|
PICHANI ni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizindua mpango wa Bima ya Afya wa Watoto mwaka 2017
|
Na Joyce Kasiki
KATIKA Taifa la
Tanzania tukizungumzia neno mtoto kila mmoja anafahamu kuwa ni mtu mwenye umri
wa chini ya miaka 18, hata kama ameanza kujitegemea lakini bado anahesabika
kama ni mtoto.
Tafsiri hii imetokana
na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, Mkataba wa Afrika kuhusu haki na
Ustawi wa Mtoto, Sera ya Maendeleo ya Mtoto na Sheria ya Mtoto Na. 21
ya 2009.
Lakini leo makala hii
inamzungumzia mtoto wa miaka 0 – 8 ambaye kitaalam inaonesha kuwa katika umri
huo ubongo wa mtoto unakua kwa asilimia 80-90 na kuanzia miaka tisa kuendelea
ndio ubongo unakua kwa asilimia 10 zilizobakia na kufikia asilimia 100.
Aidha kundi hilo la
watoto lilisahaulika katika kuhakikisha linapata afua stahiki ili kuwezesha ubongo
kukua inavyotakiwa na hivyo kumwezesha mtoto kukua hadi kufikia utimilifu wake
hali iliyofanya serikali kwa kushirikiana na wadau kuanzisha
Programu Jumuishi ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM
2021/22-2025/26)iliyolenga kutatua changamoto za ukuaji na maendeleo ya watoto
wa umri huo .
Pia Programu hiyo
itatoa mcango katika kufanikisha mpango wa tatu wa Taifa wa Maendeleo wa miaka
mitano 2021/22-2025/26 kwa kutambua kwamba watoto ambao wanakosa kufikia
kikamilifu hatua za ukuaji ni changamoto kwa maendeleo ya Taifa.
Mambo muhimu ya
kuzingatia kwa mtoto ni kuhakikisha upatikanaji Programu jiyo imelenga kuwekeza
moja kwa moja kwenye maendeleo ya watu ili kuharakisha upatikanaji wa matokeo
chanya ya maendeleo ya awali ya mtoto kwa kuhimiza ushiriki wa sekta mbalimbali
katika kutoa huduma za malezi jumuishi yenye vipengele vitano ambavyo ni Afya
bora,lishe ya kutosha tangu ujauzito,ujifunzaji wa awali,malezi yenye mtikio na
ulinzi na usalama na kuwa Taifa lenye watu wenye tija hapo baadaye.
Moja ya mambo
yanayofanywa na serikali katika kuhakikisha mtoto anakua vizuri ni pamoja na
utoaji wa huduma za afya ambapo katika kumlinda mtoto dhidi ya magonjwa
ilianzisha utaratibu wa Bima ya Afya ya Mtoto’Toto Afya Kadi’iliyokatwa kwa
gharama ya shilingi 50,400 ambayo ilirahisisha upatikanaji wa huduma bora za
afya kwa mtoto kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Nikimnukuu Waziri wa
Afya Ummy Mwalimu wakati akizindua mpango huo mwaka 2017 alisema’ Kampeni hii
iwe endelevu kwa nchi nzima ili watoto wote wawe na Bima ya Afya,hapo tutakuwa
tunajenga Taifa lenye msingi bora wa afya’,ambapo kwa kauli hiyo kulikuwa na
mwitikio mkubwa wa wazazi kukata bima za afya za watoto wao.
Licha ya kuwa kadi
hiyo ina msaada mkubwa kwa watoto wote wenye umri wa miaka 0 hadi 18 lakini kwa
watoto wa kati ya miaka 0-8 ina umuhimu mkubwa zaidi kwani ndio wakati ambao
msingi wa afya bora ya mtoto unapaswa kujengwa.
Hata hivyo kwa sababu
ambazo hazijaeleweka na wananchi,Machi mwaka huu serikali iliamua kusitisha au
kubadili mfumo wa upatikanaji wa kadi hiyo ambapo hivi sasa umewalenga zaidi
watoto waliopo shuleni huku ambao hawajaanza shule kwa sababu mbalimbali wakiwa
wamesahaulika hatua ambayo imelalamikiwa na wazazi na walezi.
Wakizungumza katika Makala
hii baadhi ya wazazi na walezi wameiangukia serikali kuiomba serikali kurudisha
utaratibu wa watoto kupata huduma za afya kupitia mpango wa Afya Toto Kadi na
bila vikwazo ili kuwawezesha watoto wengi zaidi kujiunga na mpango huo na
kupata huduma za matibabu kwa urahisi.
Kwa mujibu wa Sera ya
Afya ya 2007 ,huduma za afya kwa mama wajawazito na watoto chini ya miaka
mitano hutolewa bure kwa lengo la kuboresha afya ya mtoto kabla na baada ya
kuzaliwa mpaka anapofikisha miaka mitano.
Wananchi hao
wamesema,kitendo cha serikali kuondoa utaratibu wa watoto kutibiwa kupitia bima
hiyo,imekuwa changamoto kwao baada ya kadi walizokuwa wakitumia kuisha muda
wake na hivyo ushindwa uendeea upata matibabu .
Saida Issa mkazi wa
Nkuhungu jijini Dodoma ni mmoja wa
wazazi aliyekuwa amemkatia mwanae kadi hiyo anasema,utaratibu uliopo hivi
sasa ambao umetangazwa na serikali kwamba mtoto atapata kadi hiyo kupitia
shule,unawanyima haki watoto wengine hasa wale ambao bado hawajafikia umri wa
kwenda shule.
“Kimsingi tunaiomba
serikali irudishe utaratibu wa zamani wa watoto wote kupata kadi hiyo kwa
gharama ya sh.50,400 bila masharti yoyote maana ulikuwa ni utaratibu rahisi
uliowawezesha kupata huduma za afya katika hospitali zote nchini,utaratibu
uliopo ni wa masharti ambao uleta ugumu kwa watoto kupata matibabu.”anasema
Saida
Anaongeza kuwa”Hata
utaratibu ambao umeelezwa kwenye sera ya afya kwamba watoto wenye umri wa miaka
mitano kushuka chini watatibiwa bure,bado hauna tija sana kwa sababu unaweza
kumpeleka mtoto hospitali akaambulia vipimo tu na dawa zote akahitajika
kwenda kununua nje kwenye maduka ya dawa ya watu binafsi.”
Ramadhani Juma Mkazi
wa Mailimbili anasema,hata utaratibu uliotangazwa na serikali kwamba mtoto
atapata kadi ya matibabu kupitia shule bado siyo rasmi kwa sababu huko shuleni
kwenyewe hakuna mwongozo wowote rasmi unaoelekeza kuhusu suala hilo hali
inayoleta sintofahamu kwa wazazi na walezi.
“Lakini pia imesema
watoto watapata kadi kupitia kadi za vifurushi za wazazi,hili nalo bado changamoto
maana wazazi wengi ambao hawapo kwenye utumishi wa umma hawana hizo kadi
kutokana na kushindwa kumudu gharama za uchangiaji ,familia nyingi walikuwa
wameamua kuwekeza kwenye afya za watoto kwa kuwakatia kadi hizo kutokana na
changamoto za kiafya zilizopo kwa watoto.”anasema na kuongeza kuwa
“Hivyo tunaiomba
serikali iliangalie upya suala hili na irudishe utaratibu uliokuwa mwanzo wa
kadi kukatwa kwa mtoto mmoja mmoja na siyo kupitia kikundi cha idadi fulani ya
watoto.”anasema mzazi huyo
Mkurugenzi wa Shirika
lisilo la Kiserikali la Mimi ni Taa Girls Foundation ,linaloshirikiana na Asasi
mbalimbali katika mkoa wa Dodoma katika utekelezaji wa Mradi kwanza
unaopelekea utekelezaji wa PJT-MMMAM Dorcas Shayo anasema, ni lazima kila mmoja
afahamu kwanza ustawi wa mtoto unaanza na afya ndio maana kumekua na
uhamasishaji wa akina mama kujifungulia kwenye vituo vya afya.
“Hii ni kwa sababu
tunaamini katika afya ili mtoto akue vizuri lazima kuwe na mazingira
rafiki kati ya mtoto na mama na huduma za afya hivyo basi, kuweka vikwazo
vyovyote vinavyoweza kusababisa mtoto kuwa mbali na huduma za afya ni kupoteza
kabisa ukuaji wenye afya bora kwa mtoto”amesema shayo
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa shule ya msingi Capital (Capital Pre and Primary School)
Khan Charokiwa anasema wao kama shule walipata taarifa kuhusu watoto
kuandikishwa kadi za bima shuleni lakini wameshindwa kuandikisha watoto
kutokana na wengi wao kuwa na bima za wazazi wao.
“Taarifa ambayo
tuliipata kutoka NHIF ni kwamba ili shule ikidhi vigezo vya kuandikisha ,idadi
ya watoto inatakiwa ifikie 100 ,sasa sisi pale shuleni watoto wengi wana bima
za wazazi wao na ambao hawana ni wachache.”anasema Khan
Kwa upande wake Mganga
Mkuu wa Jiji la Dodoma Dkt.Andrew Method amesema,katika hospitali za jiji la
Dodoma watoto wanaendelea kutibiwa kwa kufuata miongozo na sera ya afya ambayo
inataka watoto walio na umri chini ya miaka mitano kutibiwa bure.
Akizungumza hivi
karibuni Bungeni jijini Dodoma Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel amekiri
kubadilika kwa mfumo wa kulipia watoto kupitia Toto Afya Kadi umebadilika huku
akisema, kwa sasa kadi za matibahu za watoto hukatwa kupitia shule na vifurushi
vya Bima ya Afya vya Najali,Wekeza na Timiza ambavyo hukatwa kifamilia hivyo na
watoto kujumuishwa humo.
Pia akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam Septemba 25,2023 Dkt.Mollel
anasema,kuna idadi ndogo ya watoto walio chini ya miaka 18 waliopata toto Afya
kadi ambao ni 210,000 tu kati ya watoto milioni 31 walio na umri chini ya miaka
18.
Anasema,tangu
kuanzishwa kwa mpango huo watoto 210,000 wameshatumia kiasi cha shilingi
bilioni 40 wakati michango yao ni shilingi bilioni 5 tu.
Hata hivyo kwa mujibu
wa Mwongozo wa Programu Jumuishi wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya
Mtoto (PJT-MMMAM 2021/22-2025/26),kuna tafiti chache kuhusiana na masuala ya Malezi,Makuzi na
Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) ambazo zimefanyika kwa ngazi ya Taifa ambapo
tafiti za kisayansi duniani zinasisitiza kwamba msingi imara wa mtoto unatakiwa
ujengwe katika miaka ya awali ya mtoto na kwamba huu ndiyo wakati muhimu wa
kuwekeza maisha ya mwanadamu.
“Imedhihirika kuwa kwa
kila dola moja iliyotumika katika afua za MMMAM kuna matokeo makubwa
yanayopatikana yanayokadiriwa kufikia dola za kimarekani 17.”imesema sehemu ya
Mwongozo huo.
Hata hivyo ,suluhisho
la kudumu la tatizo hili ni kukamilika kwa muswada wa sheria ya Bima ya Afya
kwa Wote ambao tunaamini utawezesha watoto wengi zaidi wasio na changamoto na
wenye changamoto za kiafya kulipiwa huduma za matibabu kupitia Bima ya
Afya kwa wote.”anasema Dkt.Mollel
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri huyo,hatua hiyo itapelekea kuwepo kwa uhai na uendelevu wa mfuko wa Bima
ya Afya wa Taifa huku akisema,serikali imeshaanza kupeleka elimu shuleni kuhusu
utaratibu wa wazazi kuwakatia watoto wao kadi za matibu kupitia shule.
Ikumbukwe kuwa toto
Afya kadi ilikuwa inatoa fursa Kwa watoto walio na umri wa kuanzia miaka 0hadi
18 kutibiwa kwa gharama sh 50,400 kwa mwaka mzima hivyo
kuleta unafuu kwa wazazi/walezi kuwakata kadi hizo na hivyo kurahisisha
upatikanaji wa matibabu na huduma Bora za Afya kwa watoto waliokiwa na kadi
hizo.
Hata hivyo utaratibu
huo wa Toto Afya Kadi ulioanzishwa 2017 umeondolewa mwanzoni mwa mwaka
huu huku ikielezwa kuwa watoto wakatiwe kadi za matibabu kupitia kadi za
vifurushi za wazazi wao au kupitia shule wanazosoma hatua ambayo imeelezwa na
wananchi wengi kwamba inaleta changamoto katika upatikanaji wa huduma za Afya
kwa watoto hususan wenye umri wa miaka sifuri Hadi minane kundi ambalo pamoja
na Afya nyingine,linahitaji kupata huduma Bora za Afya na uhakika kwa ajili ya
ukuaji timilifu wa ubongo na ukuaji wao kwa ujumla.