NA JOYCE KASIKI,DODOMA
MAKAMU wa Rais Dkt.Philip Mpango ameoneshwa kuridhishwa na kazi
inayofanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) ya kuwaunganishia
wananchi gesi asilia kutoka kwenye bomba kuu.
Akizungumza wakati wa kukagua mabanda kwenye Kongamano la
Wanawake la Nishati safi ya kupikia, Dkt.Mpango amesema shirika hilo linafanya
kazi nzuri ambayo itachangia wananchi kuachana na nishati chafu ya kupikia.
Hata hivyo amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo
Mussa Makame kuhakikisha wanaendelea kusambaza gesi asilia kwa wananchi huku
akilitaka shirika hilo liangalie uwezekano wa njia za kulipatia pesa shirika
kwa ajili kuliongezea nguvu katika utekelezaji wa majukumu yake.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Makame amesema
shirika hilo limeanza safari ya
kuwezesha wananchi wa Mikoa ya Lindi,Mtwara,Pwani na Dar es Salaam kutumia gesi
asilia inayozalishwa hapa nchini.
Aidha amesema mpaka sasa wameshaunganisha takriban taasisi
13 zikiwemo baadhi ya magereza na shule pia wameunganisha wananchi 1500.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo amesema changamoto kubwa
wanayokabiliana nayo ni usambazaji wa gesi kwa bomba njia ambayo gharama yake
ni kubwa huku akisema wanaangalia uwezekano wa kusambaza gesi asilia kwa njia
ya mitungi ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kuhama kwenye matumizi ya kuni na
mkaa na badala yake waanze kutumia nishati safi ya kupikia.
No comments:
Post a Comment