Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Keptain Mstaafu George Mkuchika akizundua Mwongozo wa Mpango ,Bajeti na Taarfa za Ustawi wa Jamii katika Ngazi za Serykali za Mitaa jijini Dodoma |
NA JOYCE KASIKI,DODOMA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezindua Mwongozo wa Kitaifa wa Mpango,Bajeti na Taarifa za Ustawi wa Jamii katika ngazi za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa unaolenga kuhakikisha kuwa afua zote zinazolenga masuala ya Ustawi wa Jamii zinapangiwa mipango na bajeti stahiki kulingana na mahitaji halisi.
Aidha ameziagiza Wizara za kisekta zinazohusika katika utekelezaji wa Mwongozo huo kuhakikisha zinasimamia urasimishwaji na utekelezaji wa Mwongozo huo.
Akizundua mwongozo huo kwa niaba ya Waziri Mkuu Majaliwa,Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Kazi Maalum Kaptein George Mkuchika amesema,mwongozo huo umekuja kutokana na mabadiliko ya kijamii,kiuchumi ,kiutamaduni kisiasa na kimazingira ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la wahitaji wa huduma za ustawi wa Jamii.
Amesema mabadiliko hayo yamesababisha kuibuka kwa watu wenye mahitaji maalum ambao kimsingi wanahitaji huduma mbalimbali za ustawi wa Jamii.
“Kwa muktadha huo Serikali imeona umuhimu wa kuwa na mwongozo mahsusi utakaosaidia katika ukusanyaji wa takwimu ,upangaji wa bajeti na utoaji wa taarifa za huduma za Ustawi wa Jamii katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.”amesema Kaptein Mkuchika
Waziri huyo amesema manufaa ya Mwongozo huo ni pamoja na kusaidia katika upangaji mipango ,bajeti pamoja na upatikanaji wa taarifa mbalimbali zinazowahusu watoto ,watu wenye ulemavu,wazee na makundi maalum na hivyo kujenga mustakabali imara wa jamii ya kitanzania katika kufikia matarajio yao.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amesema, mwongozo huo utasadia kuimarisha utoaji wa huduma kwa Makundi Maalum ikiwemo Wazee, Walemavu, Watu wenye magonjwa sugu, Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na makundi mengine yenye mahitaji maalum.
‘‘Ni imani yangu kuwa utekelezaji wa Mwongozo huu utachochea kasi ya utoaji na upatikanaji wa huduma bora za Ustawi wa Jamii kwa Makundi Maalum na hivyo kujenga mustakabali imara wa jamii za Kitanzania katika kufikia matarajio yao.”amesema Dkt.Gwajima
Aidha Waziri Gwajima amesema Mwongozo huu ambao ni nyenzo muhimu ya uratibu, usimamizi na utekelezaji wa Mipango, Bajeti na Taarifa za Huduma za Ustawi wa Jamii katika ngazi za Halmashauri.
Wizara zinazohusika katika utekelezaji wa Mwongozo huo ni Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum,Wizara ya Afya,Katiba na Sheria,Wizara ya Fedha na Mipango,Wizara ya Elimu ,Sayansi na Tenolojia na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
No comments:
Post a Comment