AFISA Mwandamizi wa Usajili kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Jonathan Magoti akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya katika maonyesho ya wakulima Nane Nane |
NA JOYCE KASIKI,DODOMA
AFISA Mwandamizi wa
Usajili kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Jonathan Magoti amewaasa
wananchi kujenga utaratibu wa kupata vyeti vya kuzaliwa badala ya kusubiri
mpaka wawe na shida ndipo waanze kutafuta vyeti hivyo.
Akizungumza na
waandishi wa habari katika Banda la Wakala huo Magoti amesema,cheti cha
kuzaliwa ni muhimu kwani kinahitajika katika maeneo mengi ikiwemo katika
upatikanaji wa kadi ya NIDA pamoja na huduma nyingine.
“Cheti cha kuzaliwa ni
muhimu sana kwa sababu kinahitajika katika mifumo mbalimbali ya Serikali ,kwa
mfano mtu anapohitaji kitambulisho cha NIDA, mtoto anapohitaji kwenda shule
lazima atambulishwe kwa cheti cha kuzaliwa ,hata mtu anapohitaji kadi ya Bima
ya Afya lazima awe na cheti cha kuzaliwa ili kimtambulishe ,hata uhamiaji
wanahitaji kupata utambulisho kutoka Rita”amesema Magoti
Aidha amesema,kwa
watoto wachanga cheti hicho kinatolewa ndan ya siku 90 bure na kuwahimiza
wazazi na walezi kufuatilia vyeti hivyo vya watoto ili kuondoa usumbufu pindi
wanapohitaji huduma mbalimbali zikiwemo huduma za afya na kielimu.
“Wananchi wajenge desturi ya kuhakikisha mtoto
anapata cheti mara tu anapozaliwa ambapo ndani ya siku 90 mara baada ya
kuzaliwa cheti hicho kinatolewa bure .”amesisitiza
Aidha amesema wakala
huo upo katika maonyesho hayo kwa madhumuni ya kutoa elimu kuhusiana na huduma
zitolewazo na RITA lakini pia wanafanya usajili wa vyeti upande wa vizazi na
vifo pia wanafanya usajili hata kwenye masuala ya ndoa kwa wachungaji na
Masheikh wanaotaka kusajiliwa kwa ajili ya huduma mbalimbali za ndoa pamoja na
masuala ya kisheria kuhusiana na udhamini,na kuandika na kuandaa wosia.
“Kwa hiyo unapokuja
uwanjani hapa unapata elimu pamoja na kusajiliwa pia unapewa na cheti cha
kuzaliwa ndani ya siku moja au mbili ili mradi tu awe ana vielelezo
vinavyotakiwa.”
Aidha ameeleze changamoto
wanayokutana nayo katika maonyesho pindi wananchi wanapofuata vyeti vya
kuzaliwa wanakwenda bila vielelezo vinavyomtambulisha mtoto au muhusika anayehitaji
cheti hicho.
“Changamoto tuliyonayo
ni elimu ambayo inaonekana ilikuwa bado haijawafikia wananchi kwa sababu
wanaposajili vizazi na vifo tunahitaji vielelezo vinavyotambulisha umri wa
mteja na baadhi ya taarifa, kwa hiyo wateja wanakuja bila vielelezo vya kutosha.”
Hata hivyo amesema
mwitiko wa wananchi kufika katika banda hilo na kupata huduma mbalimbali ni mkubwa
kwani wengi wamekuwa wakifika kwa ajili ya kupata huduma hasa ya vyeti vya
kuzaliwa.
Edwin Simbili ni miongoni mwa wananchi waliotembelea katika banda la RITA katika maonyesho hayo ambapo ameishukuru Serikali kwa kupeleka huduma hiyo katika viwanja vya Nane Nane ambapo wananchi wamepewa vyeti lakini pia wanatoa elimu mbalimbali kuhusiana na shughuli zao huku akiiomba serikali iendelee kuelimisha wananchi kuhusu huduma zitolewazo na RITA na umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa
No comments:
Post a Comment