Kapinga amtilia shaka MF Contractor






Published from Blogger Prime Android App



Na Joyce Kasiki,DODOMA


NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukutana na Mkandarasi MF anayetekeleza mradi wa umeme katika vijiji 15 vya Wilaya ya Nyasa, ili kuangalia uwezekano wa kuteua wakandarasi wadogo (sub-contractors) kutokana na udhaifu wa mkandarasi huyo katika utekelezaji wa kazi.

Kapinga alitoa maelekezo hayo kufuatia swali la nyongeza lililoulizwa Bungeni jijini Dodoma Aprili 24,2025 na Mbunge wa Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, ambaye alitaka wakandarasi waondolewe kutokana na kutokuwepo kwa maendeleo yoyote ya kazi katika maeneo husika.

"Pamoja na pongezi kwa Wizara ya Nishati, lakini kwa kuwa vitongoji vyote vilivyopangiwa kupata umeme awamu hii kupitia wakandarasi MF na Triple C (CCC), hakuna hata kimoja kilichowashiwa umeme. Kwa nini wasiondolewe na kuwekwa wakandarasi wenye uwezo?" alihoji Manyanya.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri Kapinga alifafanua kuwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa vitongoji hivyo ni kampuni ya CCC na alimtaja kuwa ni mkandarasi mzuri, ambaye kwa sasa yupo katika hatua za manunuzi na atatembelea eneo la mradi hivi karibuni.

Hata hivyo, kuhusu Mkandarasi MF, Kapinga alisema:
"Namuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa REA, na tayari tulishazungumza, afanye utaratibu wa kukutana naye ili watafute 'sub-contractors' kwa sababu uwezo wake tayari unatia mashaka. Tutasimamia hili kwa karibu ili kuhakikisha kuwa mradi unakamilika kwa wakati." alisisitiza Kapinga.



Share:

Serikali yaombwa kupeleka maji Tukuyu Kutoka Ziwa Nyasa




Published from Blogger Prime Android App



DODOMA

MBUNGE wa Viti Maalum Sophia Mwakagenda ameiomba Serikali kupeleka maji Mji wa Tukuyu Kutoka Ziwa Nyasa Ili kusaidia wananchi wa wilaya hiyo kupata maji safi na salama.

Akiuliza swali la nyongeza Bungeni jijini Dodoma Mwakagenda amesema  Mji wa Tukuyu hauna maji huku alihoji lini Serikali itapeleka fedha ili kujenga mradi wa kutoa maji Ziwa Nyasa na kuyafikisha Mji wa Tukuyu.

"Kama ilivyo kwa ziwa Victoria, tuna Ziwa Nyasa na Mji wa Tukuyu hauna maji, ni lini Serikali italeta fedha kuhakikisha maji yanatoka Ziwa Nyasa Hadi kufika  Tukuyu?

Akijibu swali hilo Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema Moja ya mikakati iliyopo Serikalini ni kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zinatumika na kutatua changamoto za wananchi.

"Nimhakikishie Mheshimiwa  Mbunge kwamba Moja ya mikakati na maelekezo ni kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zinatumika na kutatua matatizo ya maji,kwa  hiyo maeneo ya Ziwa Nyasa ni moja ya mikakati ya Wizara ,na Wizara ipo katika hatua mbalimbali kufanya 'visibility Study' ,naamini wananchi wa maeneo hayo pia watanufaika kupata Huduma ya maji safi na salama."amesisitiza Aweso
Share:

Sekiboko ahoji mkakati wa Serikali kuboresha soko la machungwa Tanga




Published from Blogger Prime Android App



MBUNGE wa Viti Maalum Husna Sekiboko amehoji hatua zinazochukukiwa na Serikali Ili kulinda Kilimo Cha matunda kwa lengo lai kuokoa soko la matunda linalosuasua kutokana na uingizaji mkubwa wa matunda nchini.

Akiuliza swali Bungeni Sekiboko pia amesema "Mkoa wa Tanga ni maarufu kwa Kilimo cha matunda hasa machungwa lakini bado hayajapati soko zuri kwenye viwanda,ni upi mkakatii wa Serikali katika kuboresha Kilimo Cha matunda ili kuweza kukidhi mahitaji ya viwandani?amehoji Sekiboko na kuongeza kuwa 

"Pamekuwa na changamoto kubwa ya kuoza matunda kabla ya kufika sokoni ,ni upi mkakati wa Serikali wa kujenga vyumba baridi kwa ajili ya kuhifadhi matunda ."

Akijibu maswali hayo ,Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde amesema katika  kulinda soko na kudhibiti uingiaji holela wa matunda nchini, Serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) ambayo itaweka utaratibu wa kuwezesha uingizaji na usafirishaji nje wa mazao ya nafaka na mazao mchanganyiko yakiwemo matunda.

"Pia imeamasisha uanzishaji wa viwanda vya kusindika matunda ili kuimarisha soko la ndani na kupunguza upotevu,kutoa ruzuku ya pembejeo kwa mazao ya matunda ikiwemo maembe, machungwa na parachichi ili kuongeza tija na kuimarisha utafiti na uzalishaji wa mbegu na miche bora ya matunda kulingana na mahitaji ya soko.

 Aidha Silinde amemthibitishia Mbunge huyo kwamba Serikali, inatambua mkoa wa Tanga ni Moja ya Mkoa unaotegemewa  kwa Kilimo cha machungwa .

"Tunakiri kwamba kuna changamoto kubwa ya kuoza kwa matunda hayo ambayo imekuwa ni Moja ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kuokoa matunda hayo ambapo kazi kubwa iliyofanyika sasa hivi ni kuhamasisha sekta Binafsi kuingia katika kujenga viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao haya kama vile Kutoka katika tunda kuwa juisi  na Tanga ndio mkoa ambao sasa hivi tumeuweka kwenye mkakati huo."amesema Silinde

Kuhusu kuoza mazao amesema,Serikali inao Mpango madhubuti na tayari  imepata fedha kwa ajili ya kujenga vyumba baridi kwa ajili ya kuhifadhi haya matunda
Share:

Tanzania ilivyojidhatiti maonesho ya Expo 2025 Osaka,Japan






Published from Blogger Prime Android App



Na Joyce Kasiki,DODOMA

WAZIRI  wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jaffo, amesema kuwa Tanzania imejipanga kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Dunia ya EXPO 2025 yatakayofanyika mjini Osaka, Japan kuanzia Aprili 12 hadi Oktoba 13, 2025 kwa lengo la kutangaza fursa za biashara, uwekezaji, utalii, pamoja na Mila na Utamaduni wa Taifa.

Akizungumza leo jijini Dodoma na waandishi wa habari, Dkt. Jaffo amesema EXPO ni maonesho makubwa ya kimataifa yanayoratibiwa na Bureau of International Exposition (BIE) ambapo nchi wanachama, ikiwemo Tanzania, hupiga kura kuchagua mwenyeji wa maonesho hayo.

“TanTrade kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, imekuwa ikiratibu ushiriki wa nchi yetu kwenye EXPO tangu mwaka 1967. Hadi sasa tumeshiriki katika EXPO takriban tisa, ikiwemo Expo 2020 Dubai na Expo ’70 Japan. Ushiriki huu umekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi,” alisema Waziri Jaffo.

EXPO 2025 Osaka inabeba kauli mbiu kuu isemayo “Kuwezesha jamii kwa Maisha Endelevu” ambapo Tanzania imechagua kaulimbiu ndogo ya “Kuunganisha Maisha – Connecting Lives” yenye malengo ya kuunganisha uzalishaji wa ndani na masoko ya nje, kuhamasisha uwekezaji, kuimarisha mawasiliano ya kiteknolojia, na kuchochea sekta ya utalii.

Dkt. Jaffo amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zaidi ya 160 zilizothibitisha ushiriki wake rasmi, na kwamba banda la Tanzania litakuwa na ukubwa wa mita za mraba 53 kwa ajili ya maonesho na mita za mraba 15 kwa ajili ya biashara.

“Kwa Expo 2025 Osaka, tuna matarajio makubwa zaidi. Tunaamini tutaongeza upatikanaji wa masoko ya bidhaa za Tanzania, kuimarisha uchumi wa nchi, na kuvutia wawekezaji wa kimkakati kupitia ushirikiano na sekta binafsi,” amesema Dkt. Jaffo.

Amesema maonesho hayo pia yataambatana na programu maalum za kila wiki, ikiwemo Utalii, Miundombinu, Kilimo na Uchumi wa Buluu, Afya, Sanaa na Utamaduni, Nishati na Sayansi na Teknolojia. Kila programu itaratibiwa na Wizara husika kwa kushirikiana na taasisi na sekta binafsi.

Aidha, Siku ya Tanzania katika EXPO hiyo imepangwa kufanyika Mei 25, 2025 ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa. Siku hiyo itafuatiwa na Kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii litakalofanyika Mei 26, 2025.

Waziri Jaffo alitoa wito kwa taasisi za umma, mashirika ya kimataifa na binafsi kushiriki kikamilifu katika maandalizi na maonesho hayo kwa kuwasilisha maudhui ya miradi ya kimkakati, kuthibitisha ushiriki katika programu na kongamano, pamoja na kuandaa mapendekezo ya maeneo ya ushirikiano na taasisi za Kijapani.

“Washiriki wote wanatakiwa kujisajili kupitia tovuti ya TANTRADE au kwa kutumia QR code inayotangazwa kupitia vyombo vya habari,” alihitimisha.

EXPO 2025 Osaka ni fursa adhimu kwa Tanzania kuonesha dunia nguvu yake ya kiuchumi, vivutio vyake vya kiutalii, pamoja na uwezo wake mkubwa katika ubunifu, teknolojia na maendeleo ya jamii.
Share:

Rais Samia aitaka Mahakama kutenda haki bila kuangalia hali ya mtu




Published from Blogger Prime Android App


Na Mwandishi wetu, DODOMA 

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka watendaji wa Mahakama kuhakikisha kasi ya utoaji haki kwa wananchi inaendana na ubora wa jengo jipya  la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania ambalo limejengwa kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Dkt.Samia ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo hilo  sambamba na jengo la Utumishi wa Mahakama na Makazi ya Majaji ambayo yote kwa pamoja yamegharimu kiasi Cha shilingi bilioni 185.4.

Amesema kuwa na majengo mazuri ni kwa ajili ya kujenga mazingira mazuri ya utendaji kazi hasa ya utoaji haki kwa wananchi.

Dkt.Samia amesema,mazingira hayo mazuri yaendane na ubora wa huduma zinazotolewa katika majengo hayo .

Amesema ,Serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga mazingira mazuri ya utendaji kazi kwa Majaji hapa nchini na kuwataka nao kufanya kazi ya utoaji haki bila kuangalia Hali ya mtu.

Aidha Dkt Samia ameipongeza Mahakama kwa  ujenzi wa jengo hilo  ambalo limezingatia matumizi ya TEHAMA huku akionyesha kufurahishwa na Mifumo ya Mahakama kusomana.

Amesema ,Mifumo hiyo inamwezesha mtu kuangalia mwenendo wa kesi katika mkoa wowote anaoutaka.

Ametumia nafasi hiyo kuhimiza Mahakama kuendelea kuifanya Mifumo yake kusomana Ili kurahisisha kazi ya utoaji haki na kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani.

Amesema,kwa upande wa Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya Mahakama Kila mwaka Kutoka bilioni 161 Hadi shilingi bilioni 321 mwaka huu wa fedha kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wa Mahakama.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Prof.Ibrahim Hamis Juma ameishukuru Serikali kwa kuiwezesha Mahakama kupata jengo hilo zuri na hivyo Makao Makuu ya Mahakama kuhamia Dodoma.

"Tunashukuru mheshimiwa Rais kwa kuiwezesha Mahakama kufanya maboresho kupitia mipango yake  ,bila uwezeshaji mipango yetu ingebaki kwenye makaratasi."alisema Prof.Ibrahim

Share:

Wizara ya Habari Ndiyo Roho ya Nchi - Mhe. Abdulla



Published from Blogger Prime Android App


Na Adelina Johnbosco - MAELEZO

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema Wizara ya Habari  ni muhimu sana katika nchi kutokana na majukumu yake ya uhabarishaji wa masuala mbalimbali katika kila nyanja ndani na nje ya Tanzania. 

Amesema hayo leo Aprili 3, 2025 katika Hoteli ya New Amaan Zanzibar wakati akifungua Kikao Kazi cha 20 cha Maafisa Habari wa Serikali kitakachodumu hadi Aprili 6, 2025.

"Wizara ya Habari ina mambo mengi, na ndiyo roho ya nchi, wengine wanasema ni Wizara ya Fedha, lakini hata fedha zenyewe zinataka habari, unaweza kuwa nazo ukazitumia lakini bila ya habari zisionekane matumizi yake" amesisitiza Mhe. Abdulla 

Vile vile, amewashukuru Maafisa Habari kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao ya kuuhabarisha umma na ulimwengu kwa ujumla kuhusu mafanikio ya Serikali.

"Kazi yenu Maafisa Habari imetukuka, imeifanya Tanzania kupata sifa kubwa, dunia inaendelea kupata habari za Tanzania, kuijua miradi yake hasa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)" ameongeza Mhe. Abdulla

Sanjari na hayo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amewataka walengwa wa Kikao Kazi hicho ambao ni Maafisa Habari wa Serikali nchi nzima, kuzitumia mada mafunzo zitakazowasilishwa ili kufanya kazi kwa utaalam na si kufanya kazi kwa mazoea.

..............Mwisho..........






Share:

Maafisa Habari, Kikao Kazi Hiki ni cha Mafundo na Mazingativu - Msigwa

Published from Blogger Prime Android App




Na Adelina Johnbosco - MAELEZO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amewataka Maafisa Habari wa Serikali kutambua kwamba, ujio wao Zanzibar katika Kikao Kazi ni kwa ajili ya kufundwa na kuzingatia yote yatakayoelekezwa na kukumbushwa juu ya utekelezajiwa majukumu yao.

Bw. Msigwa ametanabahisha hayo wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha 20 cha Maafisa Habari wa Serikali kinachofanyika katika Hoteli ya New Amaan Zanzibar, leo Aprili 3, 2025.

"Hiki ni kikao cha mafundo na mazingativu, tunafundana na kuzingatia mafundo kwa Maafisa Habari, Mawasiliano, Uhusiano na Itifaki wa Serikali" amesisitiza Bw. Msigwa

Aidha, ametaja malengo ya Kikao Kazi hicho kwa Maafisa Habari wa Serikali kuwa ni kuimarisha mawasiliano ya Serikali kwa umma kupitia programu za kujenga uwezo kwa watumishi pia kuimarisha Muungano na kubadilishana uzoefu.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Tabia Maulid Mwita, ameshukuru kukubaliwa ombi lake la Kikao Kazi hicho kufanyika Zanzibar na kutaja sababu kuu ya kufanya hivyo ikiwemo Maafisa Habari kujionea shughuli mbalimbali za utalii, michezo na maendeleo makubwa ndani ya Zanzibar. 

"Lengo kubwa la kuomba Kikao Kazi hiki kufanyika Zanzibar ni kuendelea kuimarisha Muungano wetu, pili ni kuwawezesha Maafisa Habari kuja kuiona Zanzibar ya sasa ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi, hivyo watapata kibali cha kuisemea Zanzibar kule Tanzania Bara na duniani kote" - Mhe. Tabia

Vile vile ameahidi kwamba, Wizara yake ya Habari Tanzania Zanzibar itaendelea kushirikiana na Wizara ya Habari Tanzania Bara katika nyanja zote zinazohusu sekta ya Habari nchini.

Wakati mafundo hayo yakiendelea, kikao hicho kimetoa fursa ya upimaji wa afya bure kwa wadau wote wa habari wanaoshiriki kikao hicho na wananchi watakaofika katika viwanja vya Hoteli ya New Amaan ambapo madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, MOI, JKCI na Lumumba wanaendelea kutoa huduma za afya za kibingwa kuanzia leo Aprili 3, 2025 hadi ukomo wa kikao hicho Aprili 6, 2025.

...........Mwisho.......






Share:

Wahitimu kidato cha nne waaswa kubadilisha Tahasusi kabla ya muhula wa masomo 2025 kuanza


Published from Blogger Prime Android App







Published from Blogger Prime Android App

Published from Blogger Prime Android App



Na Mwandishi Wetu,Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa,amewataka wahitimu wa kidato Cha nne  kwa mwaka 2024 ,kufanya mabadiliko ya tahasusi (combination) kulingana na ufaulu wao utakaowawezesha kuoangiwa kidato Cha Tano na vyuo kwa mwaka 2025.

Amesema zoezi hilo la kubadili tahasusi limeanza Machi 31 na litafunhwa  April 31 mwaka huu .

Mchengerwa ameyasema hayo  jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa kwa wahitimu wa kidato Cha mwaka 2024 kufanya mabadiliko ya tahasusi za kidato Cha Tano na kozi za vyuo kwa njia ya mtandao kwenye mfumo wa Uchaguzi wa wanafunzi wa kidato Cha Tano na vyuo mwaka 2025.

"Leo nimewaita hapa kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu kwa wahitimu wa Kidato cha Nne mwaka 2024 kuhusu fursa ya kubadilisha machaguo ya Tahasusi za Kidato cha Tano na Vyuo vya Kati na Elimu ya Ufundi kwenye mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Tano na Vyuo."amesema Mchengerwa

Amesema hayo ni  maandalizi ya awali ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Serikali Mwaka, 2025. 

Waziri Mchengerwa alisema, Serikali imekuwa ikitoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya Tahasusi (combination) na Kozi mbalimbali walizozichagua kupitia Fomu ya Uchaguzi .

Amesema,fursa hiyo huwawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).

Aidha amesema,Serikali kupitia Ofisi ya Rais  TAMISEMI imekamilisha zoezi la awali la kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye Fomu za Uchaguzi za wanafunzi kama zilivyojazwa na wanafunzi wakiwa shuleni. 

"Kukamilika kwa zoezi hili kunatoa fursa kwa wanafunzi kuweza kufanya mabadiliko ya machaguo/ tahasusi/ kozi kwa njia ya mtandao ambapo baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kanzidata hiyo ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia nafasi za Kidato cha Tano na Kozi mbalimbali katika Vyuo vya Kati na vya Elimu ya Ufundi kwa kuzingatia sifa za ufaulu na machaguo yao. "Amesema

Amesema,Ofisi ya Rais  TAMISEMI inatoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya sekondari Kidato cha Nne, mwaka 2024 kubadili machaguo yao ili kutoa nafasi zaidi kwa mwanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalamu stahiki katika maisha yake ya baadaye. 

Kwa.mujibu wa Mchengerwa,zoezi hilo litatoa fursa zaidi ya wanafunzi kuongeza machaguo na kufanya machaguo mapya ya Tahasusi na Kozi.

Amewaasa   wazazi/ walezi kushiriki katika zoezi hili kwa kushauriana na watoto wao katika kufanya machaguo sahihi kulingana na ufaulu wao lakini pia,amewahimiza  wahitimu wote  kufanya marekebisho ya machaguo ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao, kwa kuingia kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi unaopatikana kupitia kiunganishi cha selform.tamisemi.go.tz

Aidha amesema,maelekezo kwa wahitimu na jinsi ya kufanya mabadiliko watayapata kwenye mfumo kupitia 'user manual' pamoja na video ya youtube zilizopo kwenye mfumo huo.

Amesema,ili kuingia kwenye mfumo  mhitimu anapasqa atumie Namba yake ya  Mtihani wa kuhitimu Kidato cha Nne mwaka 2024, Jina lake la Mwisho, Mwaka wa Kuzaliwa na Alama ya Ufaulu aliyopata kwenye somo atakaloulizwa na mfumo au swali lolote atakaloulizwa.

"Ni matumaini yangu kuwa wahitimu wote watatumia kwa ukamilifu fursa waliyopewa ya kubadilisha Tahasusi na Kozi kulingana na ufaulu waliopata na pia wataweza kusoma tahasusi/kozi ambazo wamefaulu vizuri ama wana malengo nazo zaidi. "

Waziri huyo amewasisitiza wasisitiza wanafunzi, wazazi/ walezi kutumia muda huo vyema ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza mara baada ya matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo kutangazwa huku akisema ni muhimu kuzingatia muda uliotolewa wa kufanya marekebisho ili ratiba ya kuwachagua na kuwapangia shule na vyuo iweze kuendelea kwa muda uliopangwa. 

Aidha ameema huduma hiyo ya kubadilisha tahasusi ni bure na endapo wanafunzi watapata changamoto, wawasiliane na Dawati la Huduma la Mteja kupitia barua pepe: huduma@tamisemi.go.tz au kuwasiliana moja kwa moja na Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa simu +255 262 160 210 na +255 735 160 210. 

Aidha alisema, pamoja na maelekezo hayo, kwa mwanafunzi, mzazi/mlezi atakayekuwa na suala linalohitaji maelezo au ufafanuzi zaidi aende katika Ofisi za Elimu za Mikoa na Halmashauri.



Share:

Nderiananga aongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa tatu wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu Ujerumani

Published from Blogger Prime Android App


Published from Blogger Prime Android App


Published from Blogger Prime Android App




NA. MWANDISHI WETU BERLIN – UJERUMANI


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu unaofanyika jijini Berlin, Ujerumani tarehe 2 hadi 3 April,2025. 

Mkutano huo umeandaliwa na Shirikisho la Kimataifa wa Watu Wenye Ulemavu (IDA), Serikali ya Ujerumani, na Serikali ya Jordan na kufunguliwa rasmi kwa pamoja na Kansela wa Ujerumani Mhe. Olaf Scholz na Mfalme Abdullah II wa Jordani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano huo Mhe. Scholz amesisitiza juu ya umuhimu wa kushirikiana kimataifa kukuza haki na ujumuishaji wa masuala ya Watu Wenye Ulemavu.

“Ushirikiano wa kimataifa ni nguzo muhimu katika kuhakikisha haki na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu unatekelezwa kikamilifu duniani kote kwa kushirikiana, serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, taasisi za elimu, mashirika ya kiraia, na Mashirika ya Watu Wenye Ulemavu tunaweza kuunda sera na mipango madhubuti inayohakikisha usawa wa fursa na ushiriki kamili wa watu wenye ulemavu katika jamii, “ alisisitiza.

Naye Mfalme Abdullah II wa Jordani akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo alisisitiza dhamira ya dhati ya kuendeleza haki na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu.

Mfalme Abdullah II alitilia mkazo umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuhakikisha fursa sawa na ushiriki kamili wa watu wenye ulemavu katika nyanja zote za jamii.

Mkutano huo unalenga kuhamasisha juhudi za kimataifa katika kufanikisha ujumuishaji wa watu wenye ulemavu duniani na kuwaleta pamoja wadau wa ngazi za juu kujadili na kushiriki maendeleo katika ujumuishaji wa watu wenye ulemavu, kutoka serikalini, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, taasisi za elimu ya juu, mashirika ya kiraia na mashirika ya watu wenye ulemavu kutoka nchi mbalimbali.

Mkutano wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu (GDS) ni jukwaa la kipekee la kimataifa linaloangazia uboreshaji wa maisha ya watu wenye ulemavu, hususan kutoka Kusini mwa Dunia. 

Mkutano huo ulianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kuwakutanisha wadau wa kimataifa, kikanda, na kitaifa wanaoshiriki malengo na maono ya maendeleo jumuishi kwa watu wenye ulemavu na hatua za kibinadamu.

Mkutano huu unalenga kuziba pengo kati ya nyanja mbili za ujumuishaji watu wenye ulemavu na ushirikiano wa maendeleo.

Mkutano wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu hufanyika kila baada ya miaka mitatu ni jukwaa linalohusisha utetezi wa mara kwa mara na wadau wa maendeleo ya wenye ulemavu kimataifa pamoja na kuhamasisha vuguvugu la haki za watu wenye ulemavu na washirika wake duniani.

Mkutano huo pia unaangalia namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama na Mashirika ya Watu Wenye Ulemavu (OPDs) kupitia mipango ya pamoja ya uandaaji wa mkutano.




































Share:

Theme Support

Need our help to upload or customize this blogger template? Contact me with details about the theme customization you need.

Labels

Recent Posts

Unordered List

  • Lorem ipsum dolor sit amet, consectetuer adipiscing elit.
  • Aliquam tincidunt mauris eu risus.
  • Vestibulum auctor dapibus neque.

Pages

Theme Support

Need our help to upload or customize this blogger template? Contact me with details about the theme customization you need.