NAIBU WAZIRI WA AFYA DKT.GODWIN MOLLEL |
NA WAF, BUNGENI DODOMA.
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amebainisha juhudi
zinazofanywa na Wizara ya Afya katika mapambano dhidi ya changamoto ya utoaji
mimba usio salama ikiwemo kuwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike
ambao wapo chini ya umri wa kuzaa.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Juni 2, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Judith Kapinga katika Bunge la kumi na mbili Mkutano wa kumi na moja kikao cha 39, Jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, Wizara kupitia vitengo vyake imeendelea kutoa elimu kwa klabu za vijana na vijana balehe kutojihusisha na ngono zembe (abstinence) ili kuepuka kupata mimba zisizotarajiwa ambazo hupelekea kuongezeka vitendo vya utoaji mimba usio salama.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Wizara inaendelea kusimamia utoaji wa
huduma za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma bila malipo ili kuwawezesha
wanawake na wanaume kuzuia mimba zisizotarajiwa.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, ametoa wito kwa jamii
kuhakikisha mimba zote zinapatikana kwa mpango ili kuondokana na changamoto ya
utoaji mimba usio salama unaoweza kuathiri afya za wajawazito.
Pia, amewataka wajawazito kuhudhuria katika kliniki za uzazi wa
mpango ili waweze kupatiwa elimu ya afya ya uzazi ikiwemo jinsi ya kuepukana na
mimba zisizotarajiwa ili kuondokana na uavyaji wa mimba usio salama.
No comments:
Post a Comment