
Na Joyce Kasiki,DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ushindani wa Kibiashara (FCC) imetumia fursa ya maonesho ya biashara kufikisha elimu kwa wadau wa sekta ya biashara huku ikizindua 'clinic' maalum ya kutoa ushauri wa faragha kwa wafanyabiashara kuhusu masuala ya ushindani na ulinzi wa walaji.
Akizungumza katika maonesho hayo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Hadija Ngasongwa, alisema kuwa jukwaa hilo limewawezesha kufikia zaidi ya washiriki 3,500 kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha ushindani wenye tija na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
“FCC imeanzisha clinic ya biashara ili kutoa nafasi kwa wafanyabiashara hasa wadogo na wa kati kupata maarifa sahihi kuhusu sheria za ushindani na haki za walaji, kwa faragha na usiri unaohitajika,” alisema Bi. Ngasongwa.
Aliongeza kuwa pamoja na kuelimisha umma, FCC inaendelea kufuatilia mwenendo wa soko na kudhibiti bidhaa bandia ambazo si tu zinahatarisha afya za walaji, bali pia zinaharibu ushindani halali katika biashara.
Ngasongwa alieleza kuwa Serikali kupitia FCC imejenga mazingira rafiki ya kufanyia biashara, hali ambayo inaendelea kuwavutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
“Sheria zetu ni rafiki kwa wawekezaji, na tunajivunia kwamba Serikali imeimarisha zaidi mazingira ya biashara, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji,” alisisitiza
Alifafanua kuwa FCC inaendelea kufanya tafiti za soko zenye lengo la kuhakikisha uwiano wa ushindani unazingatiwa, pamoja na kusaidia biashara ndogo kukua hadi kufikia viwango vya juu vya ushindani.
“Dhamira yetu ni kuhakikisha kuwa siyo tu wawekezaji wa nje wanafaidika na mazingira mazuri ya biashara, bali pia wajasiriamali wa ndani wanapata nafasi ya kukuza mitaji yao kupitia ushindani wa haki,” alieleza
Maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu kati ya wadau wa biashara na taasisi mbalimbali, huku FCC ikichukua hatua za makusudi kuwa karibu zaidi na wafanyabiashara kwa njia ya ushauri wa moja kwa moja na elimu ya kisheria.
No comments:
Post a Comment