
Na Mwandishi wetu
MKURUGENZI wa Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza katika banda la TRA kwenye Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ili waweze kupata elimu muhimu kuhusu masuala mbalimbali ya kikodi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda hilo, Kayombo amesema kuwa ushiriki wa TRA kwenye maonyesho hayo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao wa kikodi.
“Tunawahamasisha wananchi wote kufika katika banda letu ili wapate uelewa wa kina kuhusu masuala ya kodi, ikiwa ni pamoja na mabadiliko mapya ya kisheria na taratibu zilizopo,” amesema Kayombo.
Amebainisha kuwa TRA inatoa elimu kuhusu masuala yote ya kikodi ikiwemo namna ya kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), fursa za vivutio vya kodi katika sekta mbalimbali kama kilimo, na huduma nyingine zinazotolewa na Chuo cha Kodi (ITA).
Aidha, alisisitiza kuwa wananchi wanaotembelea banda hilo wanaelimishwa pia kuhusu mbinu za kutambua bidhaa bandia, kwa usaidizi wa wataalam waliopo kwenye eneo hilo.
“Tunatoa pia elimu kuhusu namna ya kutoa taarifa dhidi ya watumishi wa TRA wanaojihusisha na vitendo visivyo vya kimaadili ili hatua za kinidhamu na kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao,” ameongeza Kayombo.
TRA imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwa karibu na wananchi na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa ulipaji sahihi wa kodi kwa maendeleo ya taifa.
Amesema banda lao lipo wazi kwa wadau wote wanaohitaji msaada au elimu ya kikodi wakati wote wa kipindi cha maonyesho hayo.
No comments:
Post a Comment