PICHANI ni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizindua mpango wa Bima ya Afya wa Watoto mwaka 2017
Na Joyce Kasiki
KATIKA Taifa la Tanzania tukizungumzia neno mtoto kila mmoja anafahamu kuwa ni mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18, hata kama ameanza kujitegemea lakini bado anahesabika kama ni mtoto.
Tafsiri hii imetokana na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, Mkataba wa Afrika kuhusu haki na Ustawi wa Mtoto, Sera ya Maendeleo ya Mtoto na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009.
Lakini leo makala hii inamzungumzia mtoto wa miaka 0 – 8 ambaye kitaalam inaonesha kuwa katika umri huo ubongo wa mtoto unakua kwa asilimia 80-90 na kuanzia miaka tisa kuendelea ndio ubongo unakua kwa asilimia 10 zilizobakia na kufikia asilimia 100.
Aidha kundi hilo la watoto lilisahaulika katika kuhakikisha linapata afua stahiki ili kuwezesha ubongo kukua inavyotakiwa na hivyo kumwezesha mtoto kukua hadi kufikia utimilifu wake hali iliyofanya serikali kwa kushirikiana na wadau kuanzisha Programu Jumuishi ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM 2021/22-2025/26)iliyolenga kutatua changamoto za ukuaji na maendeleo ya watoto wa umri huo .
Pia Programu hiyo itatoa mcango katika kufanikisha mpango wa tatu wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano 2021/22-2025/26 kwa kutambua kwamba watoto ambao wanakosa kufikia kikamilifu hatua za ukuaji ni changamoto kwa maendeleo ya Taifa.
Mambo muhimu ya kuzingatia kwa mtoto ni kuhakikisha upatikanaji Programu jiyo imelenga kuwekeza moja kwa moja kwenye maendeleo ya watu ili kuharakisha upatikanaji wa matokeo chanya ya maendeleo ya awali ya mtoto kwa kuhimiza ushiriki wa sekta mbalimbali katika kutoa huduma za malezi jumuishi yenye vipengele vitano ambavyo ni Afya bora,lishe ya kutosha tangu ujauzito,ujifunzaji wa awali,malezi yenye mtikio na ulinzi na usalama na kuwa Taifa lenye watu wenye tija hapo baadaye.
Moja ya mambo yanayofanywa na serikali katika kuhakikisha mtoto anakua vizuri ni pamoja na utoaji wa huduma za afya ambapo katika kumlinda mtoto dhidi ya magonjwa ilianzisha utaratibu wa Bima ya Afya ya Mtoto’Toto Afya Kadi’iliyokatwa kwa gharama ya shilingi 50,400 ambayo ilirahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa mtoto kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Nikimnukuu Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akizindua mpango huo mwaka 2017 alisema’ Kampeni hii iwe endelevu kwa nchi nzima ili watoto wote wawe na Bima ya Afya,hapo tutakuwa tunajenga Taifa lenye msingi bora wa afya’,ambapo kwa kauli hiyo kulikuwa na mwitikio mkubwa wa wazazi kukata bima za afya za watoto wao.
Licha ya kuwa kadi hiyo ina msaada mkubwa kwa watoto wote wenye umri wa miaka 0 hadi 18 lakini kwa watoto wa kati ya miaka 0-8 ina umuhimu mkubwa zaidi kwani ndio wakati ambao msingi wa afya bora ya mtoto unapaswa kujengwa.
Hata hivyo kwa sababu ambazo hazijaeleweka na wananchi,Machi mwaka huu serikali iliamua kusitisha au kubadili mfumo wa upatikanaji wa kadi hiyo ambapo hivi sasa umewalenga zaidi watoto waliopo shuleni huku ambao hawajaanza shule kwa sababu mbalimbali wakiwa wamesahaulika hatua ambayo imelalamikiwa na wazazi na walezi.
Wakizungumza katika Makala hii baadhi ya wazazi na walezi wameiangukia serikali kuiomba serikali kurudisha utaratibu wa watoto kupata huduma za afya kupitia mpango wa Afya Toto Kadi na bila vikwazo ili kuwawezesha watoto wengi zaidi kujiunga na mpango huo na kupata huduma za matibabu kwa urahisi.
Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya 2007 ,huduma za afya kwa mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano hutolewa bure kwa lengo la kuboresha afya ya mtoto kabla na baada ya kuzaliwa mpaka anapofikisha miaka mitano.
Wananchi hao wamesema,kitendo cha serikali kuondoa utaratibu wa watoto kutibiwa kupitia bima hiyo,imekuwa changamoto kwao baada ya kadi walizokuwa wakitumia kuisha muda wake na hivyo ushindwa uendeea upata matibabu .
Saida Issa mkazi wa Nkuhungu jijini Dodoma ni mmoja wa wazazi aliyekuwa amemkatia mwanae kadi hiyo anasema,utaratibu uliopo hivi sasa ambao umetangazwa na serikali kwamba mtoto atapata kadi hiyo kupitia shule,unawanyima haki watoto wengine hasa wale ambao bado hawajafikia umri wa kwenda shule.
“Kimsingi tunaiomba serikali irudishe utaratibu wa zamani wa watoto wote kupata kadi hiyo kwa gharama ya sh.50,400 bila masharti yoyote maana ulikuwa ni utaratibu rahisi uliowawezesha kupata huduma za afya katika hospitali zote nchini,utaratibu uliopo ni wa masharti ambao uleta ugumu kwa watoto kupata matibabu.”anasema Saida
Anaongeza kuwa”Hata utaratibu ambao umeelezwa kwenye sera ya afya kwamba watoto wenye umri wa miaka mitano kushuka chini watatibiwa bure,bado hauna tija sana kwa sababu unaweza kumpeleka mtoto hospitali akaambulia vipimo tu na dawa zote akahitajika kwenda kununua nje kwenye maduka ya dawa ya watu binafsi.”
Ramadhani Juma Mkazi wa Mailimbili anasema,hata utaratibu uliotangazwa na serikali kwamba mtoto atapata kadi ya matibabu kupitia shule bado siyo rasmi kwa sababu huko shuleni kwenyewe hakuna mwongozo wowote rasmi unaoelekeza kuhusu suala hilo hali inayoleta sintofahamu kwa wazazi na walezi.
“Lakini pia imesema watoto watapata kadi kupitia kadi za vifurushi za wazazi,hili nalo bado changamoto maana wazazi wengi ambao hawapo kwenye utumishi wa umma hawana hizo kadi kutokana na kushindwa kumudu gharama za uchangiaji ,familia nyingi walikuwa wameamua kuwekeza kwenye afya za watoto kwa kuwakatia kadi hizo kutokana na changamoto za kiafya zilizopo kwa watoto.”anasema na kuongeza kuwa
“Hivyo tunaiomba serikali iliangalie upya suala hili na irudishe utaratibu uliokuwa mwanzo wa kadi kukatwa kwa mtoto mmoja mmoja na siyo kupitia kikundi cha idadi fulani ya watoto.”anasema mzazi huyo
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Mimi ni Taa Girls Foundation ,linaloshirikiana na Asasi mbalimbali katika mkoa wa Dodoma katika utekelezaji wa Mradi kwanza unaopelekea utekelezaji wa PJT-MMMAM Dorcas Shayo anasema, ni lazima kila mmoja afahamu kwanza ustawi wa mtoto unaanza na afya ndio maana kumekua na uhamasishaji wa akina mama kujifungulia kwenye vituo vya afya.
“Hii ni kwa sababu tunaamini katika afya ili mtoto akue vizuri lazima kuwe na mazingira rafiki kati ya mtoto na mama na huduma za afya hivyo basi, kuweka vikwazo vyovyote vinavyoweza kusababisa mtoto kuwa mbali na huduma za afya ni kupoteza kabisa ukuaji wenye afya bora kwa mtoto”amesema shayo
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shule ya msingi Capital (Capital Pre and Primary School) Khan Charokiwa anasema wao kama shule walipata taarifa kuhusu watoto kuandikishwa kadi za bima shuleni lakini wameshindwa kuandikisha watoto kutokana na wengi wao kuwa na bima za wazazi wao.
“Taarifa ambayo tuliipata kutoka NHIF ni kwamba ili shule ikidhi vigezo vya kuandikisha ,idadi ya watoto inatakiwa ifikie 100 ,sasa sisi pale shuleni watoto wengi wana bima za wazazi wao na ambao hawana ni wachache.”anasema Khan
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma Dkt.Andrew Method amesema,katika hospitali za jiji la Dodoma watoto wanaendelea kutibiwa kwa kufuata miongozo na sera ya afya ambayo inataka watoto walio na umri chini ya miaka mitano kutibiwa bure.
Akizungumza hivi karibuni Bungeni jijini Dodoma Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel amekiri kubadilika kwa mfumo wa kulipia watoto kupitia Toto Afya Kadi umebadilika huku akisema, kwa sasa kadi za matibahu za watoto hukatwa kupitia shule na vifurushi vya Bima ya Afya vya Najali,Wekeza na Timiza ambavyo hukatwa kifamilia hivyo na watoto kujumuishwa humo.
Pia akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam Septemba 25,2023 Dkt.Mollel anasema,kuna idadi ndogo ya watoto walio chini ya miaka 18 waliopata toto Afya kadi ambao ni 210,000 tu kati ya watoto milioni 31 walio na umri chini ya miaka 18.
Anasema,tangu kuanzishwa kwa mpango huo watoto 210,000 wameshatumia kiasi cha shilingi bilioni 40 wakati michango yao ni shilingi bilioni 5 tu.
Hata hivyo kwa mujibu wa Mwongozo wa Programu Jumuishi wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM 2021/22-2025/26),kuna tafiti chache kuhusiana na masuala ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) ambazo zimefanyika kwa ngazi ya Taifa ambapo tafiti za kisayansi duniani zinasisitiza kwamba msingi imara wa mtoto unatakiwa ujengwe katika miaka ya awali ya mtoto na kwamba huu ndiyo wakati muhimu wa kuwekeza maisha ya mwanadamu.
“Imedhihirika kuwa kwa kila dola moja iliyotumika katika afua za MMMAM kuna matokeo makubwa yanayopatikana yanayokadiriwa kufikia dola za kimarekani 17.”imesema sehemu ya Mwongozo huo.
Hata hivyo ,suluhisho la kudumu la tatizo hili ni kukamilika kwa muswada wa sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambao tunaamini utawezesha watoto wengi zaidi wasio na changamoto na wenye changamoto za kiafya kulipiwa huduma za matibabu kupitia Bima ya Afya kwa wote.”anasema Dkt.Mollel
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo,hatua hiyo itapelekea kuwepo kwa uhai na uendelevu wa mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa huku akisema,serikali imeshaanza kupeleka elimu shuleni kuhusu utaratibu wa wazazi kuwakatia watoto wao kadi za matibu kupitia shule.
Ikumbukwe kuwa toto Afya kadi ilikuwa inatoa fursa Kwa watoto walio na umri wa kuanzia miaka 0hadi 18 kutibiwa kwa gharama sh 50,400 kwa mwaka mzima hivyo kuleta unafuu kwa wazazi/walezi kuwakata kadi hizo na hivyo kurahisisha upatikanaji wa matibabu na huduma Bora za Afya kwa watoto waliokiwa na kadi hizo.
Hata hivyo utaratibu
huo wa Toto Afya Kadi ulioanzishwa 2017 umeondolewa mwanzoni mwa mwaka
huu huku ikielezwa kuwa watoto wakatiwe kadi za matibabu kupitia kadi za
vifurushi za wazazi wao au kupitia shule wanazosoma hatua ambayo imeelezwa na
wananchi wengi kwamba inaleta changamoto katika upatikanaji wa huduma za Afya
kwa watoto hususan wenye umri wa miaka sifuri Hadi minane kundi ambalo pamoja
na Afya nyingine,linahitaji kupata huduma Bora za Afya na uhakika kwa ajili ya
ukuaji timilifu wa ubongo na ukuaji wao kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment