NA JUDITH FERDINAND,MWANZA
Serikali na wadau mbalimbali nchini wameombwa
kuhakikisha taulo za kike zinapatikana kwa urahisi, miundombinu ya kujihifadhia
inakuwepo pamoja na maji safi na salama ili kuwafanya watoto wa kike kuwa na
hedhi salama hususan wawapo shuleni.
Akizungumza na mtandao huu ,mmoja wa wanafunzi jijini
Mwanza Irene Shelesta, ameeleza kuwa suala la hedhi salama kwa mabinti limekuwa
changamoto kutokana na ukosefu wa miundombinu rafiki kwa ajili ya kujihifadhia
na kuhifadhia taulo zilizotumika shuleni hata nyumbani.
Irene ameeleza kuwa changamoto nyingine shule
nyingi na maeneo mengi ya vijijini
na pembezoni mwa miji kukosa maji salama ambayo ni muhimu wakati wa
binti kuchisafisha na kufanya kuwa na hedhi salama bila maambukizi yoyote.
Huku akisisitiza kuwa suala la hupatikanaji wa
taulo za kike zimekuwa changamoto kwa mabinti wawapo shuleni hata nyumbani
kwani siyo wote wanaweza kumudu gharama.
"Unakuta shule kuna miundombinu ya kutupia
taulo za kike zilizotumika lakini hakuna maji safi kwa ajili ya kujisafishia
wala chumba cha kujihifadhia chenye usiri hivyo inakuwa changamoto sana
kwetu,mfano wanaosoma shule za bweni ukikuta anatumia taulo za kike za kufua alafu
maji hamna inakuwa ni changamoto hivyo wadau na serikali itusaidia kuweka
mazingira rafiki ya kuwa na hedhi salama,"ameeleza Irene.
Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Mtoto,Mtandao wa Vijana na Watoto
Mwanza (MYCN)Nuru Massanja, ameeleza kuwa suala la hedhi salama siyo la watoto
wa kike na wanawake tu ni la kila mmoja serikali na jamii nzima katika
kuhakikisha mtoto wa kike anakuwa salama pale anapokuwa katika hedhi.
“Hivyo serikali ihakikishe watoto wa kike wanapata
maji salama wawapo shule kwa ajili ya kujisafishia pia hata nyumbani kuwe
na upatikanaji rahisi wa maji kwa serikali kusogeza huduma karibu maana
kuna kutumia taulo za kike za kufua ambazo zinahitaji maji ya kutosha kwa ajili
ya kuzifua kwa matumizi ya baadaye.”amesema Ofisa huyo
Ameongeza kuwa “Pia kuhakikisha kuna kuwa na vyoo
au vyumba vya kujihifadhia wakati wa hedhi wawapo shuleni vyenye usiri ambavyo
mtoto wa kike atakuwa uhuru kubadilisha taulo za kike bila mtu yoyote kufahamu
kama yupo hedhini.”
"Serikali iangalie miundombinu ya kutupa taka
yani taulo za kike zilizotumika ili baada ya kujisafishia anatupa uchafu kwenye
mazingira mazuri kuliko kuweka kwenye begi na kusubiria mpaka atoke shule
akatupe nyumbani,
“Mwingine hawezi kufanya hivyo anaona aibu na kuona
bora abaki nyumbani mpaka siku zake za hedhi zotakapoisha ndio aende shule
wakati huo anakuwa amepitwa na masomo," ameeleza Nuru
Akizungumzia suala la upatikanaji wa taulo za kike
Nuru ameeleza kuwa serikali ina nguvu kubwa katika kuzingatia bei kwani siyo
kila mzazi ana uwezo wa kununua taulo za kike kila mwezi kwa ajili ya binti
yake hususani vijijini .
Ameiomba Serikali iweke bei elekezi kwa wafanyabiashara
ambayo itaendana na uchumi wa Watanzania walio wengi pamoja na kuhakikisha
maeneo ya shule kwa kushirikiana na wadau zinapatikana bure wakati wote.
"Serikali iweke utaratibu wa kuhakikisha
watoto wa kike shuleni kwa kila shule wanapata taulo za kike ambazo watatumia
wawapo shuleni wakati wa hedhi ili kutokatisha
masomo kwa siku wanazokuwa hedhini pia hata kama mzazi wake ana fedha ya
kununua taulo za kike anajua akifika shule atazikuta hivyo kuendelea kusoma
katika mazingira salama yanayoendana na hedhi salama,"ameeleza Nuru.
Sanjari na hayo Nuru ametumia fursa hiyo
kuwahimiza wazazi,walezi na jamii kwa
ujumla kuzungumza na watoto wao siyo wa kike tu bali wote kuhusu hedhi salama
ili kuleta urahisi kwa mtoto wa kike kuwa katika mazingira rafiki.
"Kuwaelimisha watoto wote siyo wa kike pekee
kwani huwezi jua atakayemsaidia binti anapokuwa katika hedhi kwenye mazingira
ya shule au nyumbani kwani mtoto wa kiume akiwa anajua masuala kama hayo
itasaidia kuwa na mazingira mazuri kwa mtoto wa kike wakati wa hedhi,
“Pia elimu ya hedhi salama itawasaidia watoto
kutojiingiza katika masuala ya mapenzi kwani anatambua kuwa muda gani anaweza
kupata mabadiliko kwenye mwili na namna gani ya kujizuia,"ameeleza Nuru.
Mmoja wa wananchi wa Kata ya Nyamanoro Lydia Hugo,
ameeleza kuwa kukua kwa teknolojia kila
siku vitu vinabadilika hata vya kujihifadhia wakati wa hedhi tofauti na zamani
ambapo sasa zipo hadi taulo za kufua ambazo zinahitaji maji safi kwa ajili ya
kusafisha baada ya kutumia hivyo ni wakati wa serikali kuhakikisha upatikanaji
wa maji ya uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.
"Binafsi taulo za kufua zimenipunguzia gharama
ya kununua kila mwezi nanunua mara moja kwa mwaka na kutumia kwa muda wa zaidi
ya miezi 12, lakini changamoto ni maji hasa yanapokuwa ya mgao unashindwa kufua
vizuri hali ambayo ni hatari kwa afya,"ameeleza Lydia.
No comments:
Post a Comment