


Picha zote zinaonesha wajumne wa Bodi ya PSPTB wakiwa katika picha ya pamoja kwenye maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara kwenye banda la PSPTB
Na Mwandishi wetu
BODI ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imetangaza rasmi kuanza kwa usajili wa mitihani yake ya kitaaluma ya 31, itakayofanyika kuanzia Agosti 25 hadi Agosti 29, 2025, katika kituo maalum kilichopo jijini Dodoma.
Akizungumza Leo Julai 4,2025 na waandishi wa habari katika Maonyesho ya Kimataifa ya 49 ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam , Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi, amewahimiza waombaji wote wenye sifa kujisajili kupitia mfumo wa mtandaoni unaopatikana kwa anuani https://registration.psptb.go.tz.
"Tunapenda kuwafahamisha wadau wetu kuwa usajili wa mitihani ya 31 umefunguliwa rasmi,tunawasihi wale wote wanaokusudia kufanya mitihani hii wajisajili mapema kabla ya tarehe ya mwisho ya kupokea maombi ambayo ni Agosti 15, 2025," amesema Mbanyi.
Kwa mujibu wa Mbanyi , kwa sasa mitihani hiyo itafanyika katika kituo kimoja tu Dodoma ili kuimarisha uratibu na kuhakikisha usimamizi bora wa mitihani hiyo muhimu kwa taaluma ya ununuzi na ugavi nchini.
Aidha Mkurugenzi huyo, amewaasa wazazi na walezi kushiriki kikamilifu kwa kuwasomesha na kuwafadhili watoto wao walioko kwenye nyanja ya ununuzi na ugavi, kwa kuhakikisha wanalipiwa ada za usajili wa mitihani hiyo.
"Natoa rai kwa wazazi na walezi kuchangia katika maendeleo ya taaluma hii kwa kuwalipia ada watoto wao,hatua hiyo ni uwekezaji muhimu katika kukuza rasilimali watu yenye weledi na uadilifu," aliongeza.
Aidha, Mkurugenzi huyo amewataka wadau wote wa PSPTB nchini kote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo kwa manufaa ya Taifa, akisema kuwa taaluma ya ununuzi na ugavi ni mhimili muhimu katika usimamizi wa rasilimali za umma na sekta binafsi.
Kwa mujibu wa PSPTB, mitihani hiyo ya kitaaluma ni sehemu ya mfumo wa kutoa ithibati kwa wataalamu wa ununuzi na ugavi, ambao wana mchango mkubwa katika kudhibiti matumizi ya fedha na kuhakikisha thamani halisi ya manunuzi kwa taasisi mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment