

Na Mwandishi wetu
Meneja wa Banda la Shirika la Mawasiliano Nchini (TTCL) Janeth Maeda, ametoa wito kwa Watanzania na washiriki wote wa maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 49 yanayoendelea jijini Dar es Salaam , kutembelea banda la TTCL ili kujionea huduma za kibunifu zinazojibu mahitaji halisi ya sasa ya taasisi, mashirika, sekta binafsi na wananchi wa kawaida.
Akizungumza katika banda hilo katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Juni 30,2025 ,Mawda amesema
“TTCL ni suluhisho la sasa na la baadaye katika huduma za TEHAMA,na hii ndiyo sababu Serikali imeendelea kutuamini kusimamia miundombinu ya kitaifa yenye umuhimu mkubwa kwa usalama wa Taifa na maendeleo ya uchumi,” alisema Maeda.
Amesema TTCL inashiriki maonesho haya ili kuuhabarisha umma kuhusu namna shirika hilo linavyotekeleza wajibu wake kwa wananchi, likiwa limeaminiwa na Serikali kusimamia miundombinu ya kimkakati ya Taifa ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC).
Maeda amebainisha kuwa kupitia huduma hizo, TTCL inatoa mchango mkubwa katika kuboresha utendaji wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi. huku akizitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Wizara zote, mashirika ya kiserikali, taasisi za kifedha, sekta ya afya, elimu, madini, usafirishaji, utalii na mashirika yasiyo ya kiserikali.
“Kupitia teknolojia yetu ya fiber optic, tumeweza kuwahudumia mashirika haya kwa kasi ya kuaminika, jambo ambalo linaongeza tija na usalama katika utendaji wao wa kila siku,” ameongeza Maeda.
Amefafanua kuwa matumizi ya huduma za TTCL yamechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza ufanisi, na kuimarisha usalama wa taarifa katika taasisi nyingi nchini, huku akisisitiza kuwa huduma hizo zinapatikana ndani ya nchi na kwa kuzingatia viwango vya juu vya usalama wa kimtandao.
Maeda Maeda ametumia nafasi hiyo kuwaalika wananchi, wadau wa biashara, taasisi, mashirika, kampuni na wageni kutoka mataifa mbalimbali kutembelea banda la TTCL kujionea huduma za kisasa za mawasiliano na teknolojia ya kidigitali.
“Tunawakaribisha kuona huduma bora za Data Center, kujifunza namna bora ya kuhifadhi taarifa kwa usalama, kutumia huduma za mawasiliano ya uhakika, na kujifunza njia za kupunguza gharama za uendeshaji kupitia TEHAMA,” amesema.
Ameongeza kuwa katika msimu huu wa Sabasaba, TTCL imetoa punguzo maalum kwa vifaa vya mawasiliano ikiwemo Router, USB Modem, na MIFI, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia miongoni mwa Watanzania na kuwawezesha kufurahia ulimwengu wa kidigitali kwa gharama nafuu.
Kwa ujumla, ushiriki wa TTCL katika maonesho ya Sabasaba mwaka huu inadhihirisha dhamira ya shirika hilo kuendelea kuwa mshirika wa kweli wa maendeleo ya TEHAMA nchini, na kuhakikisha Watanzania wote wananufaika na huduma bora, salama na za kuaminika za mawasiliano.
Xxxxxx
No comments:
Post a Comment