MBUNGE WA GEITA VIJIJINI MUSUKUMA KASHEKU AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI NYUMBANI KWAKE JIJINI DODOMA |
NA JOYCE KASIKI,DODOMA
MBUNGE wa Geita Vijijini Joseph Musukuma
amesema,Serikali inapaswa kuwachukulia hatua watu wote wenye tabia ya kueneza uongo kwenye mitandao
ya kijamii pindi serikali inapotaka kufanya jambo lenye maslahi kwa nchi na hivyo
kuleta taharuki.
Musukuma ameyasema hayo kufuatia uvumi ulioenea
kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwekezaji unaotaka kufanywa na mwekezaji Ruler of Dubai katika Bandari ya Dar es Salaam huku akisema uwekezaji huo utakuwa na maslahi mapana
kwa nchi na siyo nchi kuuzwa kama inavyodaiwa kwenye mitandao hiyo.
“Hapa nchini kumekuwa na tabia ya watu kueneza
uvumi na uongo kila serikali inapotaka kutekeleza miradi yenye maslahi mapana
kwa nchi,nakumbuka hata wakati serikali ya awamu ya tano ilipotaka kutekeleza
miradi ya kimkakati watu walipiga makelele lakini sasa hivi ndiyp hiyo
tunayoitumia kupigia kampeni,tumwache Rais afanye kazi na atimize ndoto zake.”amesema
Musukuma
Amesema,wao kama Wabunge wanachojadili sasa ni
makubaliano ya nchi kwa nchi siyo kweli kwamba wanakwenda kupitisha azimio la
kumpa mwekezaji huyo Bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka 100.
“Sisi wabunge siyo wajinga tupitishe kitu ambacho
tunajua kinakwenda kuiumiza nchi,lakini hata Mama (Rais Samia Suluhu Hassan)
naye atatumikia nchi lakini baadaye ataastaafu,sasa akishastaafu yeye atakwenda
kuishi wapi mpaka aiingize nchi matatani”
Aidha Musukuma amesema,uwekezaji unaoenda kufanywa
kwenye Bandari hiyo bado haujajulikana ni wa muda gani lakini utakuwa na
maslahi mapana hasa kwenye mapato ambapo nchi inakwenda kuingiza kiasi cha
shilingi bilioni 38 kutoka shilingi bilioni 7 inayoingizwa sasa lakini pia
unakwenda kuongeza ajira kutoka 71,000 hadi ajira 128,000 .
Amesema,bandari yetu kwa sasa inapokea makontena
laki saba hadi laki nane lakini baada ya mwekezaji kuja tutakuwa tunapokea zaidi
ya makontena milioni moja huku akisema hii ni fursa kama nchi inapaswa
kuitumia.
“Bandari ni lango kuu la uchumi,tena mimi nilitamani
tukimaliza kufanya uwekezaji kwenye bandari,twende na Airport maana napo pana
mifumo mibovu.”amesisitiza
Hata hivyo amesema,uwekezaji huo unakwenda kuongeza
mapato huku akisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) haitaingiliwa kwenye
ukusanyaji wake wa mapato katika eneo hilo la Bandari.
Musukuma ametumia nafasi kuiomba Serikali ipeleke
waandishi nchini Dubai angalau 100 kutoka mikoa yote ili waende kujifunza
nchini humo na waweze kuelimisha vyema wananchi.
Aidha Musukuma amekanusha tuhuma zinazowahusisha
wabunge walioenda nchini Dubai kwa ziara ya mafunzo kwamba wamehongwa huku yeye
binafsi akihusishwa kuhongwa gari huku akisema tuhuma hizo hazina ukweli wowote
na kwamba gari linalosemwa alilinua kwa pesa yake na alilipa ushuru bandarini
kiasi cha shilingi milioni 130.
No comments:
Post a Comment