Dkt.Ernest Ibenzi akizungumza na waandishi wa habari
Na Joyce Kasiki Dodoma
MGANGA Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Waganga wafawidhi hospitali za Rufaa za Mikoa 28 Tanzania Bara Dkt.Ernest Ibenzi amesema ,licha ya hospitali kususia kupokea wagonjwa wanaotumia Bima ya Afya kutokana na Serikali kuboresha kitita katika Bima hiyo,hospitali hizo zipo tayari na zimejipanga kuwahudumia wagonjwa kwa wakati ma bila kuchoka.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo,Dkt.Ibenzi amesema hospitali za Rufaa za Mikoa ikiwemo ya mkoa wa Dodoma zimejipanga na kuongeza muda wa kuwahufumia wagonjwa kwa kufanya kazi saa 24 huku madaktari bingwa wakipatikana muda wote.
"Hospitali za Rufaa za Mikoa wamekubaliana kwamba wataona wagonjwa wote bila kujali muda wa saa za kazi ndipo wafunge kutoa huduma tofauti na awali ambapo walihudumia wagonjwa mpaka saa tisa na nusu."amesema Dkt.Ibenzi na kuongeza kuwa
"Hospitali zote za Rufaa za Mikoa zina wataalam wa kutosha na zinahudumia wagonjwa wote wenye keshi,wanaohudumiwa kupitia Bima za Afya na wale wanaohitajji msamaha."
Aidha Dkt.Ibenzi amesema hali ya utoaji huduma katika hospitali hizo imeboreka kutokana na Serikali kutoa vifaa tiba na vitendanishi vya kutosha.
"Hospitali zote 28 za Rufaa za Mikoa Tanzania Bara zimejipanga kuwahudumia wagonjwa na hapa utaona hata katika huduma za kliniki tulikuwa tunaanza saa mbili asubuhi lakini sasa tumekubaliana kuanza huduma hizo saa moja na tutawaona wagonjwa wote mpaka wanapoisha ndipo tufunge na siyo kufunga saa tisa na nusu kama ilivyokuwa awali."amesema Dkt.Ibenzi
Ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kupeleka wataalam wa kutosha na hivyo kuwezesha wagonjwa kuhudumiwa kwa wakati na bila kuchoka.
No comments:
Post a Comment