Afisa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma ACI Bahati Mwaifuge akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake.
JOYCE KASIKI,DODOMA
JESHI la Uhamiaji mkoa wa Dodoma limewakamata raia watano wa Ethiopia ambao wameingia nchini kinyume cha sheria na taratibu za nchi .
Aidha jeshi hilo linamshikilia raia mmoja wa Tanzania mwenye umri wa miaka 43 aliyefahamika kwa jina la Tito Mbwilo aliyekuwa anawasafirisha raia hao wa Ethiopia (wahamiaji haramu) kwa kutumia gari yenye namba za usajili T 991 DXB TOYOTA RUMIONI .
Akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake Afisa Uhamiaji mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji (ACI) Bahati Mwaifuge amesema ,mtanzania huyo alikuwa akiwasafirisha wahamiaji hao haramu kwenda Tunduma katika mkoa wa Songwe ili wavuke kwenda nchini Afrika ya Kusini.
“Katika uchunguzi wetu tumebaini kuwa bwana Tito Steven Mbwilo ana makazi sehemu mbili ambayo ni Iringa na Tunduma ili iwe rahisi katika kufanikisha biashara yake haramu.”amesema ACI Mwaifuge
ACI Mwaifuge amesema mtuhumiwa huyo alipokamatwa alijaribu kutoroka lakini Askari wa Uhamiaji walimdhibiti na kumuweka chini ya ulinzi.
ACI Mwaifuge ametoa onyo kwa wasafirishaji wote wanaojihusisha na wahamiaji haramu katika mkoa wa Dodoma kuacha vitendo hivyo mara moja huku akisema Jeshi hilo limegundua kuwa wamebadili mbinu kutoka magari makubwa na kutumia magari madogo .
“Kwa sababu wamebadili mbinu hizo tutaendelea kuwakamata na hata wakibadili mbinu zingine pia tutawakamata tuu.”amesisitiza ACI Mwaifuge
No comments:
Post a Comment