Pichani ni seli nyekundu nzima (za duara) na seli nyekundu zenye shida (zilizojikunja) ambazo husababisha selimundu kutokana na kujikunja kwake (PICHA YA MTANDAO) |
NA JOYCE KASIKI,DODOMA
UELEWA mdogo kwa jamii kuhusu ugonjwa wa Selimundu ni moja ya changamoto inayochangia ugonjwa huo kuendelea kuongezeka siku hadi siku hususan kwa watoto wadogo hali inayosababisha kuathiri ukuaji wao na hivyo kushindwa kufikia utimilifu wao.
Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma Halima Kassim amesema,watoto wanaohudhuria kliniki za Selimundu (Cycle cell) kwa mkoa wa Dodoma wameongezeka kutoka 338 mwaka jana hadi kufikia 559 mwaka huu huku akisema elimu bado inatakiwa kutolewa kwa jamii ili kuufahamu ugonjwa huo na kuchukua hatua za kukabiliana nao ikiwa ni pamoja na wapenzi wanaotarajia kuingia kwenye ndoa na kupata watoto kupima hali ya vinasaba vyao.
Akizungumzia kuhusu dalili za ugonjwa huo amesema zinaanza kuonyesha mtoto akiwa na umri wa kuanzia miezi sita tangu kuzaliwa huku akizitaja dalili hizo kuwa ni pamoja na mtoto kulia mara kwa mara , weupe kwenye viganja vya mikono pamoja na kuvimba mikono na miguu .
“Kwa hiyo tunashauri mzazi au mlezi akiona dalili hizo amuwahishe mtoto hospitali haraka kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa kuangalia kama amerithi ugonjwa wa selimundu (Cyclecell) kutoka kwa wazazi wake.”amesema Dkt.Halima na kuongeza kuwa
“Hatua hiyo itasaidia mtoto kuanza kupatiwa tiba mapema na hivyo kupunguza changamoto za ugonjwa huo ambazo ni kupungukiwa damu ,maumivu ya mifupa lakini pia kupunguza kupata uambukizo wa bakteria,kuumwa kifua,kubanwa kifua ,kupooza ,kupunguza shida ya nyonga na kulazwa mara kwa mara.”
Pichani ni seli nyekundu nzima (za duara) na seli nyekundu zenye shida (zilizojikunja) ambazo husababisha selimundu kutokana na kujikunja kwake .(PICHA YA MTANDAO) |
Dkt.Halima amesema,ugonjwa wa Selimundu kwa kiasi kikubwa unaathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto na makuzi yake kwa ujumla huku ikielezwa kuwa kukosekana kwa fursa za ukuaji kwa watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi minane kunaweza kusababisha changamoto katika maendeleo yao ambayo yanaweza kuathiri kizazi na kizazi lakini pia Taifa kukosa nguvukazi yenye tija.
“Ugonjwa huu una athari nyingi kwa mtoto kwa sababu muda mwingi mtoto anakuwa ni mwenye kuugua, kuongezewa damu,hapati afya lakini hakui kulingana na umri wake,unaweza kumwona mtoto wa miaka 11 lakini ukadhani ana miaka saba kwa sababu ya kuumwa mara kwa mara,
“Ugonjwa huu pia humwathiri mtoto kisaikolojia kwa sababu ya kuumwa lakini pia unamwathiri mtoto kwa kushindwa kuhudhuria masomo yake mfululizo kwani kila wakati anakuwa wodini hivyo uchumi mwingi kutumika kwa ajili ya kumuuguza,lakini pia hawezi kuwa mtu ambaye ataweza kuzalisha au kuongeza kipato kwa maana ya uchumi wa Taifa .”amesema Dkt.Halima
Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa jamii hasa kwa wachumba wanaotarajia kufunga ndoa na kupata watoto kuvunja ukimya kwa kupima ili kujua hali zao za vinasaba vya selimundu ili kuepuka kuzaa watoto wenye ugonjwa huo.
“Kwa kufanya hivi tutavunja mduara na tutapunguza hali ya maambukizi ya selimundu na kupelekea kupata kizazi kisichokuwa na selimundu na hivyo Taifa kuwa na nguvukazi yenye tija.”amesisitiza
Vile vile ametoa rai kwa jamii kuwapima watoto wao mapema ,kusikiliza vyombo vya habari kupata elimu ya ugonjwa huo ili waweze kujua umuhimu wa wao kujua hali zao lakini pia kuweza kujua hali za watoto wao ili kuwakinga baadaye wasije wakapata wenza wenye vinasaba na wakatengeneza watoto wenye selimundu.
Aidha amesema,upo umuhimu wa elimu ya ugonjwa huo kutolewa kliniki za akina mama wajawazito na watoto ili wajenge uelewa kuhusu ugonjwa huo,licha ya kuwa tayari wameshaingia kwenye ndoa na kupata watoto, lakini itasaidia kujua hali ya mtoto mapema na kuweza kumsaidia kama amesharithi vinasaba vya ugonjwa huo na kupata matibabu mapema.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya selimundu ambayo huadhimishwa Juni 19 ya kila mwaka,Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa, zaidi ya watoto 300,000 duniani huzaliwa na Sikoseli kila mwaka.
Aidha amesema, nchini Tanzania takwimu zinaonyesha kuwa, takribani watoto 11,000 huzaliwa na ugonjwa wa sikoseli kila mwaka ambayo ni sawa na watoto 11 kati ya watoto 1000 wanaozaliwa.
Kwa mujibu wa Ummy takwimu zinaonyesha kuwa, takribani watoto 7 kati ya watoto 100 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki hapa nchini kutokana na madhara yanayohusiana na ugonjwa wa sikoseli.
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza hivi karibuni katika maadhimisho ya Siku ya Selimundu Duniani |
Amesema,katika kuboresha zaidi huduma kwa wagonjwa wa Sikoseli, serikali inaendelea kufanya tafiti za sikoseli nchini ambazo zitasaidia kupata takwimu na kufanya maamuzi ya Kisera yenye uthibitisho wa kisayansi unaoendana na mahitaji ya nchi ili kuwa na kizazi kisichokuwa na ugonjwa wa sikoseli.
Kwa upande wake Mkurugenzi idara ya Tiba wa wizara ya Afya Prof Paschal Ruggajo amesema Serikali inaendelea kutoa elimu ya kupunguza uwezekano wa kupata watoto waliorithi vinasaba vya sikoseli kwa kuhamasisha ushauri na upimaji wa vinasaba vya sikoseli kwa vijana kabla ya kuingia kwenye mahusiano.
Aidha takwimu zinaonyesha kuwa, asilimia 15-20 ya watanzania 100 wana vinasaba vya ugonjwa huu, yaani wana uwezekano wa kupata watoto wenye ugonjwa wa Sikoseli iwapo watakuwa na wenza wenye vinasaba vya Sikoseli.
Juni 19 ya kila mwaka ,Tanzania huungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku ya Selimundu yaani ‘Sicklecell ‘huku ikielezwa kuwa ugonjwa huo husababishwa na kurithi vinasaba vya ugonjwa huo kutoka kwa wazazi wote wawili.
Simon na Doreen Aloyce ni wachumba wanaotarajia kufunga ndoa wakizungumza na mwandishi wa habari hii wamesema,ni jambo zuri kwenda kupima kuangalia hali za vinasaba vyao vya selimundu ili waweze kuchukua hatua zaidi za kitaalam kwa lolote litakalotokea mbele yao.
Hata hivyo wameiomba Serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii kwani bado haina elimu ya ugonjwa huo huku akisema wengi waliozaa watoto wenye selimundu huenda ni kutokana na kutokuwa na elimu hiyo.
No comments:
Post a Comment