NA JOYCE KASIKI,DODOMA
MBUNGE wa Makete Festo Sanga(CCM) ameitaka Serikali lini itakamilisha ujenzi wa mradi wa Matamba Kinyika ambao umefgharimu fedha nyingi lakini umeshindwa kutekelezeka kwa takribani miaka saba sasa.
Mbunge huyo ameoa kauli hiyo Bungeni jijini hapa wakati akiuliza swali la nyongeza ambapo alisema licha ya mradi huo kutokamilika kwa muda mrefu lakini tayari umeshaigharimu Serikali kiasi cha shilingi bilioni 2.8 kuujenga.
“Je ni lini serikali itakabidhi mradi huo kwa wananchi wa kijiji cha Nungu ,kijiji cha Ng’onde ,kijiji cha Mbela na kijiji cha Itani ili waweze kupata huduma ya maji Kwa sababu imebaki hatua ya usambazaji?”alihoji Mbunge huyo
Vile vile alitaka kujua ni lini Serikali itatoa kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kati ya shilingi bilioni tatu ili kukamilisha mradai huo baada ya kutoa shilingi milioni 500 pekee yake mpaka hivi sasa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kwa wananchi wa kata ya Iwawa .
Akijibu maswali hayo Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi alisema,Serikali inaendelea kutoa pesa na kutekeleza miradi ya maji ili wananchi wapate maji safi na salama.
Kuhusu mradi ambao umeshatolewa shilingi milioni 500 na Serikali,Mhandisi Mahundi alisema,utekelezaji wake unaendelea vizuri .
“Huu ni ule mradi uliotumia fedha za mapambano dhidi ya uviko 19 na fedha iliyobaki tutaendelea kutoa kuanzia mwezi huu wa sita na tutaendelea kuongeza fedha ili kuukamisha.”
Kuhusu mradi wa Matamba Kinyika ,Mhandisi Mahundi alikiri kwamba ni kweli mradi huo umechukua muda mrefu huku akisema huo ni miongoni mwa ile miradi ambayo iikuwa ni chechefu.
Hata hivyo alisema Serikali inaendelea kuikwamua na mradi umeshafikiwa kwa zaidi ya asilimia 80 katika utekelezaji wake na kwamba utamaliziwa muda siyo mrefu.
Awali katika swali la msingi Sanga alitaka kujua Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa mradi wa maji Kata ya Iwawa Makete Mjini.
Akijibu swali hilo Mhandisi Mahundi alisema,katika mwaka wa fedha 2021/22 Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji wa kuhudumia Kata ya Iwawa kwa kutumia chanzo cha mto Isapulano. “Mradi huu unahusisha ujenzi wa chanzo, ulazaji wa bomba kuu umbali wa Kilometa 12.5, ulazaji wa mabomba ya usambazaji umbali wa Kilometa 39.0 na ujenzi wa matanki matatu yenye ujazo wa lita 450,000. “alisema Mhandisi Mahundi
Aidha alisema,utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2022/2023.
No comments:
Post a Comment