Mhasibu Kitengo cha Mapato wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Osward Mobily akiwa katika banda la TARURA jijini Dodoma akionyesha maeneo ambayo Ttarura iinayafanyia kazi.
Afisa Uhusiano wa TARURA Theresia Chimagu akimpa kipeperushi mteja aliyefika katika banda la TARURA jijini Dodoma. |
JOYCE KASIKI,DODOMA
MFUMO wa malipo ya kielektroniki wa maegesho ya magari unatarajiwa kufikia mikoa yote hapa nchini ifikapo Juni 2022 ili mfumo huo uanze kutumika kote nchini kwa lengo la kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato ya maegesho ya magari.
Hayo yamesemwa jijini hapa na Mhasibu Kitengo cha Mapato kutoka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Osward Mobily wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya Usalama na Afya Mahali pa kazi huku akisema kwa sasa mfumo huo umeshafika katika mikoa 10 hapa nchini.
Ameitaja mikoa ambayo mfumo huo tayari umeshaanza kufanya kazi kuwa ni pamoja na Iringa,Singida,Dodoma,Mwanza,Dar es Salaam,Pwani,Morogoro,Tanga,Kilimanjaro na Mbeya.
Mobily amesema ,TARURA wameanzisha mfumo huo ili kukoa mapato ambayo yamekuwa yakipotea kutokana na pesa zinazokusanywa kupita kwenye mikono mingi na kusababisha upotevu kabla ya kufika panakohusika.
Ametumia nafasi hiyo kuelezea mafanikio katika mikoa ambayo imeshaanza kuutumia mfumo huo huku akisema,mfumo umeonyesha mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato ya maegesho ya magari ikilinganishwa na ushuru wa maegesho ulivyokuwa unakusanywa kupitia kwenye mikono ya watu.
“Ndio maana mfumo ulifanyiwa majaribio katika mikoa michache na kuanza kuongezwa mikoa mingine ambapo hadi sasa kuna mikoa kumi ambayo mfumo umewekwa na tayari kuna mikoa ambayo ipo kwenye mchakato wa kuongezwa kwenye matumizi ya mfumo huo ambapo itaongezwa mikoa mitano mitano kwa awamu mpaka kukamilika mikoa yote.”amesema Mobily
Kwa mujibu wa Mobily mfumo wa awali uliokuwa unahusisha kupokea fedha taslim, kulikuwa kuna ucheleweshwaji na upotevu wa fedha kutokana na kupita katika mikono ya watu wengi ambapo ilikuwa inapunguza usalama wake tofauti na mfumo mpya wa kidigitali ambao muhusika akishalipa fedha ile inaenda moja kwa moja kwenye mfuko wa Serikali.
“Kwa hiyo fedha zinakuwa zinapatikana kwa wakati na zinaenda kufanya shughuli zilizokusudiwa ikiwemo uboreshaji wa barabaraza mijini na Vijijini .”amesisitiza Mobily
Akizungumzia changamoto za mfumo wa awali amesema,kulikuwa na wateja ambao wanaondoka bila kulipa ushuru licha ya kuandikiwa risiti lakini kwa mfumo huu imekuwa ni rahisi kwa sababu chombo kikifika tu kinachukuliwa taarifa na kutengenezewa Ankara ya kudaiwa .
Vile vile amesema,kulikuwa na usumbufu kwa wanaokusanya ushuru dhidi ya wenye vyombo vya moto kutaka mazungumzo hali ambayo kwa sasa haipo kwani haihusishi na kuchukua fedha taslim,hivyo hakuna mazungumzo yoyote huku akisema hatua hiyo imerahisisha na imeongeza ufanisi ambao umepelekea makusanyo kuongezeka kwa asilimia 40 ikilinganishwa na makusanyo yaliyokuwa yanapatikana awali.
Hata hivyo Mobily amesema,bado kuna uhitaji wa elimu ya mfumo mpya kufika kwa watumiaji wa vyombo vya moto ili kuuelewa vizuri mfumo huo na kuondoa changamoto katika utekelezaji wake.
“Wananchi bado wanahitaji elimu kwani bado haijawafikia vya kutosha ,kwa hiyo kwa sehemu kubwa tunahitaji nguvu kubwa ya kuwekeza kwenye utoaji wa elimu na kuhakikisha mmiliki wa chombo cha moto anakuwa na uelewa dhidi ya mfumo huu lakini pia watu wetu wanaofanya ile kazi tuwaongezee uelewa zaidi ili wawe mabalozi wazuri wanapokutana na wateja kwani wao ndio wanakutana na wateja moja.”
Hata hivyo amesema , tayari wameshaanza kufanyia kazi changamoto zote zinazoukabili mfumo ili kuufanya kuwa na tija kwa wateja na Taifa kwa ujumla.
Mobily amesema TARURA pia imejikita zaidi katika utengenezaji,usanifu na maboresho ya miundombinu ya barabara za mijini na vijijini ili ziweze kupitika vizuri katika majira yote ya mwaka.
Maonyesho hayo yanafanyika Jijini Dodoma katika viwanja vya Jakaya Kikwete ambapo yameandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi (TUCTA) na Wakala wa Usalama na Afya mahala pa kazi.
No comments:
Post a Comment