



Na Joyce Kasiki,DAR ES SALAAM
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umewahimiza Watanzania kote nchini kuondokana na mtazamo potofu kwamba matumizi ya nishati safi ya kupikia ni gharama kubwa ukilinganisha na kuni au mkaa, akisisitiza kuwa teknolojia ya kisasa imepunguza sana gharama hizo.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu, wakati wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam, katika banda la REA.
“Kumekuwepo na dhana kwamba kutumia nishati safi ya kupikia kama vile umeme ni gharama kubwa ikilinganishwa na kutumia kuni au mkaa. Hii si kweli. Teknolojia imebadilika sana sasa; kuna majiko ya kisasa yanayotumia umeme kwa kiwango kidogo sana,” alisema Mhandisi Olotu.
Aliwataka wananchi kutembelea banda la REA ili kujionea kwa macho jinsi teknolojia hizo zinavyofanya kazi na kuona jinsi upishi kwa kutumia nishati safi unavyowezekana bila kupoteza ladha ya chakula, huku muda wa kupika ukiwa mfupi zaidi.
Akizungumzia juhudi za REA katika kuhamasisha na kuwawezesha waendelezaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia, Mhandisi Olotu alieleza kuwa lengo ni kuwawezesha Watanzania kubadili mtindo wa maisha na kulinda afya zao pamoja na mazingira.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Afya, watu takribani 33,000 hufariki kila mwaka kutokana na athari za matumizi ya nishati chafu ya kupikia. Mhandisi Olotu alisisitiza kuwa REA ni miongoni mwa wadau wakuu wanaojitahidi kupunguza idadi hiyo kwa kutoa elimu na kuwapatia wananchi mbinu mbadala salama.
“Dhamira yetu ni kuachana kabisa na matumizi ya kuni na mkaa, lakini tunatambua kuwa mabadiliko haya hayawezi kufanyika kwa mara moja. Ndiyo maana tumekuwa tukisambaza majiko ya kisasa yanayotumia kiasi kidogo cha mkaa au kuni kama njia ya mpito,” alieleza.
Katika hatua za awali, REA imeanza kusambaza majiko ya gesi yenye mitungi ya kilo 6. Hadi sasa, jumla ya mitungi 3,255 pamoja na vichomeo vyake vimegawiwa katika kila wilaya Tanzania Bara kwa ruzuku ya asilimia 50, huku zoezi hilo likiendelea.
“Tunalenga kumwezesha kila Mtanzania kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati hatarishi kwenda kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kwa wale wanaohitaji muda kubadilika, tumeanzisha suluhisho la mpito kwa kutumia teknolojia ya majiko yanayotumia mkaa kidogo,” aliongeza.
Aidha, alieleza kuwa REA inatekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuzitaka taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ya kupikia.
“Tumeanza utekelezaji katika taasisi mbalimbali, zikiwemo Jeshi la Magereza. Mpaka sasa, maeneo 211 yameshafikiwa yakiwemo magereza 129, kambi 47, ofisi za mikoa 26, pamoja na nyumba za watumishi, vyuo, shule na hospitali,” alisema.
Nishati safi zinazotumika katika taasisi hizo ni pamoja na bayogesi, gesi ya mitungi (LPG), gesi asilia, mkaa kutoka makaa ya mawe, pamoja na mashine za kutengeneza mkaa mbadala. Vilevile, REA imewajengea uwezo Maafisa wa Magereza 280 kuhusu matumizi bora ya nishati safi.
Kwa ujumla, REA inaendelea kutoa elimu na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia ya kisasa ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanahama kutoka matumizi ya nishati chafu kuelekea kwenye mfumo wa upishi salama, rafiki kwa afya na mazingira.
.
No comments:
Post a Comment