RAIS Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi mbalimbali katika hafla ya utiaji saini mkataba wa usimamizi wa shughuli za lishe . |
NA JOYCE KASIKI,DODOMA
RAIS Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara
ya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum kuwatambua watoto wote
wanaoishi katika mazingira hatarishi ili Serikali iweze kuwasaidia kwa kuhakikisha wanalelewa,wanakua vizuri na kufukia utimilifu wao ambao utaleta tija katika maisha yao ya baadaye na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki Mtumba
katika hafla ya utiaji saini mkataba wa lishe kwa Wakuu wa mikoa hapa nchini.
“Pamoja na kuwekeza katika suala la lishe,
lakini tunafahamu kuwa wimbi la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi
linazidi kuwa kubwa “amesema Rais Samia
Amesema,mwaka 2021 jumla ya watoto
992,901 walitambuliwa na kupewa huduma mbalimbali za kukabiliana na lishe duni
na utapiamlo huku akihimiza kuendelea kutambuliwa kwa watoto hao ili kuimarisha
afua za ukuaji wao na waweze kufikia hatua timilifu za ukuaji.
“Kuna watoto wanaishi katika mazingira
magumu na kukua kwao kunakuwa kugumu hivyo hivyo, na hawa ndiyo wanakuja kuwa
wahalifu wa baadaye kwa sababu kama anaishi mazingira magumu atatoka mapema
nyumbani kwenda kujitafutia ,hana elimu hana namna yoyote lakini anakwenda kujitafutia,lazima wengi wao watakuwa
wezi,watakuwa na vitendo viovu halafu tunakuja kupiga kelele.”amesema na
kuongeza
“Gwajima (Waziri wa Maendeleo ya Jamii
,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum) hili la kwako,mkahakikishe watoto wanaoishi
mazingira magumu na hatarishi wanatambuliwa na tunawasaidia.”
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy
Mwalimu amesema lishe bora ni msingi wa afya na uchumi wa mtu mmoja mmoja ambapo
suala hili linapaswa kuzingatiwa kuanzia kwenye malezi na makuzi ya watoto ili
kueta tija kwa Taifa.
“Lishe mbovu inaleta utapiamlo ambao
unaleta madhara ya kiafya na kiuchumi na hivyo kuathiri maendeleo ya mtu
binafsi na jamii kwa ujumla ,lakini utapiamlo wa kuzidi au wa kupungua
virutubishi mwilini unapelekea magonjwa ya mara kwa mara na magonjwa yasiyo ya
kuambukiza na hivyo kuathiri kipato cha familia na sekta ya afya.
Aidha amesema,udumavu kwa watoto unasababisha
madhara ya kiakili na kimwili ya muda mrefu yanayoweza kupelekea magonjwa ya
mara kwa mara ,upungufu wa uelewa darasani hatimaye kuathiri uchumi wa nchi
hapo baadaye .
“Tunaweza tukadharau suala hili la lishe
tukawekeza kwenye barabara na vitu vingine ,lakini lazima tujue hivyo vikibomoka
tunaweza kupata fursa ya kukarabati ,lakini kwenye lishe na ubongo wa mtoto ,hatuna
fursa ya kukarabati baada ya miaka
mitano,kwa hiyo wakati wa kuwekeza kwa mtoto ni sasa na hapa tutapata Taifa
lenye watu wenye tija.”amesema
Hata hivyo amesema,nchi inaenda vizuri
katika suala la lishe huku akisema Tafiti za TDHS zinazotumika inaonyesha utapiamlo
,ukondefu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano umepungua kutoka asilimia 4.5 mwaka 2015/16
hadi kufikia asilimia 3.5 mwaka 2018.
Kuhusu upungufu wa damu kwa wanawake
wenye umri wa kuzaa umepungua kutoka asilimia 45 mwaka 2015/16 hadi asilimia 29
mwaka 2015/16 huku udumavu nao ukipungua kutoka asilimia 34 mwaka 2015/16 hadi
kufikia asilimia 32 mwaka 2018/19.
“Lakini sasa hapa kwenye udumavu ,maana
yake tunapozungumza asilimia 32,watoto wenye umri wa miaka mitano kwa mujibu wa
sensa ya mwaka 2012 ni kama takriban watoto milioni tisa kwa hiyo tunazungumza
watoto milioni tatu Tanzania wana udumavu,wamedumaa na hawafundishiki,
“Pia
watoto hawa hawaelewi,hawawezi kuwa wabunifu katika kufanya kazi na kuleta
maendeleo ya nchi ,tunaweza tukapishana huko mikoani,mawizarani lakini tayari
ubongo wa huyo mwenzetu ulishadumaa hauwezi kubadilikahauwezi kuingiza
vipya,hauwezi kuja na ubunifu wa mambo mapya.
Kutokana na hali hiyo amesema Wizara ya
Afya itaendelea na jukumu la kuandaa na kuto sera miongozo na mikakati ya afya
ikiwemo huduma za lishe na kuzifanyia kazi sera zilizopitwa na wakati kwa
maslahi mapana ya watoto hapa nchini na Taifa kwa ujumla.
Kuhusu kupunguza udumavu kwa watoto amesema
wataendelea kushirikiana na wadau wa lishe nchini kutekeleza afua za lishe
zenye matokeo makubwa zinazolenga siku 1000 za maisha ya mtoto ikiwemo utoaji
wa madini ya chuma na acid ya folic kwa akina mama wajawazito takriban kwa
akina mama wajawazito milioni 2.3 kwa mwaka.
Naibu Katibu Mkuu Afya Dkt.Grace Maghembe
amesema,mkakati uliowekwa ni kuwafikia wananchi ili waweze kuelewa suala hili
la lishe kwa kurejesha siku ya maadhimisho ya lishe ya kijiji ili iweze kuadhimishwa kwenye ngazi ya kijiji .
Vile vile amesema pia mpango ni
kuelimisha jamii kupitia wahudumu wa ngazi ya afya ya jamii na kufanya vikao
vya tathimini kwa ngazi ya kata na ngazi ya kijiji badala ya tathimini hizo
kufanyika katika ngazi ya mikoa na halmashauri lakini pia kutumia mitandao ya
kijamii ili elimu iweze kufika kwa jamii.