NA JOYCE KASIKI,MBEYA
MENEJA Mawasiliano Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA)
Subira Kaswaga, ametoa wito kwa taasisi
za umma kujiunga na mfumo wa ubadilishanaji taarifa serikalini (GovESB) ili
taasisi hizo ziweze kuwasiliana na kubadilishana taarifa kidijitali
kupitia mfumo huo.
Kaswaga ametoa wito huo leo
wakati alipofanya mkutaa waandishi wa Habari mkoani Mbeya, kuhusu huduma
mbalimbali zinazotolewa na e-GA kwenye maonyesho ya wiki ya wakulima yanayoendelea
jijini humo.
“Mfumo wa GovESB ni shirikishi na unaziwezesha
taasisi za umma kuunganisha mifumo ya TEHAMA kupitia mfumo huo ili kuweza kuzungumza na
kubadilishana taarifa kidijitali. “amesema Kaswaga
Kwa mujibu wa Kaswaga ,faida za
mfumo huo ni pamoja na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi za
umma, kuokoa muda, gharama za uendeshaji wa taasisi pamoja na kurahisisha
utoaji wa huduma kwa wananchi kwa wakati.
“Mfumo wa GovESB ni jitihada za
Mamlaka za kuhakikisha mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma inazungumza na
kubadilishana taarifa ili kupunguza urudufu wa mifumo serikalini, kwa sasa
taasisi mbalimnbali za umma zimeunganisha mifumo yake na GovESB lakini zipo
taasisi ambazo bado hazijaunganisha, hivyo nitoe wito kwa taasisi hizo kujiunga
na mfumo huu wa GovESB”, alisema Kaswaga.
“ e-GA imedhamiria kuhakikisha
utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao katika taasisi za umma unaimarika
ili kuhakikisha taasisi za umma zinatumia TEHAMA kwenye utendaji kazi wake na
kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.”amesisitiza
Aidha, aliongeza kuwa e-GA
hushirikiana na taasisi nyingine za umma katika kutengeneza mifumo ya TEHAMA
inayotumika katika taasisi hizo ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika
taasisi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Mamlaka imedhamiria
kuhakikisha kuwa, mwananchi anapata huduma zote za serikali kidijitali mahali
alipo, ili kufikia malengo hayo, tunashirikiana na taasisi mbalimbali za umma
kutengeneza mifumo ya kisekta itakayosaidia utendaji kazi katika taasisi hizo
na kuwasaidia wananchi kupata huduma kidijitali”, alisisitiza.
Kwa upande wake Afisa TEHAMA wa
e-GA Caesar Mwambani amesema kuwa,
Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kushirikiana Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imetengeneza mfumo wa e-Mrejesho
unaowawezesha wananchi kuwasiliana na serikali kidijidati.
Amesema kuwa, mfumo huo
unawawezesha wananchi kuwasilisha maoni, changamoto, pongezi au malalamiko
kwenda katika taasisi yoyote ya umma na kisha kufuatilia utekelezaji wake
kwa njia ya kidijitali.
“Mfumo huu unamrahisishia
mwananchi kuwasiliana na serikali kidijitali na hivyo kumpunguzia gharama za
kusafiri kwenda katika taasisi husika ili kuwasilisha kero yake na badala yake
anaweza kuwasiliana na taasisi hiyo kupitia mfumo wa e-Mrejesho popote alipo”,
amesema
Ameongeza kuwa, mfumo wa
e-Mrejesho unapatikana kupitia tovuti ya www.emrejesho.go.tz, simu janja kwa
kupakua aplikesheni yake au kwa namba ya msimbo kwa kupiga *152*00# na kisha
atachagua namba 9, kisha namba 2 na kuwasilisha hoja yake kwenye taasisi
husika.
Mamlaka ya Serikali Mtandao
imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya 2019 ikiwa na
jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezajia wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango
na Miongozo ya Serikali Mtandao katika taasisi za umma.
No comments:
Post a Comment