
Na Adelina Johnbosco - MAELEZO
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema Wizara ya Habari ni muhimu sana katika nchi kutokana na majukumu yake ya uhabarishaji wa masuala mbalimbali katika kila nyanja ndani na nje ya Tanzania.
Amesema hayo leo Aprili 3, 2025 katika Hoteli ya New Amaan Zanzibar wakati akifungua Kikao Kazi cha 20 cha Maafisa Habari wa Serikali kitakachodumu hadi Aprili 6, 2025.
"Wizara ya Habari ina mambo mengi, na ndiyo roho ya nchi, wengine wanasema ni Wizara ya Fedha, lakini hata fedha zenyewe zinataka habari, unaweza kuwa nazo ukazitumia lakini bila ya habari zisionekane matumizi yake" amesisitiza Mhe. Abdulla
Vile vile, amewashukuru Maafisa Habari kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao ya kuuhabarisha umma na ulimwengu kwa ujumla kuhusu mafanikio ya Serikali.
"Kazi yenu Maafisa Habari imetukuka, imeifanya Tanzania kupata sifa kubwa, dunia inaendelea kupata habari za Tanzania, kuijua miradi yake hasa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)" ameongeza Mhe. Abdulla
Sanjari na hayo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amewataka walengwa wa Kikao Kazi hicho ambao ni Maafisa Habari wa Serikali nchi nzima, kuzitumia mada mafunzo zitakazowasilishwa ili kufanya kazi kwa utaalam na si kufanya kazi kwa mazoea.
..............Mwisho..........
No comments:
Post a Comment