
Na Joyce Kasiki,Dar es Salaam
WANAFUNZI wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wameibuka na ubunifu wa kipekee kwa kutengeneza mfumo wa kisasa wa kudhibiti matumizi ya umeme majumbani, unaotumia teknolojia ya mawasiliano bila waya.
Mfumo huo, uliopewa jina la Smart Home ulioneshwa kwa mara ya kwanza kwenye Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa maonyesho hayo, Sayuni Haule, mwalimu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), alisema kuwa mfumo huo umetengenezwa na wanafunzi wake kama sehemu ya mazoezi ya vitendo yanayolenga kutafsiri elimu ya darasani kwenda kwenye maisha halisi.
Alisema kuwa mfumo huo ni mfano wa awali (prototype) unaoonesha jinsi teknolojia rahisi inaweza kutatua changamoto za kila siku za matumizi ya nishati majumbani.
“Kwa kutumia mfumo huu, mtu anaweza kuwasha au kuzima taa, feni na vifaa vingine vya umeme akiwa mbali na nyumbani kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano isiyotumia waya,” alisema Mwalimu Haule,
“Mfano, mtu anaweza kuwa kazini au safarini na akagundua kuwa alisahau kuzima taa kwa kutumia mfumo huu, anaweza kuzima taa hizo kwa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) bila ya kurudi nyumbani.”
Mwalimu Haule aliongeza kuwa mfumo huu unaleta urahisi kwa watumiaji kwa kuwa unamwezesha mtu kuwa na udhibiti wa vifaa vya umeme popote alipo lakini pia ni msaada mkubwa kwa watu wenye ulemavu wa viungo kwani huwapa uwezo wa kuendesha mifumo ya nyumbani bila kulazimika kwenda moja kwa moja kwenye swichi.
Mbali na kuongeza urahisi, amesema mfumo huu pia unasaidia kudhibiti matumizi ya umeme na kupunguza gharama. “Kwa mfano, unaweza ‘kufunga’ (lock) mfumo fulani wa umeme ambao hautaki utumike kwa muda husika,umeme utakuwepo lakini hautatumika hadi ufungue tena mfumo huo,” aliongeza.
Mradi huu unaonesha uwezo mkubwa wa wanafunzi wa NIT katika kuoanisha elimu na mahitaji halisi ya jamii. ni ishara njema kwa mustakabali wa teknolojia ya ndani ya nchi na inatoa matumaini ya maendeleo ya kiteknolojia yanayoendana na mazingira ya Kitanzania
No comments:
Post a Comment