
Na Joyce Kasiki,DODOMA
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jaffo, amesema kuwa Tanzania imejipanga kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Dunia ya EXPO 2025 yatakayofanyika mjini Osaka, Japan kuanzia Aprili 12 hadi Oktoba 13, 2025 kwa lengo la kutangaza fursa za biashara, uwekezaji, utalii, pamoja na Mila na Utamaduni wa Taifa.
Akizungumza leo jijini Dodoma na waandishi wa habari, Dkt. Jaffo amesema EXPO ni maonesho makubwa ya kimataifa yanayoratibiwa na Bureau of International Exposition (BIE) ambapo nchi wanachama, ikiwemo Tanzania, hupiga kura kuchagua mwenyeji wa maonesho hayo.
“TanTrade kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, imekuwa ikiratibu ushiriki wa nchi yetu kwenye EXPO tangu mwaka 1967. Hadi sasa tumeshiriki katika EXPO takriban tisa, ikiwemo Expo 2020 Dubai na Expo ’70 Japan. Ushiriki huu umekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi,” alisema Waziri Jaffo.
EXPO 2025 Osaka inabeba kauli mbiu kuu isemayo “Kuwezesha jamii kwa Maisha Endelevu” ambapo Tanzania imechagua kaulimbiu ndogo ya “Kuunganisha Maisha – Connecting Lives” yenye malengo ya kuunganisha uzalishaji wa ndani na masoko ya nje, kuhamasisha uwekezaji, kuimarisha mawasiliano ya kiteknolojia, na kuchochea sekta ya utalii.
Dkt. Jaffo amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zaidi ya 160 zilizothibitisha ushiriki wake rasmi, na kwamba banda la Tanzania litakuwa na ukubwa wa mita za mraba 53 kwa ajili ya maonesho na mita za mraba 15 kwa ajili ya biashara.
“Kwa Expo 2025 Osaka, tuna matarajio makubwa zaidi. Tunaamini tutaongeza upatikanaji wa masoko ya bidhaa za Tanzania, kuimarisha uchumi wa nchi, na kuvutia wawekezaji wa kimkakati kupitia ushirikiano na sekta binafsi,” amesema Dkt. Jaffo.
Amesema maonesho hayo pia yataambatana na programu maalum za kila wiki, ikiwemo Utalii, Miundombinu, Kilimo na Uchumi wa Buluu, Afya, Sanaa na Utamaduni, Nishati na Sayansi na Teknolojia. Kila programu itaratibiwa na Wizara husika kwa kushirikiana na taasisi na sekta binafsi.
Aidha, Siku ya Tanzania katika EXPO hiyo imepangwa kufanyika Mei 25, 2025 ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa. Siku hiyo itafuatiwa na Kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii litakalofanyika Mei 26, 2025.
Waziri Jaffo alitoa wito kwa taasisi za umma, mashirika ya kimataifa na binafsi kushiriki kikamilifu katika maandalizi na maonesho hayo kwa kuwasilisha maudhui ya miradi ya kimkakati, kuthibitisha ushiriki katika programu na kongamano, pamoja na kuandaa mapendekezo ya maeneo ya ushirikiano na taasisi za Kijapani.
“Washiriki wote wanatakiwa kujisajili kupitia tovuti ya TANTRADE au kwa kutumia QR code inayotangazwa kupitia vyombo vya habari,” alihitimisha.
EXPO 2025 Osaka ni fursa adhimu kwa Tanzania kuonesha dunia nguvu yake ya kiuchumi, vivutio vyake vya kiutalii, pamoja na uwezo wake mkubwa katika ubunifu, teknolojia na maendeleo ya jamii.
No comments:
Post a Comment