
Mkufunzi wa VETA Faulata Mtalemwa akiwa na watoto waliotembelea Banda la VETA kona ya watoto kwenye maonyesho ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba.
Na Joyce Kasiki,DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeandaa mpango kabambe wa kuanzisha programu maalum ya kuwafundisha watoto wadogo stadi za mikono, ikiwa ni hatua ya kimkakati katika kukuza vipaji na kuandaa kizazi cha Tanzania ya viwanda inayojitegemea.
Hayo yamesemwa Julai 4 ,2025 na Mkufunzi kutoka VETA Songea Faulata Mtalemwa katika Banda la VETA ,kona ya watoto ambapo amesema kitengo hicho kimeanzishwa Ili kutambulisha Mpango huo.
Amesema Mpango huo unaotarajiwa kuanza rasmi mwakani na kwamba utatekelezwa katika vyuo vyote vya VETA nchini, ambapo kila kituo kitapanga muda maalum katika kipindi cha likizo kwa ajili ya kuwafundisha watoto mbinu mbalimbali za ufundi stadi ambapo Wazazi watachangia gharama ndogo tu, hususan kwa ajili ya chakula na huduma za msingi wakati wa mafunzo hayo.
Kuibua vipaji mapema
Mtalemwa amesema wa lengo la programu hiyo ni kuanza kuwaandaa watoto kuifahamu thamani ya kazi za mikono wakiwa katika umri mdogo, hatua itakayosaidia kukuza vipaji na uwezo wa ubunifu kabla hata hawajafikia umri wa ujana.
“Tunatamani kuibua mafundi, wahandishi, wabunifu na wajasiriamali kuanzia utotoni,na katika umri mdogo, mtoto ana uwezo mkubwa wa kushika na kukumbuka jambo,tukiwapa maarifa mapema, tunawajengea msingi imara wa maisha yao ya baadaye,” amesema.
Maeneo ya Mafunzo
Mafunzo yatakayofundishwa kwa watoto yamegawanywa kulingana na mahitaji ya msingi na usalama wa mtoto lakini pia kulingana na umri wa mtoto husika , yakiwemo:
Ujenzi wa vitu vidogo kama nyumba za matofali ya matope au mfano wa upakaji rangi,umeme wa majumbani mfano, namna ya kutumia swichi kwa usalama, kutambua waya hatarishi, na mbinu rahisi za kuhifadhi vifaa vya umeme.
Vile vile amesema watafundishwa ushonaji mfano kufunga vifungo, kurudishia nguo zilizochanika, kukukunja nguo vizuri,utunzaji wa mavazi kwa ujumla pamoja na Stadi za maisha kama kupamba meza, kupanga vitu, kusuka nywele, usafi wa mazingira, na kazi ndogo ndogo za kusaidia nyumbani.
Kuibadilisha Mitazamo ya Jamii
Mtalemwa amesema mpango huo pia ni sehemu ya juhudi za VETA kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu elimu ya ufundi stadi, ambayo kwa muda mrefu imeonekana kuwa ni ya watu waliokosa nafasi nyingine.
“Jamii nyingi za magharibi zimepiga hatua kwa sababu waliwekeza katika stadi za mikono, Tanzania tuna uwezo, tuna vijana wengi wenye vipaji tunachohitaji ni kuviendeleza mapema,” amesisitiza
Kona ya watoto maonyesho ya Kitaifa
Kufuatia hali hiyo amesema,katika kuhamasisha jamii na kuonyesha mwelekeo mpya, katika maonyesho ya mwaka huu kwa mara ya kwanza VETA ambayo hii inalenga kuwaonesha Watanzania kuwa vipaji vya watoto vinaweza kulelewa mapema na kuzaa mafanikio makubwa.
"Watoto wanaopata nafasi ya kupiga katika Kona hii, walionyesha kazi mbalimbali, zikiwemo kazi za ufundi, uchoraji, kushona, na hata kubuni bidhaa rahisi kwa kutumia vifaa vya kawaida jambo lililowagusa na kuwatia moyo wazazi wengi waliotembelea banda hilo."amesema Mtalemwa
Aidha Mkufunzi huyo amesema hatua hiyo itasaidia kujenga Taifa imara kwa Msingi Imara
“Hili ni jibu kwa changamoto ya kizazi kinachokua bila maarifa ya msingi ya maisha maana wazazi tumekuwa tunahangaika kutafuta fedha, lakini tusisahau msingi wa kulea watoto. Kupitia VETA, tunatengeneza jamii yenye ujuzi, yenye kujiamini, na inayoweza kulibeba Taifa kwa maendeleo,”
No comments:
Post a Comment