Mbunge wa Makete Festo Sanga Akizungumza Bungeni jijini Dodoma wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa Fedha wa 2022/23
JOYCE KASIKI,DODOMA
MBUNGE wa Makete Festo Sanga (CCM) ameiomba Serikali kupeleka Bungeni muswada wa sheria ya kuilinda elimu ya hapa nchini.
Mbunge huyo ameyasema hayo leo Bungeni jijini hapa wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia iliyoliomba Bunge kuiidhinishia kiasi cha sh.Trilioni 1.493 ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa mwaka 2022/23.
Amesema,kutokana na kutokuwepo sheria ya kuilinda elimu hapa nchini ndio maana kumekuwa na tabia ya kila Waziri anayeteuliwa anakuja na utaratibu wake hali iliyochangia kuzorotesha elimu hapa nchini.
“Mfumo wa elimu umekuwa ukichezewa sana,
katika mabadiliko tuhakikishe jinsi gani elimu haifuati mawazo ya mtu binafsi”alisema na kuongeza kuwa
“Tunaomba mlete sheria hapa bungeni ya kuilinda elimu yetu ili isichezewe,kusiwe na mtu mmoja anaamua kubadilisha elimu anavyotaka yeye,inatakiwa kila mabadiliko tunayoyafanya lazima yalete tija katika elimu yetu.”amesisitiuza Sanga
Aidha Mbunge huyo amesema,ubora wa elimu hapa nchini pia unapungua kutokana na baadhi ya vyuo kutoka kwenye misingi ya kuanzishwa kwake.
“Kwa mfano chuo kama SUA ,kilianzishwa kwa ajili ya masuala ya kilimo,ardhi ,hii siyo sawa kilianzishwa kwa ajili ya masuala ya ardhi na vyuo vingine vingi ambavyo sasa vimetoka katika mlengo wa kuanzishwa kwake na badala yake vyuo hivyo vimekuwa vikifundisha masomo mengine mengi kwa ajili ya kutafuta fedha,hii siyo sawa .Amesema Sanga
Ametumia nafasi hiyo kumuomba Waziri apitie vyuo vyote ili kuhakikisha kila chuo kinafundisha masomo yale yaliyokusudiwa katika kuzalisha wataalam husika.
“Tunakutegemea sana Waziri maana tunajua unaenda kufanya mageuzi makubwa kwenye wizara ya Elimu.”amesema
Mbunge huyo pia ametoa ushauri kwa Wizara hiyo kuangalia mrundikano mkubwa wa vitabu uliopo nchini hali ambayo amesema inawachanganya wanafunzi.
“Kwenye mfumo wa elimu kuna mrundikano wa vitabu,havina utaratibu kiasi ambacho inawachanganya watoto,tumeruhusu mrundikano wa vitabu ambavyo havina ubora wala ithibati ya elimu.”ameongeza
Vile vile mbunge huyo ameshauri kuwe na muunganiko baina ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,Utumishi na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) ili wanafunzi wafundishwe kozi ambazo zipo kwenye soko la ajira.
No comments:
Post a Comment