Na Joyce Kasiki,Geita
MAABARA ya upimaji wa sampuli za Madini (MSALABS) yenye Makao Makuu yake nchini Canada , imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 5 za kitanzania kwa ajili ya upimaji wa sampuli hizo kwa kiwango cha Kimataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Maabara hiyo Mugisha Lwekoramu amesema hayo Septemba 27, 2023 Mbele ya Waziri wa Madini Anthony Mavunde wakati wa uwekeaji wa jiwe la msingi wa maabara hiyo iliyojengwa katika halmashauri ya Mji wa Geita ,mkoani Geita.
Lwekoramu amesema Maabara hiyo inatumia teknolojia ya kisasa ya upimaji wa sampuli kwa kutumia mionzi ambayo pia husaidia katika utunzaji wa mazingira tofauti na teknolojia ya awali ya kutumia kemikali na moto lakini pia hutoa majibu kwa muda mfupi.
“Maabara hii inatumia teknlojia ya kisasa ya upimaji wa madini kwa mionzi ambayo ni rafiki hata kwa mazingira yetu maana haitumii kemikali wala moto katika upimaji na hutoa majibu ya ufanisi mkubwa,
“Pia Teknolojia humwezesha mteja kupata ,majibu ya sampuli ndani ya muda mfupi sana ukilinganisha teknolojia za zamani za kutumia moto na kemikali ambazo majibu huchukua siku kadhaa ikiwemo uwezekano wa kuwa na makossa ya kibinadamu na mwisho wa upimaji sampuli huwa imeharibika kabisa,kwa hiyo teknolohjia hii ya kisasa baada ya upimaji kukamilika mteja ana uhuru wa kuondoka na sampuli iliyo katika ubora wake wa awali .”amesema Lwekoramu na kuongeza kuwa
“Kwa kufanya hivi tunategemea ongezeko la tija katika uzalishaji wa madini ambao utasaidia kipato cha uchumi wetu na kipato cha serikali kwa ujumla”
Aidha amesema,kwa asilimia 99.8 ya wafanyakazi wa maabara hiyo ni watanzania ambapo matarajio yao ni watanzania hao kujifunza teknolojia hiyo ya kisasa ili waweze kueneza ujuzi wa teknolojia hiyo hapa nchini kwa kadri teknolojia jiyo itakavyoendelea kukua.
Amesema maabara hiyo inatarajiwa kufunguliwa rasmi na kuanza kutoa huduma Novemba mwaka huu na itajikita katika upimaji wa madini ya dhahabu ,Shaba na Fedha .
Pia amesema wana malengo ya kupanua wigo wa biashara yao na wamedhamiria kufungua maabara nyingine katika mkoa huo wa Geita yenye uwezo wa kupima sampuli za madini ya aina zote lakini pia kufungua matawi mengine Kusini mwa Tanzania itakayopima madini ya Graphite.
Amesema uwekezaji huo umefanyika kutokana na juhudi za Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya uwekezji nchini.
Akizungumza katika hadhara hiyo Waziri wa Madini Anthony Mavunde amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Maabara kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini unaoendana na Dunia ya sasa ya Sayansi na teknolojia lakini pia kwa kusogeza huduma hiyo katika eneo husika na wakati muafaka.
Kwa mujibu wa Mavunde,Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kushirikiana nao ili wadau katika sekta ya madini waweze kupata huduma yao , akiwataka kuendelea kufungua matawi mengine nchini.
“Kwa niaba ya Serikali nataka niwahakikishie kwamba sisi tunaunga mkono matumizi ya teknolojia ya kisasa na tutaendelea kutoa ushirikiano kwenu kwa sababu tunajua huduma zetu zinawagusa wadau wetu na tutakuwa tayari pale ambapo mtahitaji msaada wetu tutakuwa tayari kushirikiana nanyi.”amesisitiza Mavunde
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Sheigela amesema uwekezaji huo ni kutokana na ukweli uliopo kwamba nchi ina Rais anayesimamia na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji .
No comments:
Post a Comment