
Na Joyce Kasiki,DAR ES SALAAM
MWANAFUNZI aliyekuwa akisoma kozi ya Hoteli na Utalii katika Chuo cha VETA Njiro Fredrck Mlay , amefanikiwa kuibadili kabisa hali yake ya kiuchumi na kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wengine kwa kujiajiri mwenyewe baada ya kuhitimu masomo yake.
Fredrick alianza kozi hiyo mwaka 2023 na kuhitimu Mei 2025 akiwa na Cheti na Diploma, elimu ambayo imekuwa nguzo kubwa ya mafanikio yake ya sasa.
Kupitia kiwango cha cheti, alipata maarifa kuhusu jinsi ya kuongeza idadi ya watalii wanaovutiwa na mbuga za wanyama huku kiwango cha diploma kikimuwezesha kuelewa mbinu za ubunifu na uuzaji wa vinywaji mbalimbali katika hoteli ikiwa ni pamoja na vinywaji vikali na laini vinavyotengenezwa kwa matunda.
Akizungumza Julai 2,2025 katika Banda la VETA kwenye maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya 49 Fredrick amesema,"Elimu ya VETA imenipa ujuzi ambao umeniwezesha kujiamini, kujiendeleza na sasa kuajiri vijana wenzangu,”
Fredrick amesema kwa anatengeneza vinywaji kama juisi , cocktails na pombe kali , akitumia matunda na viambato halali. Vinywaji hivyo hutumika katika hafla mbalimbali kama harusi na matamasha.
Aidha amesema, alichagua kozi hiyo ili aweze kuitumia kama daraja la kujiajiri. "Katika kozi hii nimejifunza mengi ikiwemo namna ya kuhudumia wageni, masoko, usimamizi wa shughuli, pamoja na kutengeneza cocktails kwa kutumia matunda na alcohol,” anaeleza.
Mbali na kujiajiri amesema elimu hiyo imemsaidia pia kuwa sehemu ya suluhisho kwa vijana wasiokuwa na ajira ambapo kwenye shughuli zake, huwashirikisha vijana ambao wengi wao hawakuwa na ujuzi, lakini sasa wanajifunza, wanapata uzoefu na kipato.
“Katika kazi zangu, hasa kwenye matukio kama harusi na sherehe, huwa nachukua vijana kufanya kazi nami. Hii imenisaidia mimi kiuchumi na pia kuwapa wao fursa ya kipato na maarifa. Wengine wameendelea na kazi hadi sasa,” anasema kwa fahari.
Kijana huyo amesema,mpango wake wa baadaye ni kufungua mgahawa mkubwa wa kisasa, ambao utatoa ajira kwa vijana wengi zaidi wakiwemo wale ambao hawakubahatika kusoma VETA kutokana na changamoto mbalimbali.
Anahitimisha kwa kuwasihi vijana wa Kitanzania kujiunga na vyuo vya VETA ili wapate ujuzi wa kuwasaidia kujiendeleza kimaisha na kuchangia katika maendeleo ya taifa. “Ujuzi ndio msingi wa mafanikio ya kweli, na VETA ndio sehemu sahihi ya kuanzia,” amesema.
No comments:
Post a Comment