BAADHI ya wadau wanaotekeleza mradi wa Mtoto kwanza wakiwa katika kikao cha tathimini ya utekelezaji wa Mradi wa Mtoto kwanza kilichofanyika jijini Dodoma. |
NA JOYCE KASIKI,DODOMA
MKURUGENZI Msaidizi Ofisi ya Rais Tamisemi anayeshughulikia Serikali za Mitaa Stephan Motambi amesema, kushindwa kufanya vizuri kwenye utoaji huduma za malezi,makuzi na maendeleo ya awali kwa watoto, kunachangia kuwa na kundi kubwa la watoto waliokosa malezi bora ambao wanakwenda kuwa mzigo kwa familia na Taifa kwa siku za baadaye.
Akifungua kikao cha wadau wa malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto jijini Dodoma kilichoandaliwa na Mtandao wa Malezi na Makuzi ya Mtoto (TECDEN) Motambi amesema,hatua hiyo inasababisha kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kuhudumia watoto hao kuliko ambazo zingetumika katika malezi na makuzi yao.
“Sasa hivi tunahitaji kuajiri maafisa ustawi wengi ili wakashughulikie changamoto za watoto wa mitaani na fedha nyingi inatumika,lakini kama wangepata malezi mazuri wasingekuwepo mitaani na hivyo fedha zinazotumika kuwahudumia hivi sasa zingefanya kazi nyingine kwenye Taifa.”amesema Motambi
Kufuatia hali hiyo amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka sekretarieti za mikoa kumi iliyoanza kutekeleza mradi wa Mtoto Kwanza kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha watoto wanakua na kufikia utumilifu wao na hatimaye kuwa na tija kwa Taifa lao.
“Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka sekretarieti za mikoa kumi iliyoanza kutekeleza mradi wa Mtoto Kwanza lazima muone kuwa hii ni fursa ya kuonyesha umahiri wenu katika kutekeleza afua zinazohusu malezi ya watoto, na mara nyingi mlikuwa mkalamika kwamba hamna wadau au mradi wa kuwawezesha kuifikia jamii,
“Sasa mradi huu wa mtoto kwanza muutumie vizuri na mshiriki kikamilifu katika kuutekeleza kwa faida ya jamii na Taifa,kushindwa kufanikiwa kwa mradi huu kutasababishwa na sisi wenyewe kushindwa kutimiza majukumu yetu sawasawa ,kwa hiyo nawaomba maafisa wote ,mshiriki na mtoe matokeo ambayo ni kufanikiwa kwa utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM ).Amesema Motambi
Aidha amewataka watendaji wote
wanaofanya uratibu katika ngazi mbalimbali wahakikishe kwamba Programu hiyo
inatekelezwa kwa ufanisi ili dhima ya kuanzishwa kwa programu hiyo iweze
kufanikiwa.
Awali Mkurugenzi wa Mtandao wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN) Mwajuma Rwebangila amesema Mradi wa Mtoto kwanza unatekelezwa katika mikoa 26 Tanzania Bara ingawa kwa sasa wameanza na mikoa 10 ya Lindi ,Mbeya,Tabora,Dodoma,Rukwa,Manyara,Arusha,Morogoro,Dar es Salaam na Kagera .
Amesema,utekelezaji wa Mradi wa Mtoto kwanza umelenga katika kuchochea utekelezaji wa Programu Jumuishi ya MMMAM.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Action For Community Care (ACC) linalotekeleza mradi wa Mtoto kwanza mkoani Dodoma Pendo Maiseli amesema,mwelekeo unaonyesha mradi huo kuleta ufanisi katika utekelezaji wa PJT-MMMAM.
Amesema,kwa kipindi cha miezi minne tangu wapatiwe elimu ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto wao kama wadau wanaotekeleza mradi huo wamefanikiwa kuwakutanisha wadau kutoka mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali yanayofanya shughuli za watoto na kuwapa uelewa kuhusu elimu ya malezi ,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
“Vievile tumefanya uzinduzi wa PJT-MMMAM kwa mkoa wa Dodoma ambao umeshirikisha wadau wengi,pia tumefanikiwa kuwafikia na kutoa elimu hii kwa wazazi na walezi 328 ,haya ni mafanikio kwetu ambayo tunaona ni mwelekeo mzuri katika utekelezaji wa Programu ya Taifa ya MMMAM.”amesema Maiseli
Akielezea kuhusu changamoto
amesema,bado wananchi hawana uelewa wa kutosha kuhusu suala la malezi,makuzi na
maendeleo ya mtoto huku akisema bado wadau wana kazi kubwa ya kutoa elimu kwa
jamii kuhusu suala hilo.
No comments:
Post a Comment