JOYCE KASIKI,DODOMA
BAADHI ya wabunge wameonyesha kuchukizwa na vitendo vya ukatili vinavyoendelea hapa nchini hususan matukio ya ulawiti na ubakaji wa watoto ambapo wametoa maoni tofauti huku baadhi yao wakitaka wanaume wanaofanya vitendo hivyo wahasiwe ili kuwanusuru watoto dhidi ya vitendo vya ubakaji na ulawiti.
Wakichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum ambayo imeomba shilingi bilioni 43.403 kwa mwaka wa Fedha wa 2022/23 bungeni jijini Dodoma,wabunge hao wamesema matukio hayo ni miongoni mwa mambo ambayo yanaathiri malezi na makuzi ya watoto wadogo na hivyo kuathiri makuzi katika maisha yao.
Mbunge wa Viti Maalum Subira Mgalu amesema, takwimu za matukio ya ukatili zinatisha huku akisema kwa kipindi cha Januari 2019 mpaka sasa matukio hayo jumla yake ni takribani 29,000 lakini miongoni mwao kubakwa ni takribani 19,000 sawa na asilimia 70 huku yaliyofikishwa mahakamani yakiwa ni asilimia 75 na yaliyohukumiwa ni kama asilimia 67.
“Tatizo hili ni kubwa na katika moja ya changamoto ni matukio ya kulawiti ambapo watoto wa kiume zaidi ya 3000 kati ya 3,260 sawa na asilimia 64 wamelawitiwa,hali hii inatisha mpaka tunatamani kama adhabu iongezwe ,au tuseme wanaume wahasiwe ,hii yote ni kuona namna gani tuanweza kuondoa ukatili huu wa ulawiti na ubakaji wa watoto,
“Serikali inafanya maendeleo kwa ajili
ya kizazi cha sasa na kijacho lakini maendeleo haya yatakuwa hayana maana kama
tunaandaa kizazi cha watoto wanaobakwa ,watoto wa kiume wanaolawitiwa,
“Kwa hiyo naiomba Serikali kupitia
Wizara mtambuka zinazohusika katika eneo hilo ,kuangalia sheria kwani pamoja na
kwamba zipo lakini haipiti wiki yanasikika matukio ya ubakaji,ulawiti wa
watoto,
“Na kinachosikitisha zaidi matukio
yameambukiza ndani ya familia,unakuta baba anabaka watoto wake ,baba analawiti
watoto wake,tumnwombe mwenyezi Mungu atuongoze tuondokane na haya matukio.”
Mbunge huyo aliwaasa watanzania kutahimini
kwa matukio hayo ambayo yamekuwa yakijiotokeza kila siku huku akiiomba mahakama mahakama
iendelee kutenda haki katika kuhakikisha walawiti na wabakaji wa watoto
wanachukuliwa hatua stahiki.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum
Fatma Toufiq (CCM) amepongeza mikakati
mbalimbali ya serikali iliyopo ambayo
inalenga kuhakikisha ukatili unatokomezwa kupitia Mpango wa Mpango Kazi wa
Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ambao una dhamira ya kuhakikisha ukatili dhidi
ya wanawake na watoto unatokomezwa kwa asilimia 50 ifikapo Juni 2022.
Hata hivyo amesema,kumekuwa na ukatili
mwingi hapa nchini ukiwemo wa kingono ,vipigo ,kuuawa,kuchomwa moto
watoto,usafirishaji watoto,ubakaji wa watoto,ulawiti wa watoto,huku akisema,kwa
matukio hayo inaonyesha ukatili umekithiri kupita kiasi .
“Na pia kwa kuwa vyombo vya habari
vimekuwa vikitoa taarifa mbalimbali vimekuwa vikiripoti kuwa wahusika wa
matukio ya ukatili hususan wa ubakaji wa watoto ni pamoja na ndugu wa karibu
ambao ni baba ,ndugu wa karibu wanabaka na kulawiti watoto vitendo ambavyo vina
athari kubwa katika Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya mtoto,
“Nitoe mfano wa matukio ambayo
yameripotiwa hivi karibuni Mkoa wa Kilimanjaro kuna mume amemuua mkewe mbele ya
mtoto wake wa miaka miwili,sasa huyu mtoto akikua akili yake itakuwaje hilo ni
tatizo,kuna mtoto alinyongwa Machi mwaka huu ,kuna tukio la baba kumuua mtoto
wake kwa kushindwa kusoma ,kuna mama mkubwa naye amemuua mtoto wa mdogo
wake,kwa hiyo mambo haya yanatisha ,.”amesema Toufiq
Mbunge huyo pia ameiasa Serikali kutupia macho shuleni huku akisema kuna matukio ya ubakaji na ualwiti yamekuwa yakifanyika huko kwa watoto walio katika madarasa ya juu kuwafanyia vitendo hivyo watoto wenzao wa madarasa ya chini .
Baadhi ya shule zetu nazo siyo
salama,baadhi ya watoto wa madarasa ya juu wamekuwa wakiwalawiti watoto wa
madarasa ya chini na hili jambo nalo inapaswa tuliangalie kwa kuona jinsi
tunavyoielimisha jamii,maana inawezekana baadhi ya tabia za watoto wanazirithi
kutoka katika nyumba na familia zao.”
Kufuatia changamoto hizo za ukatili
Toufiq ameishauri Serikali kuiangalia upya sheria ya kanuni ya adhabu kuhusu
mimba zinazotokana na kubakwa na ndugu wa damu
ili iwaondolee sonona walengwa (wasichana) na kama itafaa ujauzito
utolewe na wataalam.
Ameiomba Serikali kuchukua hatua kwa wazazi
wa kiume wanaotelekeza watoto wao kwa sababu baadhi ya akina mama wanashindwa
kuwalea watoto na hivyo kuathiri Malezi na makuzi yao na hatimaye kushindwa
kukua hadi kufikia utimilifu wao.
Awali Waziri wa Maendeleo ya Jamii
,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima alisema, pamoja na hatua
za kila siku za Serikali na wadau mbalimbali kupambana na ukatili
kupitia MTAKUWWA, Wizara inaratibu utekelezaji wa kampeni kubwa ya kupambana na
ukatili sambamba na kuimarisha mifumo ya kubaini viashiria vya ukatili na
kuchukua hatua za kuzuia.
Aidha alisema,kwa kuwa utekelezaji wa MTAKUWWA unafikia ukomo mwezi Juni mwaka huu, Wizara imeanza mchakato wa kufanya tathmini ya Mpango huo kwa lengo la kubaini mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji kwa kipindi cha miaka mitano, changamoto na upungufu wa kimuundo na kiutendaji ulioathiri kufikiwa kwa malengo ya Mpango.
“Tathimini inatarajiwa kubainisha masuala
ya kuigwa na kutoa mapendekezo ya namna
bora zaidi ya kukabiliana na changamoto
na upungufu uliobainika,matokeo au mapendekezo yatakayobainishwa katika taarifa ya Tathmini
ya Mpango yatawezesha kuanza kwa maandalizi ya MTAKUWWA awamu ya pili itakayotoa
mikakati mahsusi ya kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa miaka mitano ijayo.”amesema
Dkt.Gwajima
Kwa mujibu wa Dkt.Gwajima ,tathmini na
Maandalizi ya MTAKUWWA II yanatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Septemba, 2022.
Akizungumzia kuhusu uratibu na
utekelezaji wa MTAKUWWA Waziri huyo alisema,Wizara imeendelea kuratibu
utekelezaji wa Mpango huo kupitia maeneo
nane ya utekelezaji.
Amesema mpango huo ambao utekelezaji wake ulianza Julai, 2017 na kutarajiwa kufikia ukomo Juni mwaka huu, baadhi ya mafanikio yake ni Matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa
katika Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi yamepungua kwa asilimia kutoka
matukio 42,414 mwaka 2020 hadi matukio 29,373 mwaka 2021.
Aidha, matukio ya ukatili wa kijinsia
kwa watoto yaliyoripotiwa
kwenye Dawati hilo yamepungua kwa asilimia 28 kutoka matukio 15,870 mwaka 2020
hadi matukio 11,499 mwaka 2021.
Dkt.Gwajima amesema,mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa vituo vya mkono kwa
mkono ambavyo hadi Aprili 2022, jumla ya Vituo 21
vya Mkono kwa Mkono (One Stop Centers) vimeanzishwa katika Hospitali mbalimbali
za Serikali kwenye Mikoa 12 ikilinganishwa
na Vituo 14 vilivyoanzishwa hadi kufikia mwaka 2020/21.
Amesema,lengo la vituo hivyo ni kuwezesha utoaji wa huduma hizo katika eneo
moja ili kuepusha usumbufu, ucheleweshaji wa huduma, kuharibu au kupoteza
ushahidi.
Waziri huyo alisema,Serikali kwa kushirikiana
na Wadau itaendelea kuratibu uanzishwaji wa Vituo vya Mkono kwa Mkono katika
Mikoa ambayo haijaanzisha Vituo hivyo ikiwemo Mikoa ya Dodoma,
Singida, Tanga, Geita, Katavi, Rukwa, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Mara, Kagera, Njombe,
Songwe na Manyara.
“Vituo hivi vinarahisisha huduma kwa
kumpa fursa manusura kufika katika kituo na kupata huduma za unasihi, utoaji
taarifa kwa Afisa
wa Polisi na kupata matibabu lakini pia vinarahisisha
upatikanaji wa haraka wa ushahidi unaotokana na vipimo vya kitabibu
unaowasilishwa katika Mahakama. “
Akizungumzia hali hiyo ya matukio mengi ya ukatili ,Danson Kaijage mkazi wa Ilazo jijini Dodoma amesema,matukio hayo ya ulawiti ,ubakaji hususan wa watoto yamekuwa yakitokea kwa wingi kutokana na ukosefu wa maadili na watu kutokuwa na hofu ya Mungu hali inayofanya jamii kukimbilia kwenye ushirikina ili kujipatia mali kirahisi badala ya kufanya kazi.
"Kinachotakiwa serikali iendelee kutoa elimu zaidi mashuleni kuwajengea uwezo wa kujieleza watoto kuanzia darasa la awali kwani matukio haya huwakumba hata watoto walio chini ya miaka mitano ."amesema Kaijage
No comments:
Post a Comment