
Na Joyce Kasiki,DAR ES SALAAM
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) ubunifu wa tiba mpya kwenye maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya 49 Sabasaba , unaotegemea rasilimali za asili za mimea ya Kitanzania.
Mwalimu Dismas Tullo ambaye ni mmoja wa wabunifu hao kutoka UDOM, amefichua kuwa chuo hicho kimefanikiwa kubuni dawa tatu mpya zinazoweza kuwa suluhisho kwa maradhi sugu kama malaria, vidonda vya tumbo na kisukari,changamoto zinazotikisa maisha ya maelfu ya Watanzania kila siku.
Akizungumza Juni 30 ,2025 kwenye maonyesho hayo katika Banda la chuo hicho Tullo amesema ,"Tumetumia rasilimali zetu za mimea na mizizi ya asili kutengeneza dawa ambazo tayari zimeanza kuonyesha matokeo chanya kwa wagonjwa waliopatiwa dawa hizo ,” alisema Tullo
Dawa Tatu Zinazolenga Suluhisho Endelevu
Dawa ya kwanza ni Gymerine, ambayo inalenga kudhibiti ugonjwa wa kisukari. Tullo amesema dawa hiyo tayari imefanyiwa majaribio ya awali katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na baadhi ya wagonjwa waliotumia wameripoti kuimarika kwa afya zao.
Kwa upande wa vidonda vya tumbo, UDOM imebuni dawa iitwayo Ulcerexia, ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua za majaribio, lakini wagonjwa waliotumika kama sampuli wameripoti nafuu kubwa na dalili za kupona.
Lakini pengine uvumbuzi wa kusisimua zaidi ni Malaherb dawa mbadala ya malaria ambayo Tullo anasema ni rahisi zaidi kwa mgonjwa kuitumia tofauti na dawa mseto zilizopo sasa.
“Kwa sasa, dawa mseto ndiyo inatumika kutibu malaria, lakini changamoto kubwa ni kwamba wagonjwa wengi hushindwa kumaliza dozi kutokana na wingi wa vidonge. Hali hiyo husababisha malaria kujirudia na kusababisha matatizo mengine kama ya figo. Malaherb ni dozi fupi, rahisi kutumia, na haina madhara kwa sababu haina kemikali,” alieleza.
Mbali na Dawa, UDOM Yaleta Lishe Tiba
Mbali na dawa hizo, Tullo amesema UDOM pia imebuni lishe maalum kwa ajili ya wagonjwa wa kisukari na ini, watoto wenye utapiamlo, pamoja na watu wanaoishi na VVU. Lishe hiyo imeundwa kwa kutumia vyakula asilia visivyoongezwa viuatilifu hatari, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutibu kwa njia salama zaidi.
Tiba Asili Zinavyoweka Tanzania kwenye Ramani ya Kisayansi
Bunifu hizi kutoka UDOM si tu zinathibitisha uwezo wa wasomi wa ndani ya nchi kutoa suluhisho kwa matatizo ya kiafya, bali pia zinaashiria mwelekeo mpya wa Tanzania katika kutegemea tiba asilia kama mbadala wa dawa za viwandani.
Katika dunia inayoshuhudia ongezeko la usugu wa dawa na madhara ya viuatilifu, hatua kama hizi zinaweza kuwa mwanzo wa mageuzi makubwa katika sekta ya afya nchini.
Wakati Maonyesho ya Sabasaba yakiendelea, banda la UDOM limekuwa kielelezo cha kile kinachowezekana tukitumia maarifa, maliasili na dhamira ya dhati kubadilisha maisha ya Watanzania.
No comments:
Post a Comment