eneo husika.

Share:

Musukuma ataka waenezaji uvumi kuhusu nchi kuuzwa wachukuliwe hatua

MBUNGE WA GEITA VIJIJINI MUSUKUMA KASHEKU AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI NYUMBANI KWAKE JIJINI DODOMA

 

 

           NA JOYCE KASIKI,DODOMA

MBUNGE wa Geita Vijijini Joseph Musukuma amesema,Serikali inapaswa kuwachukulia hatua watu wote  wenye tabia ya kueneza uongo kwenye mitandao ya kijamii pindi serikali inapotaka kufanya jambo lenye maslahi kwa nchi na hivyo kuleta taharuki.

Musukuma ameyasema hayo kufuatia uvumi ulioenea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwekezaji unaotaka kufanywa na mwekezaji Ruler of Dubai katika Bandari ya Dar es Salaam huku  akisema uwekezaji huo utakuwa na maslahi mapana kwa nchi na siyo nchi kuuzwa kama inavyodaiwa kwenye mitandao hiyo.

“Hapa nchini kumekuwa na tabia ya watu kueneza uvumi na uongo kila serikali inapotaka kutekeleza miradi yenye maslahi mapana kwa nchi,nakumbuka hata wakati serikali ya awamu ya tano ilipotaka kutekeleza miradi ya kimkakati watu walipiga makelele lakini sasa hivi ndiyp hiyo tunayoitumia kupigia kampeni,tumwache Rais afanye kazi na atimize ndoto zake.”amesema Musukuma

Amesema,wao kama Wabunge wanachojadili sasa ni makubaliano ya nchi kwa nchi siyo kweli kwamba wanakwenda kupitisha azimio la kumpa mwekezaji huyo Bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka 100.

“Sisi wabunge siyo wajinga tupitishe kitu ambacho tunajua kinakwenda kuiumiza nchi,lakini hata Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) naye atatumikia nchi lakini baadaye ataastaafu,sasa akishastaafu yeye atakwenda kuishi wapi mpaka aiingize nchi matatani”

Aidha Musukuma amesema,uwekezaji unaoenda kufanywa kwenye Bandari hiyo bado haujajulikana ni wa muda gani lakini utakuwa na maslahi mapana hasa kwenye mapato ambapo nchi inakwenda kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 38 kutoka shilingi bilioni 7 inayoingizwa sasa lakini pia unakwenda kuongeza ajira kutoka 71,000 hadi ajira 128,000 .

Amesema,bandari yetu kwa sasa inapokea makontena laki saba hadi laki nane lakini baada ya mwekezaji kuja tutakuwa tunapokea zaidi ya makontena milioni moja huku akisema hii ni fursa kama nchi inapaswa kuitumia.

“Bandari ni lango kuu la uchumi,tena mimi nilitamani tukimaliza kufanya uwekezaji kwenye bandari,twende na Airport maana napo pana mifumo mibovu.”amesisitiza

Hata hivyo amesema,uwekezaji huo unakwenda kuongeza mapato huku akisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) haitaingiliwa kwenye ukusanyaji wake wa mapato katika eneo hilo la Bandari.

Musukuma ametumia nafasi kuiomba Serikali ipeleke waandishi nchini Dubai angalau 100 kutoka mikoa yote ili waende kujifunza nchini humo na waweze kuelimisha vyema wananchi.

Aidha Musukuma amekanusha tuhuma zinazowahusisha wabunge walioenda nchini Dubai kwa ziara ya mafunzo kwamba wamehongwa huku yeye binafsi akihusishwa kuhongwa gari huku akisema tuhuma hizo hazina ukweli wowote na kwamba gari linalosemwa alilinua kwa pesa yake na alilipa ushuru bandarini kiasi cha shilingi milioni 130.


Share:

Watalii wa uwindaji wa kitalii waongezeka nchini, rekodi yavunjwa,..haijawahi kutoke

 

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MOHAMED MCHENGERWA


        NA BEATUS MAGANJA 

Waziri wa Maliasili na Utalii  Mohamed Mchengerwa amesema Tanzania kupitia  Sekta ya Utalii imeshuhudia kuvunjwa Kwa rekodi ya idadi ya watalii waliotembelea Nchi Yetu Kwa shughuli mbalimbali za Kitalii wakiwemo watalii wa uwindaji wa kitalii ikiwa ni idadi kubwa kuwahi kuipokea kuliko Wakati wowote katika historia ya kuanzishwa Kwa sekta hiyo.

Ameyasema hayo leo June 2, 2023 akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Kwa Mwaka wa fedha 2023/2024 Jijini Dodoma ambapo ongezeko hilo ni kwa mujibu wa taarifa za miezi 10 tu yaani kuanzia Julai mwaka jana hadi Aprili mwaka huu.

"Mheshimiwa Spika, pamoja na kuongezeka Kwa ujumla Kwa idadi ya watalii Kitaifa, katika kipindi hiki cha utekelezaji, taasisi kubwa za Utalii Nchini zimeshuhudia kuvunjwa Kwa rekodi ya idadi ya watalii katika maeneo yao..." amesema

"..Kwa Upande wa TAWA watalii wa Uwindaji wameongezeka kutoka 541 Kwa Mwaka 2021/22 hadi kufikia watalii wa uwindaji 692 Kwa kipindi Cha miezi 10 tu ya mwaka wa fedha 2022/23" amesema

Katika jitihada za kuendeleza uhifadhi wa rasilimali muhimu Mhe. Mchengerwa amesema Wizara imefanikiwa kupandisha hadhi Mapori Tengefu mawili (2) yaani Kilombero na Pololeti kuwa Mapori ya Akiba

Aidha amesema hatua hiyo imeongeza idadi ya Mapori ya Akiba Nchini kutoka 27 hadi 29 lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Katika kuendeleza jitihada za Kukabiliana na changamoto za migogoro baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu Waziri Mchengerwa ameiagiza TAWA na Wataalamu wengine wa wanyamapori  kuendelea kutoa elimu Kwa wananchi  kuhusu namna ya kujikinga na wanyamapori hao na kuwafundisha askari wa vijiji mbinu zaidi za medani.

 

Hata hivyo Waziri Mchengerwa amebainisha mikakati 10 ya Wizara yake anayoendelea nayo katika kudhibiti changamoto ya Wanyamapori Wakali na Waharibifu.

Amesema kukamilisha Maelekezo ya Baraza la Mawaziri juu ya Mipaka kati ya vijiji 975 vilivyokuwa na Migogoro na Hifadhi, kuendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa utatuzi wa Migogoro baina ya binadamu na Wanyamapori Wakali na Waharibifu (2020 -2024) na kutoa elimu kuhusu namna ya Kukabiliana na wanyama hao ni sehemu ya mikakati yake.

Mikakati mingine ni pamoja na kutoa vifaa Kwa wananchi vya kupambana au kuwafukuza Wanyamapori Wakali na Waharibifu, kutoa kifuta jasho na machozi Kwa wanaoathirika na Wanyamapori Wakali na Waharibifu pamoja na kufanya utafiti Kwa kuwafunga mikanda ya mawasiliano viongozi wa makundi ya Wanyamapori hao Ili kubaini mienendo yao.

Mingine ni kutumia ndege Maalum kuondoa Wanyamapori kwenye makazi, kuongeza vitendea kazi vya kupambana na Wanyamapori Wakali na Waharibifu, kuongeza Askari wa Doria na kutumia Askari Wanyamapori wa vijiji pamoja na kuunda Kamati Maalum ya Wataalamu kumshauri Waziri

Share:

Juhudi za serikali dhidi ya utoaji mimba usio salama zatajwa

 

NAIBU WAZIRI WA AFYA DKT.GODWIN MOLLEL

      NA WAF, BUNGENI DODOMA. 

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amebainisha juhudi zinazofanywa na Wizara ya Afya katika mapambano dhidi ya changamoto ya utoaji mimba usio salama ikiwemo kuwa ni pamoja na  kutoa elimu juu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike ambao wapo chini ya umri wa kuzaa.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Juni 2, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Judith  Kapinga katika Bunge la kumi na mbili Mkutano wa kumi na moja kikao cha 39, Jijini Dodoma. 

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, Wizara kupitia vitengo vyake imeendelea kutoa elimu kwa klabu za vijana na vijana balehe kutojihusisha na ngono zembe (abstinence) ili kuepuka kupata mimba zisizotarajiwa ambazo hupelekea kuongezeka vitendo vya utoaji mimba usio salama.

Aidha, Dkt. Mollel amesema, Wizara inaendelea kusimamia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma bila malipo ili kuwawezesha wanawake na wanaume kuzuia mimba zisizotarajiwa. 

Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, ametoa wito kwa jamii kuhakikisha mimba zote zinapatikana kwa mpango ili kuondokana na changamoto ya utoaji mimba usio salama unaoweza kuathiri afya za wajawazito. 

Pia, amewataka wajawazito kuhudhuria katika kliniki za uzazi wa mpango ili waweze kupatiwa elimu ya afya ya uzazi ikiwemo jinsi ya kuepukana na mimba zisizotarajiwa ili kuondokana na uavyaji wa mimba usio salama.


Share:

Serikali,wadau waombwa kuwezesha upatikanaji wa hedhi salama


 

NA JUDITH FERDINAND,MWANZA

Serikali na wadau mbalimbali nchini wameombwa kuhakikisha taulo za kike zinapatikana kwa urahisi, miundombinu ya kujihifadhia inakuwepo pamoja na maji safi na salama ili kuwafanya watoto wa kike kuwa na hedhi salama hususan wawapo shuleni.

Akizungumza na mtandao huu ,mmoja wa wanafunzi jijini Mwanza Irene Shelesta, ameeleza kuwa suala la hedhi salama kwa mabinti limekuwa changamoto kutokana na ukosefu wa miundombinu rafiki kwa ajili ya kujihifadhia na kuhifadhia taulo zilizotumika shuleni hata nyumbani.

Irene ameeleza kuwa changamoto nyingine shule nyingi na maeneo  mengi ya vijijini na  pembezoni mwa miji  kukosa maji salama ambayo ni muhimu wakati wa binti kuchisafisha na kufanya kuwa na hedhi salama bila maambukizi yoyote.

Huku akisisitiza kuwa suala la hupatikanaji wa taulo za kike zimekuwa changamoto kwa mabinti wawapo shuleni hata nyumbani kwani siyo wote wanaweza kumudu gharama.

"Unakuta shule kuna miundombinu ya kutupia taulo za kike zilizotumika lakini hakuna maji safi kwa ajili ya kujisafishia wala chumba cha kujihifadhia chenye usiri hivyo inakuwa changamoto sana kwetu,mfano wanaosoma shule za bweni ukikuta anatumia taulo za kike za kufua alafu maji hamna inakuwa ni changamoto hivyo wadau na serikali itusaidia kuweka mazingira rafiki ya kuwa na hedhi salama,"ameeleza Irene.

Kwa upande wake Ofisa  Maendeleo ya Mtoto,Mtandao wa Vijana na Watoto Mwanza (MYCN)Nuru Massanja, ameeleza kuwa suala la hedhi salama siyo la watoto wa kike na wanawake tu ni la kila mmoja serikali na jamii nzima katika kuhakikisha mtoto wa kike anakuwa salama pale anapokuwa katika hedhi.

“Hivyo serikali ihakikishe watoto wa kike wanapata maji salama wawapo shule kwa ajili ya kujisafishia pia hata nyumbani kuwe na  upatikanaji rahisi wa maji  kwa serikali kusogeza huduma karibu maana kuna kutumia taulo za kike za kufua ambazo zinahitaji maji ya kutosha kwa ajili ya kuzifua kwa matumizi ya baadaye.”amesema Ofisa huyo

Ameongeza kuwa “Pia kuhakikisha kuna kuwa na vyoo au vyumba vya kujihifadhia wakati wa hedhi wawapo shuleni vyenye usiri ambavyo mtoto wa kike atakuwa uhuru kubadilisha taulo za kike bila mtu yoyote kufahamu kama yupo hedhini.”

"Serikali iangalie miundombinu ya kutupa taka yani taulo za kike zilizotumika ili  baada ya kujisafishia anatupa uchafu kwenye mazingira mazuri kuliko kuweka kwenye begi na kusubiria mpaka atoke shule akatupe nyumbani,

“Mwingine hawezi kufanya hivyo anaona aibu na kuona bora abaki nyumbani mpaka siku zake za hedhi zotakapoisha ndio aende shule wakati huo anakuwa amepitwa na masomo," ameeleza Nuru

Akizungumzia suala la upatikanaji wa taulo za kike Nuru ameeleza kuwa serikali ina nguvu kubwa katika kuzingatia bei kwani siyo kila mzazi ana uwezo wa kununua taulo za kike kila mwezi kwa ajili ya binti yake hususani vijijini .

Ameiomba Serikali iweke bei elekezi kwa wafanyabiashara ambayo itaendana na uchumi wa Watanzania walio wengi pamoja na kuhakikisha maeneo ya shule kwa kushirikiana na wadau zinapatikana bure wakati wote.

"Serikali iweke utaratibu wa kuhakikisha watoto wa kike shuleni kwa kila shule wanapata taulo za kike ambazo watatumia wawapo shuleni wakati wa hedhi ili kutokatisha  masomo kwa siku wanazokuwa hedhini pia hata kama mzazi wake ana fedha ya kununua taulo za kike anajua akifika shule atazikuta hivyo kuendelea kusoma katika mazingira salama yanayoendana na hedhi salama,"ameeleza Nuru.

Sanjari na hayo Nuru ametumia fursa hiyo kuwahimiza  wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kuzungumza na watoto wao siyo wa kike tu bali wote kuhusu hedhi salama ili kuleta urahisi kwa mtoto wa kike kuwa katika mazingira rafiki.

"Kuwaelimisha watoto wote siyo wa kike pekee kwani huwezi jua atakayemsaidia binti anapokuwa katika hedhi kwenye mazingira ya shule au nyumbani kwani mtoto wa kiume akiwa anajua masuala kama hayo itasaidia kuwa na mazingira mazuri kwa mtoto wa kike wakati wa hedhi,

“Pia elimu ya hedhi salama itawasaidia watoto kutojiingiza katika masuala ya mapenzi kwani anatambua kuwa muda gani anaweza kupata mabadiliko kwenye mwili na namna gani ya kujizuia,"ameeleza Nuru.

Mmoja wa wananchi wa Kata ya Nyamanoro Lydia Hugo, ameeleza kuwa  kukua kwa teknolojia kila siku vitu vinabadilika hata vya kujihifadhia wakati wa hedhi tofauti na zamani ambapo sasa zipo hadi taulo za kufua ambazo zinahitaji maji safi kwa ajili ya kusafisha baada ya kutumia hivyo ni wakati wa serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.

"Binafsi taulo za kufua zimenipunguzia gharama ya kununua kila mwezi nanunua mara moja kwa mwaka na kutumia kwa muda wa zaidi ya miezi 12, lakini changamoto ni maji hasa yanapokuwa ya mgao unashindwa kufua vizuri hali ambayo ni hatari kwa afya,"ameeleza Lydia.


Share:

Theme Support

Need our help to upload or customize this blogger template? Contact me with details about the theme customization you need.

Labels

Recent Posts

Unordered List

  • Lorem ipsum dolor sit amet, consectetuer adipiscing elit.
  • Aliquam tincidunt mauris eu risus.
  • Vestibulum auctor dapibus neque.

Pages

Theme Support

Need our help to upload or customize this blogger template? Contact me with details about the theme customization you need.