
Na Mwandishi wetu, Dodoma
KATIBU wa Itikadi ,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla, ametoa ufafanuzi kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani, akisisitiza kuwa vikao muhimu vya maamuzi vitafanyika jijini Dodoma kuanzia Julai 26 hadi Julai 28, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 19,2025 Makao Makuu ya chama hicho jijini Dodoma, Makalla alieleza kuwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kitafanyika Julai 26 na kitatanguliwa na kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho siku hiyo hiyo, ambapo maamuzi ya awali kuhusu mchakato wa uteuzi yatawekwa wazi.
Makalla amesema maandalizi ya uchaguzi ndani ya CCM yanaendelea vizuri, huku kikao cha mwisho kuhusu uteuzi wa wagombea kikiwa kimepangwa kufanyika Julai 28, mwaka huu jijini Dodoma.
Amesema vikao hivi vya juu vitaamua majina ya wagombea watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi ujao katika ngazi za Ubunge na udiwani.
"Leo wengi walitarajia Kamati Kuu ingeketi kwa ajili ya uteuzi, lakini shughuli hiyo sasa imepangwa kufanyika Julai 28. Hili ni zoezi nyeti linalohitaji umakini mkubwa, na ndiyo maana tumeamua kujipa muda zaidi ili tuweze kufanya kazi hii kwa weledi," amefafanua Makalla.
Aidha, Makalla amewataka wagombea wote waliowasilisha nia zao kuwa watulivu na kuvuta subira wakati mchakato ukiendelea, akibainisha kuwa jumla ya watu zaidi ya 10,000 wameomba ubunge, huku zaidi ya watu 27,000 wakitia nia kugombea nafasi ya udiwani kupitia CCM.
"Napigiwa simu nyingi kuhusu lini uteuzi utafanyika. Sasa nawaambia, kazi ni kubwa, lakini tunaenda kwa hatua makini,hakuna mtu aliyekatwa bado, na kikao cha Julai 28 ndicho kitaamua rasmi nani anasonga mbele," amesisitiza.
Baada ya uteuzi huo, Makalla aliongeza kuwa chama kitapanga na kutangaza ratiba ya kura za maoni, hatua inayofuata katika mchakato wa kuwapata wagombea wa mwisho.
Amesisitiza kuwa chama hakina shaka na tarehe iliyopangwa na kimejipanga kutoa wagombea bora na wa kuaminika.
CPA Makalla amewahimiza wagombea wote kuwa watulivu hadi pale vikao vya mwisho vitakapotoa maamuzi rasmi kuhusu wagombea watakaoteuliwa kwenda kwenye kura za maoni.







No comments:
Post a Comment