Na Joyce Kasiki ,Dodoma
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais ,Muungano na Mazingira Dkt.Selemani Jafo ameeelezea mafanikio lukuki ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akisema mafanikio hayo yamejidhihirisha katika awamu zote za uongozi.
Aidha amesema tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao vya pamoja mwaka 2006 hadi sasa, kasi ya utatuzi wa changamoto imeongezeka ambapo hoja 22 za Muungano zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 25 zilizoibuliwa.
Alisema changamoto nyingi ambazo zilikuwa hazijapatiwa ufumbuzi zimejadiliwa na pande zote mbili za Muungano na kupatiwa ufumbuzi ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 pekee hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo kwa kipindi hicho huku akisema hoja zilizobakia zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio hayo Dkt.Jafo alisema ,Mafanikio hayo yamejidhihirisha katika kuboresha hali ya nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii na kwamba Muungano umeendelea kudumishwa na hifadhi ya mazingira nchini imeimarika.
Mafanikio ya Kisiasa
Alisema Muungano huo umedumu kutokana na utashi wa dhati wa kisiasa hapa nchini waliokuwa nao Waasisi wa Muungano ambao uliwezesha vyama vya siasa vya TANU na ASP kuungana na baadaye kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM) Februari 5, 1977.
Alisema kuunganishwa kwa vyama hivyo kuliongeza ari ya umoja na ushirikiano baina ya watu wa Tanganyika na Zanzibar huku akisema , Muungano wa vyama hivyo umekuwa ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo wa kuwa na vyama vya siasa vya kitaifa na hivyo kukuza demokrasia, uhuru wa kutoa maoni na uwazi katika uendeshaji wa shughuli za kisiasa.
Mafanikio ya Kijamii
Alisema mafanikio hayo hasa katika eneo la ulinzi na usalama ,Serikali zote mbili zimefanikiwa kusimamia utekelezaji wa masuala yaMuungano kwa ufanisi mkubwa ikijumuisha kuimarika kwa utaifa, umoja, amani, utulivu na hali ya maisha ya wananchi kutokana na ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili za Muungano.
Huduma za Kijamii
Kuhusu huduma za kijamii Dkt.Jafo alisema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano mafanikio makubwa yamepatikana katika huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji, barabara, umeme, utoshelezi wa chakula pamoja na ustawi wa jamii kwa
ujumla.
“Kwa upande wa huduma za elimu, Shule za Msingi zimeongezeka kutoka shule 3,270 mwaka 1961 hadi shule 20,562 mwaka 2024. Kati ya hizo, shule za Serikali ni 18,012 na za binafsi ni shule 2,550. Shule za Sekondari nazo zimeongezeka kutoka shule 41 mwaka 1961 hadi shule 6,511 mwaka 2024,kati ya hizo, shule 4,892 ni za Serikali na 1,619 ni za binafsi.
Huduma za Afya
Huduma za afya zimeendelea kuimarika kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kipindi chote cha Muungano kutokana na uwekezaji huo, vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote vimeongezeka kutoka vituo 1,343 mwaka 1960 hadi vituo 9,662 mwaka 2024,kati ya vituo hivyo, Zahanati ni 8,043, Vituo vya Afya 1,176, Hospitali za Halmashauri 171, Hospitali zenye hadhi ya Wilaya 182, Hospitali za Rufaa za Mikoa 28; Hospitali zenye hadhi ya Mkoa 34; Hospitali za Rufaa za Kanda 5; Hospitali zenye hadhi ya Kanda 11; Hospitali maalumu 6; Hospitali ya Taifa 1; na Hospitali Maalumu za Taifa 6.
Aidha alitaja mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano kuwa ni kuimarika kwa upatikana wa huduma za maji, umeme na mtandao wa barabara.
Alisema upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 32 mwaka 2000 hadi asilimia 77 mwaka 2022. Aidha, upatikanaji wa umeme umeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2000 hadi 78 mwaka 2022.
Vile vile, mtandao wa barabara za lami na zege mijini na vijijini umeongezeka kutoka Kilomita 1,360 mwaka 1961 hadi Kilomita 11,966 mwaka 2022.
Mafanikio ya Kiuchumi
Tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 Tanzania imepata mafanikio ya makubwa kiuchumi ambapo alisema Takwimu zinaonesha kuwa mwenendo wa ukuaji wa uchumi katika kipindi cha miaka
60 umekuwa ni wa kuridhisha ambapo Pato Ghafi la Taifa limeendelea kukua na kufikia shilingi trilioni 170.3 mwaka 2022 kutoka shilingi trilioni 156.4 mwaka 2021.
Aidha alisema , Pato la Taifa kwa mtu limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia wastani wa shilingi 2,844,641 (sawa na dola za Marekani 1,229.1) mwaka 2022 kutoka wastani wa shilingi 2,708,999 (sawa na dola za Marekani 1,173.3) mwaka 2021.