
Joyce Kasiki,Dodoma
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza bidhaa mbalimbali zisizokidhi viwango ya ubora vyenye thamani ya Shilingi bilioni 1.5 kati ya Julai na Disemba 2024, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda afya na usalama wa watumiaji pamoja na kuzuia uingizaji wa bidhaa hafifu nchini.
Hayo yamesemwa Jana jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo hasa katika kipindi Cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Dkt.Katunzi alisema kuwa, bidhaa hizo ziliteketezwa baada ya kukutwa na kasoro mbalimbali, zikiwemo kutokuwa na viwango vya ubora vinavyotakiwa, kuwa na viambato hatarishi kwa afya, ama kuingizwa nchini bila kufuata taratibu za kisheria.
“Katika kipindi cha miezi sita, tumeteketeza bidhaa zenye thamani ya Shilingi bilioni 1.5, ikiwa ni hatua madhubuti ya kuzuia bidhaa zisizofaa kufika kwa watumiaji,hii ni sehemu ya mkakati wa TBS wa kuhakikisha soko la Tanzania linakuwa na bidhaa salama na bora kwa wananchi,” alisema Dkt. Katunzi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, bidhaa zilizoteketezwa ni pamoja na vipodozi vyenye viambato vilivyopigwa marufuku, chakula kilichoisha muda wake, vifaa vya umeme visivyokidhi viwango, pamoja na bidhaa nyingine zisizo na usajili wa ubora kutoka TBS.
Alisema, shirika hilo limeendelea kuimarisha mifumo yake ya ukaguzi wa bidhaa zinazoingia nchini, ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia za kisasa katika maabara zake 12 ambazo zote zimepata ithibati ya kimataifa.
Dkt. Katunzi aliongeza kuwa hatua hii imewezesha kubaini kwa haraka bidhaa hafifu na kuzuia zisifike kwa watumiaji.
Mbali na ukaguzi wa bidhaa zinazoingizwa nchini, pia TBS imeendelea kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa ndani ili kuhakikisha wanazalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, shirika hilo limeandaa viwango 1,823 vya sekta mbalimbali na kutoa vyeti na leseni za ubora 2,402 kwa wazalishaji, wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,066.
Aidha, TBS imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali, vyuo vikuu, na mashirika ya kimataifa ili kuhakikisha mifumo yake ya udhibiti ubora inazidi kuwa na ufanisi mkubwa.
Kwa upande wa wananchi, Dkt. Katunzi aliwataka kuwa makini wanaponunua bidhaa kwa kuhakikisha zinakuwa na alama ya ubora ya TBS na kuepuka bidhaa zisizo na usajili wa shirika hilo. Pia alihimiza wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapobaini bidhaa zisizokidhi viwango zikiuzwa sokoni.
Alisema, TBS litazidi kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wanaoingiza au kusambaza bidhaa hafifu nchini, ikiwa ni pamoja na kutaifisha na kuteketeza bidhaa hizo, pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wote.
No comments:
Post a Comment